Dar es Salaam. Familia zilizopotelewa na vijana wao watano tangumwishoni mwa mwaka jana zimeiomba Serikali kuingilia kati kusaidia kuwasaka kwani wamefanya kila wawezalo ikiwamo kupita kwenye hospitali na vituo vya polisi bila mafanikio.
Vijana hao; Tawfiq Mohamed, Self Swala, Kunambi, Hemed Abass na Rajabu Mdoe walipotea Disemba 26 mwaka jana wakiwa maeneo ya Kariakoo katika Mtaa wa Kamata wakielekea ufukwe wa Kigamboni kusherekea Sikukuu ya Krismasi.
Wakizungumza na Mwananchi jana, Longili Martin ambaye ni baba mzazi wa Edwin Kunambi alisema wapo kwenye sintofahamu licha ya kupanga na wenzake kwenda kumwona Waziri wa Mambo ya Ndani lakini bado hawajafanikiwa.
“Tulipofika ofisini kwa waziri iliyopo Posta Mpya tuliambiwa yupo Dodoma, basi tumeishi hapo. Kupitia vyombo vya habari tunaiomba Serikali watusaidia, wao wana mkono mrefu wa kufanya uchunguzi kupitia vyombo vyake, watusaidie kwani familia zetu zipo kwenye taharuki ukizingatia mtoto wangu ni baba mwenye familia,” alisema Martin.
Sylvia Quentin, mama mzazi wa Tawfiq alisema juzi walienda kuwatafuta vijana hao mkoani Pwani. “Tulizunguka kwenye hospitali na mochwari hatujawaona. Akili bado hazijatulia, tukienda kuulizia polisi bado wanaendelea kutujibu majibu yaleyale wanafanya uchunguzi ambao hautupi maendeleo japo ya kututia moyo,” alisema.
Juzi, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alisisitiza kuwa taarifa hizo ameshazipata na ameagiza zifanyiwe kazi kama zilivyo taarifa nyingine zinazopokelewa kwenye vituo vya polisi.
Kwenye mkutano wake huo na waandishi wa habari, Muliro alisema katika mfumo wa utekelezaji wa majukumu, taarifa yoyote inapopatikana inafanyiwa kazi kwa sababu wakati mwingine zinaweza kuwa za kweli au si za uongo.
“Taarifa ya kupotea kwa vijana hao ninayo, nimeagiza ifanyiwe kazi kama zilivyo taarifa zingine za kawaida zinazofikishwa kwenye vyombo vya dola ikiwemo polisi,” alisema Kamanda Muliro
Wanachosema marafiki
Baadhi ya marafiki wa vijana hao ambao walikuwa wakifanya nao biashara maeneo ya Kariakoo katika Mtaa wa Aggrey, walisema kupotea kwa wenzao kumewapa hofu na sasa hawajui hatima yao.
“Wote watano waliopotea ni marafiki zetu wa karibu sana, tulikuwa tunafanya nao biashara ya kuuza simu hapa Kariakoo. Walikuwa wanafanya kazi yao kwa ufanisi mkubwa na hawajawahi kukorofishana na mtu yeyote, walikuwa wanatoa huduma sawa na zingine,” alisema Oswini Mohamed, mmoja wa marafiki wa wana hao wapotevu.
Alisema walikuwa wanafanya kazi kwa ushirikiano kama familia moja na miongoni mwao akipatwa na shida walikuwa wanasaidiana kifedha.
Naye Moses John alisema vijana hao walikuwa marafiki zake na siku wanaenda kusherekea sikukuu ufukweni walipanga waende wote lakini alichelewa kuungana nao kwa sababu alikuwa akitoka mbali hivyo hakuweza kuwahi muda waliopanga kuondoka.
Alisema wanapata wasiwasi namna wanavyopambana kuwatafuta lakini hawapatikani na kudai huenda wasionekane huku akielezea kuwa hilo ni tukio la nne kutokea na wote waliopotea katika mazingira kama hayo hawajaonekana tena.
“Mimi ni mzoefu hapa Kariakoo kuna wenzetu kwa miaka mitatu tofauti walipotea katika mazingira ya aina hiyo na hawajaonekana tena na hii inatupa wasiwasi kubwa,” alisema John.