Chama Afunguka "Watoto Wangu Wamenirudisha Msimbazi"




“WANANGU ni moja ya sababu iliyonirudisha kucheza soka la kulipwa Tanzania.” Hiyo ni kauli ya kiungo fundi wa mpira, Clatous Chama aliyerejea Simba, baada ya kutowekwa kwa siku zisizopungua 150 tangu auzwe RS Berkane ya Morocco.

Chama aliuzwa Agosti mwaka jana wakati Simba ikiwa kambini nchini Morocco, lakini ndoto na akili yake ilionekana kuwa Msimbazi.

Ubora wa Chama ndani ya uwanjani ni sababu pia iliyowafanya mabosi wa Simba kumrejesha baada ya kocha Mkuu Pablo Franco kupitisha urejeo wake na kupitia mahojiano maalum ya kwanza yaliyowekwa na mtandao wa klabu yake Chama kafunguka;

FAMILIA YAMREJESHA DAR

Katika mahojiano hayo, Chama aliwesema watoto wake wamechagia kurudi kukipiga Simba kwa mara nyingine kwa kuwa Tanzania ni nchi inayopendwa na wanae hao.


“Najisikia vizuri sana, kurudi Simba, nilipokuwa Zambia niliwauliza wanangu mko tayari kurudi Tanzania, walifurahi na kuniambia baba tuko tayari kurudi Tanzania,” anasema Chama.

MZUKA WA MASHABIKI

Chama anasema mashabiki wa Simba na wao ni moja ya urejeo wake Simba kutokana na namna ambavyo alikuwa akipokea meseji zao kila uchao wakimtaka kurejea.

“Ni ndoto ambayo nilikuwa nikiiota kurudi Simba, nimepata meseji nyingi kutoka kwa mashabiki wa Simba nikaona ni vyema kuja, na ni timu ambayo nimefanya makubwa kupitia wao, najisikia vizuri kurudi hapa,” anasema Chama.


“Sio suprise kurudi Simba, sema namna ambavyo wameishi na mimi ndio maana nimerejea, na mimi naipenda Simba na najiona ni sehemu ya Simba,” anabainisha Chama na kuongeza;

“Mimi nawakubali sana mashabiki na wanasimba wote, kazi yangu ni kuwapa kile ambacho wanakihitaji naamini wanahitaji kuwafanya watambe na mimi nimerejea kwa kushirikiana na wenzangu tutafanya.”

ATETA NA MAGORI

Miongoni mwa vigogo ambao Chama alikuwa akiwasiliana nao kila mara ni Crescentius Magori na Mzambia huyo anakiri alimweleza anaamini malengo watayafikia.

“Nilimwambia Magori ndoto zangu bado zipo na Simba kuona inafikia malengo yake makubwa ndio maana nimechagua kurudi ni sehemu ambayo ninafuraha kuwepo,” anasema.


PABLO AMPOKEA

Kocha wa Simba, Pablo Franco ni miongoni mwa waliopendekeza Chama arejee Msimbazi baada ya kufuatilia video zake mbalimbali wakati akiwa na timu hiyo.

“Kocha amenipokea na kunikubali na ananihitaji kwenye mipango yake na kanipokea vizuri, ni baba mzuri... jana tulikuwa tunataniana, akiniambia nisijekuwa kama Chico (mmoja wa watu wa idara ya habari ya Simba), nimeona ni kocha mzuri na nitafurahi kufanya naye kazi,” anasema.

KIWANGO CHAKE

Hakuna mwanasimba mwenye hofu na kiwango cha Chama, kutokana na mchango wake mkubwa ndani ya kikosi hicho, licha ya kuondoka sambamba Luis Miquissone.

Chama anasema, katika maisha yake hapendi kujizungumzia sana nini anakifanya uwanjani, ila anapedna kuiacha miguu yake iongee na wanaomtaza wamuongelee.


“Naamini watu wataona nini nitakifanya ndani ya uwanja, na nitafanya kadri ya uwezo wangu,” anasisitiza Chama.

“Niliondoka Simba nilivikosa vitu vingi, kuanzia ukaribu na wanasimba namna nilivyoishi na wenzangu na mambo mengine mengi,” anasema na kuongeza kuwa amefurahi kurudi nyumbani.

Aliwataja Shomary Kapombe na Hassan Dilunga kuwa ni miongoni mwa wachezaji waliokuwa wakimpigia na kuongea naye kila mara na amefurahi kujumuika nao tena.

Kuhusu michuano ya Kombe la Mapinduzi ambayo Simba imetwaa, Chama anasema;

“Nawapongeza wachezaji wenzangu kwa kazi nzuri ambayo wameifanya katika michuano ya Mapinduzi kwa kulitwaa taji hilo, ni huo ni mzuri kipindi kilichopita nilikuwepo na tulikosa, binafsi kama mchezaji nimefurahi sana kuona wachezaji wenzangu wamechukua kombe hilo.”


AKABIDHIWA TUZO

Licha ya kuwa ameondoka nchini, lakini msimu ulipita baada ya kumalizika aliibuka kiungo bora wa msimu, tuzo iliyopokelewa na uongozi wake na jana kukabidhiwa rasmi na Msemaji wa klabu hiyo, Ahmed Ally katika ofisi za klabu hiyo jijini Dar.

Juu ya usajili wake kughubikwa na utata wa kuhusishwa kutua Yanga, hakupenda sana kuzungumzia kwani mkataba wake kwenda Berkane ulikuwa na kipengele kilichosema; ‘Endapo (Chama) atashindwa kucheza timu hiyo ndani ya miaka mitano, basi timu pekee ya kurudi nchini ni Simba’ na hiki kiliitesa Yanga.

MWENYEKITI BODI

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema, ujio wa Chama ni kutokana na mahitaji na mapendekezo ya kocha wao Pablo.

Anasema mbali ya Pablo, hata wanasimba wengi walionekana kumuhitaji kiungo huyo na wao kama viongozi jukumu lao ni kuwapa kile wanachohitaji na ndio maana wapo kuiongoza klabu yao.

“Siku ya Mkutano Mkuu niliwapa salamu za Chama, nilipokuwa nikisikia mara sijui anaenda kule mara kafanya hivi nilikuwa nawaangalia tu, maana mimi nilikuwa najua nini nafanya, haya wanasimba Chama karudi huyo.”
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad