NI wiki ngumu kwa makada 71 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliojitokeza kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kuwania nafasi ya Spika wa Bunge.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa Januari 9, mwaka huu, na Katibu Idara ya Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Shaka Hamdu Shaka, urejeshaji fomu ulikamilika Januari 15.
Makada hao wa CCM wamejitokeza kuwaniwa kiti hicho, baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kujiuzulu wadhifa huo, Januari 6, mwaka huu.
Leo Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama hicho itakutana kwa ajili ya kujadili wagombea na kuishauri Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wagombea waliojitokeza kuomba kiti hicho.
Januari 18 na 19, itakuwa ni kazi ya kuchuja na kufanya uteuzi wa mwisho utakaofanywa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu.
Kabla ya kupigiwa kura na wabunge wote, Janauri 21 hadi 30 itakuwa ni kikao cha chama cha wabunge wa CCM (caucus), kupiga kura kumpata mgombea ambaye atakwenda kuomba kura bungeni.
Miongoni mwa waliojitokeza kwenye kinyang’anyiro hicho ni Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa UWT Taifa, Sophia Simba na aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mbunge wa Jimbo la Bariadi (CCM), Andrew Chenge.
Vile vile, kiti hicho kinawaniwa na wabunge mbalimbali akiwamo Joseph Kasheku, maarufu Msukuma, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Bunge la Afrika (PAP) na Mbunge wa Shinyanga Mjini, Steven Masele na msomi aliyejinasibu kuwa na shahada tisa, Baraka Byabato.
Hadi juzi watu 71 walikuwa wamejitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo, ambayo ilitolewa kwa gharama ya shilingi milioni moja.
Kuanzia leo itakuwa wiki ya mchakato wa kumpata kada atakayekiwakilisha chama hicho kwenye kinyang’anyiro cha kumpata Spika mpya wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kifungu cha 84.-(1) kutakuwa na Spika wa Bunge ambaye atachaguliwa na wabunge kutoka miongoni mwa watu ambao ni wabunge au wenye sifa za kuwa wabunge; atakuwa ndiye kiongozi wa Bunge na atawakilisha Bunge katika vyombo na vikao vingine vyote nje ya Bunge.