Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema na wenzake wakiwa mahakamani
FEDHA kiasi cha Sh. 699,000, zinazodaiwa kutolewa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe mwaka 2020 kwa ajili ya kufadhili vitendo vya kigaidi, zimeibua mkanganyiko Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, jijini Dar es Salaam. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Mkanganyiko huo umebainika leo Jumatatu, tarehe 31 Januari 2022, mahakamani hapo mbele ya Jaji Joachim Tiganga, wakati Wakili wa utetezi, Peter Kibatala, anamuuliza maswali ya dodoso, shahidi wa 12 wa Jamhuri, Luteni Denis Urio.
Anayediwa kutumiwa fedha hizo na Mbowe, kwa ajili ya kumtafutia makomando wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), waliostaafu au kufukuzwa kazi, ili kumsaidia katika njama za kufanya vitendo vya kigaidi.
Mkanganyiko huo umebainika baada ya viwango vya fedha vilivyotajwa na Luteni Urio kuwa aliwapa makomando hao ambao ni washtakiwa wenzake Mbowe, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya, kutofautiana na viwango vilivyotajwa kwenye maelezo yao ya onyo.
Utata mwingine uliibuka katika dhumuni la fedha hizo, ambapo washtakiwa wanadai walipewa fedha hizo kwa ajili ya kwenda Moshi mkoani Kilimanjaro, kufanya kazi ya ulinzi, Luteni Urio akidai walipewa hela ili kwenda kwa Mbowe jijini Dar es Salaam.
Mbali na Mbowe kwenye kesi hiyo ya ugaidi, wengi ni Adam Kasekwa, Halfan Bwire pamoja na Mohamed Ling’wenya.
Yafuatayo ni mahojiano kati ya Wakili Kibatala na Luteni Urio;
Kibatala: Katika maelezo ya onyo Kasekwa anasema, kwa kutumia simu ya mke wangu nilimpigia Ling’wenya kuna kazi ya VIP Protection ila anajua zaidi Urio.
Tuliondoka kufika Msamvu tukakutana na Urio, akasema kuna kazi ya VIP protection na maelezo tutayakuta huko huko.
Akatupa Sh.87, 000, kama kila mmoja alipewa Sh.87,000 mara mbili ni 174,000?
Shahidi: Ndio
Kibatala: Nikauliza statement ya Kasekwa na maelezo yako yanatofautiana?
Shahidi: Ndio
Kibatala: Ni sahihi ile Sh.195,000 ilikuwa ni fidia kwa gharama zao?
Shahidi: Si mimi, yaani hela zilizotumwa nimewapa kamili ambazo nilizotumiwa
Kibatala: Unakumbuka ulisema baada ya kukutana nao Msamvu uliwapa nauli ya kwenda wapi?
Shahidi: Dar es Salaam
Kibatala: Na hapa hamjazungumzia Sh.199,000, kutoka Morogoro kwenda huko wanakokwenda Adam na Ling’wenya, uliwapa shilingi ngapi ili kwenda kwa Mbowe?
Shahidi: Niliwapa Sh.195,000 na Sh.190,000, sikumbuki vizuri kama niliwapa cash au niliwatumia isipokuwa Sh.195,000 niliwapa cash
Kibatala: Wao wanasema Mbowe alitoa Sh. 699,000 kufadhili ugaidi
Shahidi: Ndio hela niliyopokea mimi
Kibatala: Ulitumiwa Sh.500,000 ukatoa Sh.300,000 ukawapa, ukabaki na Sh.200,000, ukatoa Sh.199,000 ukawapa Ling’wenya na wenzake kuwarudia?
Shahidi: Sahihi
Kibatala: Ni sahihi ile Sh.199,000 iliyotumwa baade ndio uliwapa hawa wawili waende kwa Mbowe?
Shahidi: Sahihi
Kibatala: Nataka destination, unafahamu kwamba katika statement yake Adam katika ukurasa wa nne inasema kila mtu ulimpa nauli ya kwenda Moshi kukutana na Mbowe.
Wewe unasema destination yao kwenda Dar es Salaam, Kasekwa anasema destination kwenda Moshi, Vinafanana vinatofautiana?
Shahidi: Kuna utofauti
Kibatala: Maelezo ya onyo ya Ling’wenya, wenzetu wanasema yeye baada ya mazungumzo Luteni Denis Urio alimuuliza kuwa huko Mtwara kwenye kibarua changu nilikuwa nalipwa shilingi ngapi, nikamueleza Sh.15,000 kwa siku, ukamshauri kwa Mbowe mshahara Sh.800,000 na kuendelea?
Shahidi: Sikumwambia hivyo
Kibatala: Kilichoandikwa huku kinatofautiana na wewe?
Shahidi: Sahihi
Kibatala: Ling’wenya anasema tulipokamilisha maongezi yetu Urio alitupatia fedha jumla Sh. 190,000 kwa ajili ya nauli kueleka Moshi na kununua mavazi.
Anachokisema huku kuhusu hela ambazo umewapatia nauli ya kwenda Moshi kinafanana na ulichosema?
Shahidi: Kinatofautiana na kinatofautiana hata na cha Adam
Kibatala: Unaona shahidi ziko tofauti, lakini pia hata hii Sh.190,000 inatofautiana na Sh.199,000 ambayo wewe unasema uliwapa nauli kwenda Moshi?
Shahidi: Mimi najua walienda Dar es Salaam sio Moshi
Kibatala: Kuna utofautiano au mfanano?
Shahidi: Kuna utofautiano
Kibatala: Unakubaliana na mimi wewe unazungumzia Sh.199,000, hawa wanuzungumzia Sh.190,000, si ndo anachosema Ling’wenya ?
Shahidi: Sahihi
Kibatala: Kuna utofauti wa Sh.9,000?
Shahidi: Sahihi
Kibatala: Unakubaliana na mimi kwamba katika maelezo ya kwanza na kielelezo cha upande wa mashtaka wale watu ambao uliwapa pesa wanasema matumizi yake yalikuwa kwa mambo mengine sio ugaidi, unakubaliana na mimi?
Shahidi: Sikubaliani na wewe
Kibatala: Na huyu Ling’wenya anasema hela hiyo Sh.190,000 uliwapa ili waweze kwenda Moshi, kwa hiyo mpaka hapa walikuwa bado hawaja kutana na Mbowe?
Shahidi: Walikuwa bado
Kibatala: Kabla hawajakutana na Mbowe kulikuwa na ugaidi au bado?
Shahidi: Hapo kulikuwa hakuna ugaidi
Kibatala: Unafahamu wenzetu walijumlisha hela zote hizi zilitumika kufadhili ugaidi, unafahamu?
Shahidi: Sifahamu
Kibatala: Anaendelea kusema Ling’wenya kwamba fedha hiyo ilikuwa kwa ajili ya nauli kuelekea Moshi na mavazi ili kwenda kununua mavazi nadhifu ?
Shahidi: Si kweli
Kibatala: Unakubakiana na mimi kwamba unachokisema wewe na Ling’wenya kuna utofautiano katika mambo mawili, la kwanza wewe unasema aliwapa kwenda Dar es Salaam, wewe unasema kwenda Moshi?
Shahidi: Ndiyo hivyo kwamba walipewa hela waende Dar es Salaam
Kibatala: Ni sahihi eneo la pili ukiacha destination eneo la pili mnatofautiana unasema hela ilikuwa ya nauli, Ling’wenya anasema ilijumlisha mavazi ili wawe nadhifu?
Shahidi: Ni sahihi