Wakati aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai akijiuzulu, wapo watu hawatamsahau kutokana matendo na kauli alizozitoa dhidi yao alipokuwa akitekeleza majukumu yake.
Ndugai alikuwa Spika kuanzia Novemba 2015 hadi Januari 6, 2021. Ni katika kipindi hicho wapo wanasiasa, watendaji wa Serikali na wanaharakati waliojikuta wameingia kwenye njia za mwanasiasa huyo na kupata shubiri.
Miongoni mwao ni waliokuwa wabunge na wengine wanaendelea mpaka sasa, wakiwamo wa upinzani Freeman Mbowe, Halima Mdee, Godbless Lema, Tundu Lissu, Zitto Kabwe na wengine kadhaa.
Wanasiasa hao walifukuzwa bungeni mara kadhaa, kukatwa mishahara yao na kufikishwa kwenye Kamati ya Hadhi, Maadili na Madaraka ya Bunge.
Aliyekuwa Mbunge wa Shinyanga Mjini, Steven Masele na aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, Profesa Mussa Assad nao kwa nyakati tofauti walikumbana na mkono wa Ndugai.
Freeman Mbowe
Kwa nyakati tofauti, Mwenyekiti wa Chadema na aliyekuwa Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, alikwaruzana na Spika Ndugai, ikiwa pamoja na kufukuzwa nje ya ukumbi wa Bunge na walinzi wa mhimili huo.
Aprili 6, 2017, Mbowe na Halima Mdee waliagizwa na Spika Ndugai kufika Kamati ya Haki, Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa tuhuma za kutukana Bunge kufuatia uchaguzi wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA).
Mbali na kushtakiwa kwenye Kamati ya Maadili, Hadhi na Madaraka ya Bunge, Ndugai alikuwa akitoa kauli za kebehi kwa Mbowe, ikiwemo ya kumtaka kurejesha Sh2 milioni alizopewa na Bunge ili kuhudhuria vikao vya Bunge, lakini hakuhudhuria.
Juni 9, 2020 baada ya Mbowe kudai kuvamiwa na kuvunjwa mguu na watu wasiojulikana, Ndugai alisema aliwatuma madaktari kufuatilia suala hilo na kudai kuwa Mbowe alikuwa amelewa na alianguka kwenye ngazi.
“Mheshimiwa Msukuma, tulienda kule kwa sababu ni mwenzetu, lakini baadaye nimetuma madaktari wangu kwenda kuzungumza na madaktari wa kule na kweli mwenzetu Mheshimiwa Mbowe amefikishwa kule kati ya saa 8 au 9 usiku na walipompokea alikuwa amelewa chakari,” alisema Ndugai.
Lissu kupigwa risasi
Licha ya madhila mengi waliyofanyiwa wabunge wa upinzani, aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki ambaye sasa ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu hatakuja kusahau hatua ya Spika Ndugai kutangaza kuwa amepoteza ubunge wake kwa kuwa hajahudhuria vikao vya mikutano mitatu mfululizo ya Bunge na ofisi ya Bunge haina taarifa aliko.
MOTO PIC2
Wakati Ndugai akitangaza jambo hilo, Lissu alikuwa nchini Ubelgiji akipatiwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 16 na watu wasiojulikana mjini Dodoma Septemba 7, 2017.
Baada ya shambulio hilo, alipelekwa kwenye hospitali ya rufaa jijini hapo kabla ya kusafirishwa kwenda Nairobi nchini Kenya na baadaye kwenda nchini Ubelgiji anakoishi mpaka sasa.
Awali Spika Ndugai alitoa kauli ya Bunge kumhudumia katika kipindi hicho. Lakini Juni 28, 2019 alidai kuwa Bunge halijui kuwa Lissu yuko wapi.
Spika alisema kwa zaidi mwaka mmoja, Lissu hakutoa taarifa ya mahali alipo na hakutoa taarifa ya madeni.
“Napenda kuwafahamisha kuwa nimemwandikia Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kiti kilichokuwa kinashikiliwa na Mbunge Tundu Antiphas Lissu kiko wazi na kuwa Mwenyekiti wa Tume aendelee na hatua ya kukijaza. Ubunge wake unakoma na ataacha kiti chake,” alisema Ndugai.
Awali kabla ya hapo, Spika Ndugai alimwonya Lissu alimtaka Lissu kurejea nyumbani kwa kuwa hana kibali cha kuwa nje ya nchi kufuatia kauli zake za kuikosoa Serikali akiwa nje ya nchi. “Sasa achunge kidogo, maana Spika ana nguvu zake. Arudi nyumbani aache maneno maneno nje huko.”
Juzi Lissu, alisema kuondoka kwa Ndugai ni jambo jema na kutoa funzo la kutafuta dawa ya Bunge lisiwe na maspika wa aina ya yake.
Alisema Ndugai hakuwa Spika mzuri si kwasababu alimuondoa yeye (Lissu) bungeni bali aliufanya muhimili huo kuwa dhaifu na kuwaumiza watu wengine hivyo ni furaha kwa wote walioumizwa.
Zitto
Mwingine aliyejikuta matatani ni aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ambaye pia ni kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo.
Mapema kabisa wakati Bunge la 11 linaanza, Machi 22, 2016 Zitto Kabwe alimwandikia barua Spika wa Bunge, Job Ndugai kujiuzulu ujumbe wa kamati ya huduma za kijamii.
Kutokana na mikwaruzano ya mara kwa mara, Septemba 13, 2017 Spika Ndugai alimwonya Zitto akimtishia kumzuia kuzungumza bungeni kwa kipindi chote cha Bunge hilo.
“Naweza kukupiga marufuku kuongea humu mpaka miaka yote ikaisha na hakuna pa kwenda, hakuna cha swali, hakuna cha nyongeza hakuna cha kuongea chochote humu ndani ya Bunge, utanifanya nini? Pambana na kitu kingine siyo Ndugai.”
Katika hatua nyingine, Spika Ndugai alikiri kukerwa na Zitto pale alipoliambia Bunge:
“Niseme ukweli kutoka moyoni mwangu, Zitto Kabwe amekuwa akinisumbua sana na kuniumiza kichwa, kwanza kwa sababu yupo peke yake na chama chake na hata nikisema nimchukulie hatua kama ambavyo nawafukuza wabunge wengine, namuonea huruma.”
Pamoja na kupatana na aliyekuwa Mbunge wa Kawe, Halima Mdee baada ya uchaguzi wa 2020, Spika Ndugai alikwaruzana na mbunge huyo mara kwa mara.
Julai 5, 2017 Ndugai aliagiza Mdee akamatwe kwa madai amekuwa akitoa maneno machafu ya kumdhalilisha Spika, “Halima Mdee popote pale atakapokuwa akamatwe kama ikibidi aletwe kwa pingu na mkiniletea hati nitaisaini.”
Stephen Masele
Mbali na wabunge wa upinzani, Mbunge mwingine wa CCM aliyejikuta matatani ni aliyekuwa mbunge wa Shinyanga Mjini, Steven Masele ambaye pia alikuwa Makamu wa Rais Bunge la Afrika (PAP).
Mei 16, 2019, Spika Ndugai aliliambia Bunge kuwa kwenye Bunge la Afrika (PAP) kumetokea matatizo makubwa kwa Stephen Masele na amelazimika kumrudisha nyumbani lakini amegoma.
Hata hivyo, Masele alihutubia PAP na kusema japo ameitwa na Spika Ndugai lakini aliwasiliana na Waziri Mkuu na kumtaka apuuze.
Kutokana na hali hiyo, Mei 16, 2019, Spika Ndugai alitangaza kusitisha uwakilishi wa Mbunge Stephen Masele PAP hadi Kamati ya Maadili itakapokamilisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili. Spika alisema Masele ana matatizo ya kinidhamu na amekuwa akigonganisha mihimili.
Mei 20, 2019 Stephen Masele aliwasili bungeni Dodoma kuitikia wito wa Spika Ndugai kufika mbele ya Kamati hiyo, ambapo, Masele alimtuhumu Spika Ndugai kuwa amewasiliana na Rais wa Bunge la Afrika ili amng’oe nafasi yake Makamu wa Rais wa PAP na ubunge wa Bunge hilo.
Masele pia aliikataa taarifa ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge iliyomkuta na hatia.
Kiini cha mzozo huo ilidaiwa kuwa Spika Ndugai alikuwa akimkingia kifua Spika wa PAP ambaye alikuwa akikabiliwa na kibano cha kung’olewa kutokana na tuhuma za ukiukaji wa haki za binadamu.
