Filamu ya Bongo yawaogopesha Wakenya

 


Huko nchini Kenya siku za hivi karibuni kumeibuka gumzo kubwa mitandao baada ya kuenea kwa kipande cha video ikimuonyesha mwanamume mmoja akimpiga mwanamke aliyeonekana kuwa mke wake, kwa kutumia mkanda na kumtupa mtoto mchanga chini.


Kitendo hicho kiliwaumiza wengi, huku kundi kubwa la watu likiamini kuwa tukio hilo ni la ukweli na pengine linaihusu moja ya familia nchini humo.


Baada ya kuzua tahararuki kubwa, Hatimaye ukweli wa dhati juu ya uvumi huo umebainika, kuwa video hiyo si ya tukio halisi bali ni kipande kutoka kwenye filamu ya Kitanzania inayoitwa ‘Sitamani Kuolewa Tena’.


Kulingana na ripoti za awali, video hiyo iliaminika kuwa ya mwanamume Mkenya mwenye umri wa miaka 23 ambaye alidaiwa kugundua kuwa yeye sio baba mzazi wa mtoto huyo na ndio ikawa sababu ya kumpiga mkewe na kisha kukitupa kichanga hicho chini.


Jambo hilo lililounganishwa na tukio lingine lililowahi kutokea katika meneo ya Murang’a nchini humo ambapo kijana wa umri wa miaka 23 aliyetambulika kama Mark Njuguna alipigana na mkewe Mary Muthoni mnamo Januari 25. Njuguna anasemekana naye alimshika mtoto mchanga wa miezi minne na kumtupa sakafuni.


Kwa upande wa sehemu ya filamu hiyo iliyozua gumzo nchini Kenya, inaelezwa kuwa dhamira kuu ya waandaaji ilikuwa ni kukuza uelewa kwa wafuatiliaji wa maudhui hayo kuhusu ukatili dhidi ya wanawake na watoto.


Filamu hiyo inajumuisha matukio kadhaa ya kuogofya na kuhuzunisha kama ilivyoonekana kwenye baadhi ya vipande vilivyosambaa mtandaoni.


Kwa mujibu wa kituo cha masuala ya unyanyasaji wa kijinsia nchini Kenya (Gender Violence Recovery Centre), mwanamke mmoja kati ya watatu nchini humo yuko katika uwezekano mkubwa wa kukumbana na aina ya unyanyasaji wa kijinsia kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad