Mbeya. Makundi ya walemavu, wazee na kaya maskini wasiokuwa na msamaha wa matibabu katika Jimbo la Mbeya Mjini wanatarajiwa kufikiwa na Mpango wa bima ya Afya ya Jamii iliyoboreshwa (ICHF) ili kuwezesha kupata matibabu bure na kuondokana na adha ya kukosa huduma kutokana na ukosefu wa fedha.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Januari 3, 2021 Mbunge wa Mbeya Mjini na Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema kuwa amewiwa kusadia makundi hayo kutokana na kuwepo na changamoto mbalimbali Ikiwamo ukosefu wa kipato wanapokwenda katika hosptali na vituo vya afya kupatiwa huduma.
''Kumekuwepo na shida kwa wazee ambao hawajafikia umri wa kupata misamaha ya matibabu kwa kushindwa kumudu gharama hiyo kwa kundi la walemavu hivyo kuna kila sababu ya kugusa makundi hayo ili yaweza kupata matibabu bure'' amesema.
Ameongeza kuwa ''Kila atakayefikiwa na mpango huo atakatiwa bima ya afya iliyoboreshwa ambayo atalipiwa gharama ya Sh30, 000 kwa mwaka huku makundi mengine kama mama lishe, bodaboda watakatiwa bima na kurejesha Sh100 kwa kila mwezi.''amesema.
Dk Tulia ameongeza kuwa kwa mwaka jana utaratibu wa mtu kukatiwa bima na kurejesha Sh100 haufanya vizuri hivyo kwa mwaka huu watahakikisha linasimamiwa kikamikifu na kifanya vizuri lengo ni kila Mtanzania awe na bima'' amesema
Amesema kuwa wakati wakiwa kwenye utekelezaji wa kuanza utoaji wa bima kuna kila sababu maofisa maendeleo ya jamii kuanza kufuatilia taarifa za wazee na kundi la walemavu ili kuwezesha kufikiwa kwa wakati mara baada ya mpango kuanza.
''Sio kwamba naweza kutoa kwa kila mtu hapana kuna makundi maalumu ambayo yanapaswa kufikiwa hivyo ndugu zangu ningependa kupata taarifa zao ili waweze kufikiwa na mpango''amesema.
Dereva bodaboda, Jumanne Suleiman amesema kwa mwaka jana alikuwa mnufaikaji wa bima ya afya na kwamba alikamilisha kulipia kiwango chote cha Sh30, 000 kwa kutoa kwa mwezi kiasi cha Sh100.
''Kimsingi utaratibu ulioletwa na mbunge ulitusaidia sana sisi vijana wa bodaboda pindi tunapopata ajali za barabarani licha ya baadhi ya gharama kuwa kubwa lakini kwa kiasi furani zilikuwa mkombozi”.
Mkazi wa Iyunga jijini Mbeya, mzee Joshua Amos amesema mpango wa wazee kupatiwa bima itakuwa mkombozi kwani idadi kubwa wanapoteza maisha kutokana na kukosa fedha za matibabu kwa kukosa msamaha.