Profesa Mussa Assad
Aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad naye alijikuta matatani baada ya kutoa kauli kuwa Bunge ni dhaifu kutokana na kushindwa kuibana Serikali na matokeo yake makosa yaleyale yanajirudia kila zinapowasilishwa ripoti za CAG.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Januari 7, 2019, Spika Ndugai alimtaka Profesa Assad kufika mbele ya Kamati ya Haki, Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge ili ahojiwealifanya hivyo lakini aligoma kuomba radhi na kufuta neno ‘dhaifu’ kwakuwa ni la kihasibu na halikuwa na lengo la kudhalilisha Bunge.
Kutokana na msimamo huo, Januari 16, 2019, Spika Ndugai alisema Bunge limesitisha kufanya kazi na kiongozi huyo ambaye alisema anamuweka kwenye wakati mgumu aliyemteua (Rais John Magufuli).
Ili kutekeleza suala hilo, Ndugai aliwatawanya wajumbe wa Kamati za PAC na LAAC ambazo hufanya kazi na CAG, ili wakafanye kazi katika kamati nyingine.
Novemba 2019, Rais hayati John Magufuli alimteua Charles Kicheere kuwa CAG, kwa maelezo kuwa muda wa CAG kuwa katika ofisi hiyo umekwisha.
Uamuzi huo ulilalamikiwa na Profesa Assad na wadau wengine waliodai Katiba imekiukwa, lakini pia ulifanywa kwa lengo ya kulifurahisha Bunge ili kudumisha uhusiano mzuri wa mihimili hiyo miwili.
Jenerali Ulimwengu
Pengine mtu pekee aliyekuwa akisubiri kibano cha Spika Ndugai ni mwandishi wa habari mkongwe, Jenerali Ulimwengu ambaye naye alitoa kauli za kumkera Ndugai mwishoni mwa mwaka jana.
“Ndugai haelewi kwa nini watu wanaitwa mawakili wasomi, ingawaje yeye anaona ni sawa tu kwa kila mtu aliyeko kwenye nyumba yake kuitwa mheshimiwa, halafu wengine tunajua wengine hawana heshima yoyote,” alisema Ulimwengu katika moja ya mijadala ya demokrasia aliyoshiriki.
Kauli hiyo ilionekana kumgusa Ndugai na ndipo Novemba 11, 2021, alimwonya Ulimwengu kwa kauli zake, akidai kuwa analivunjia heshima Bunge na akimuonya achunge ulimi wake la sivyo watamshughulikia ndani na nje, yaani mahakamani.”
Jana Jenerali Ulimwengu aliliambia Mwananchi ni vema Watanzania wakamuacha Ndugai apumzike na atafakari kilichotokea.
Wabunge 19 wasio na vyama
Baada ya uchaguzi wa 2020, Chadema iliambulia mbunge mmoja, lakini kutokana na wingi wa kura zake, ilipata wabunge wa viti maalumu 19.
Hata hivyo, chama hicho kilisusia matokeo ya uchaguzi huo na kinadai hakikupeleka majina ya uteuzi wa viti maalumu katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Lakini katika hali isiyotarajiwa, makada 19 wanawake wa chama hicho wakiongozwa na Halima Mdee walikwenda bungeni jijini Dodoma Novemba 24 na kuapishwa na Spika Ndugai bila idhini ya chama hicho.
Hatua hiyo ilisababisha Chadema kuwavua nyadhifa zao na kuwafukuza uanachama.
Lakini bado Ndugai aliwatetea, huku akiikataa barua iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika ya uamuzi wa kuwafukuza.
“Makatibu wajifunze kuandika barua nzuri kwangu, huwezi kuniandikia kikaratasi hivi halafu unataka niwafukuze wabunge 19, hiyo siyo kazi yangu hata kidogo, ninyi wabunge chapeni kazi kwani mko kwenye mikono salama,” alisema Ndugai.
Askofu Gwajima, Jerry Silaa
Mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima na mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa nao walionja chungu ya Spika Ndugai ambaye aliagiza waitwe na wahojiwe kwenye Kamati ya Haki, Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa kusema uongo na kulivunjia heshima Bunge.
Wabunge hao baada ya kuhojiwa walipatikana na hatia na kupewa adhabu ya kufungiwa kuhudhuria vikao vya Bunge baada ya kugoma kuomba radhi walipokuwa wakihojiwa.