Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson Mwansasu leo Januari 10, 2022 amezungumza mbele ya Rais na viongozi wa serikali kwa nafasi ya Kiongozi wa Mhimili wa Bunge.
Dkt. Tulia amezungumza katika uapisho wa mawaziri na manaibu waziri wateule uliofanyika hii leo Ikulu Jijini Dodoma na kueleza kazi kuu ya mhimili huo wa Bunge ambayo ni kumsaidia Rais kusimamia sheria na katiba ambazo zitasaidia kuendesha shughuli za Serikali na sio kumpinga Rais.
“Rais ni Mkuu wa Nchi, Sasa wako watu wanachukua hiyo sehemu ambayo imesema Rais ni kiongozi wa Serikali, lakini Rais ana mambo yote ni Mkuu wa nchi, ni Kiongozi wa Serikali na ni Amiri Jeshi Mkuu wa nchi hii. Naamini kwa ufafanuzi huu watu wataelewa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan sio tu Kiongozi wa Serikali bali ni Mkuu wa Nchi kwa hiyo yeye uongozi wake hauko sawasawa na kiongozi yoyote wa muhimili wowote hapa nchini.” Alisema.
Aidha, Dkt. amewaasa viongozi wateule wa Rais kufanya kazi kwa uadilifu na kwa nia ya kumsaidia Kiongozi wa nchi haswa wanapokuwa Bungeni na kumsemea mazuri Rais wa awamu ya 6.
“Niseme tu kuwa kila mmoja ambae ameteuliwa kwa nafasi yoyote ile hapa Mheshimiwa Rais ameshayafanyia kazi maeneo hayo, na ninawapongeza kwa sababu mnayo sehemu ya kuanzia kusema mazuri ya serikali ya awamu ya hii ya 6 na kazi nzuri ambayo Mhe, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameifanya kwa nchi hii,” alisema.
“Labda niwape ushauri mmoja, niwaombe jambo moja, kwa sababu Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewaamini kwenda kumsaidia, hizo kazi ni kazi zake, na ninyi mnapoenda kuzifanya hizo kazi fanyeni kama wasaidizi wa Rais wa Tanzania na si vinginevyo.” Dkt. Tulia.
Aidha Dkt Tulia aliongeza kuwa Wabunge wote wapo tayari kusimamia shughuli zote za Serikali Bungeni na kushirikiana na Rais Samia katika kila hatua ili kuleta maendeleo ya nchi.
“hivi karibuni tumeshuhudia migongano kati ya mihimili tofauti ya serikali lakini kwa mujibu wa katiba, ni kazi yetu kutunga sheria, kuishauri serikali, na kuisimamia Serikali. Sasa yapo mazingira ambayo watu wanaamini kila wakati ni kuikosoa Serikali. Kwa hivyo kazi zote hizo tatu zinafanywa na Bunge na sio tu kuikosoa serikali…Kwa Muktadha huo basi Mhe. Rais, niseme tu kwamba Bunge lipo tayari kabisa kushirikiana na serikali yako ya awamu ya 6 kwa mambo yote utakayoleta Bungeni ili kutungia sheria, kutoa ushauri, na kukosoa serikali, na yote haya yatafanyika kwa namna ambayo itainufaisha serikali,” Alisema Dkt. Tulia
Hivi karibuni aliyekua Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Yustino Ndugai aliwasilisha barua kwa Katibu wa Chama cha Mapinduzi ya kujiuzulu wadhifa huo wa kuongoza mhimili wa Serikali kutokana na mkinzano uliokuwepo kati yake na Rais Samia na nafasi hiyo ipo wazi ikitegemea kupata mwenyewe kuanzia Februari 1, 2022.