Hizi Hapa Mbinu Wanazotumia Trafiki Kupokea Rushwa



VITENDO vya rushwa ni miongoopni mwa mambo yanayopigwa vita kutokana na kurudisha nyuma maendeleo baada ya sekta na taasisi mbalimbali za umma hasa ya Jeshi la Polisi wa Usalama Barabarani kutuhumiwa kujihusisha na vitendo hivyo.

Rais Samia Suluhu Hassan, hivi karibuni alionyesha kukerwa na vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa na baadhi ya aska9ri wa usalama barabarani kwa madereva na kuwataka kujiepusha na vitendo vya kuomba na kupokea rushwa.

Kwa nyakati tofauti katika mikoa ya Iringa na Kilimanjaro askari wawili wa usalama barabarani walidaiwa kukamatwa kutokana na kuhusishwa na tuhuma za kupokea rushwa.

Katika tukio la Januari 14, mwaka huu, Himo wilayani Moshi, askari polisi mwenye cheo cha Mkaguzi Msaidizi alikamatwa akidaiwa kupokea Sh. 20,000 ili kushughulikia dhamana ya mtuhumiwa.

Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Kilimanjaro, Frida Wakesi, alikiri kukamatwa kwa ofisa huyo, ambaye alisema upelelezi wa tukio lake unaendelea.


Tukio la pili lilitokea Januari 18, siku nne baada ya tukio la kwaza baada ya askari wa usalama barabarani wa Mkoa wa Iringa, kukamatwa na fedha anazodaiwa kuzikusanya kwa njia ya rushwa kutoka kwa madereva wa magari.

Baada ya tukio hilo katikati ya wiki hii, picha zilianza kusambaa katika mitandao ya kijamii zikionyesha noti za Sh. 1,000, 2,000, 5,000, na 10,000 na kuhifadhiwa kwenye kiti ndani ya gari na zingine zikiwa zimeshikwa mkononi na askari.

NJIA ZINAZOTUMIKA

Uchunguzi wa Nipashe kwa kuwahoji baadhi ya madereva wa mabasi ya mikoani, daladala, bajaji na bodaboda katika Mkoa wa Dar es Salaam, umebaini kuwapo njia tofuati zinazotumiwa na askari hao wakati wa kupokea rushwa.


LESENI

Saidi Halfani ambaye ni dereva wa daladala inayofanya safari za Kinyerezi - Mnazi Mmoja, alisema wanapata kero kutoka kwa baadhi ya maofisa usalama barabarani kwa kusimamishwa katika maeneo ambayo sio rafiki.

“Wakati mwingine wanakusimamisha ghafla na sehemu ambayo usipokuwa makini unaweza kusababisha ajali, baada ya kusimama anakuambia unakosa fulani nipe kiasi fulani la sivyo nikuandikie cheti, na njia wanayoitumia sana ni wakati wa kupokea leseni.

“Akikusimamisha anakuambia nipe leseni na wakati huo huo anataka umkunjie fedha kwa chini hali ambayo kwa kawaida mtu wa pembeni hawezi kutambua kitu gani kinaendelea,” alidai.

RISITI

Rasuli Ally, anayeendesha daladala ya Segerea – Chanika, alidai kuwa njia nyingine wanayoitumia askari wa usalama barabarani kupokea rushwa ni kwa kutumia risiti baada ya kukamata gari alidai kuwa risiti walizozitoa siku za nyuma hutumika kuwapatia fedha.


“Baadhi yao baada ya kukamata gari humtaka konda au dereva kuikunja fedha ndani ya risiti na kumpatia wakati huo wakiwa wamesimama nyuma ya gari mahali ambapo mtu sio rahisi kuwaona,” alidai.

KOFIA/VICHWA NDANI YA GARI

Sabrina Rashidi, dereva wa gari binafsi alidai kuwa kwa upande wa gari ndogo baadhi ya askari wa usalama barabarani baada ya kusimamisha gari na kutambua kuwa lina kosa hutumia kofia au kuingiza kichwa ndani ya gari ikiwa ni njia ya kumtaka dereva ampe fedha.

“Wengine huhitaji wawekewe fedha ndani ya kofia zao, au anapoingiza kichwa ndani ya gari anakuonyesha ishara kuwa udumbukize ndani ya shati lake, kitendo ambacho ni ngumu mtu anayepita pembeni kutambua kwani atahisi tu kuwa ni mazungumzo yanaendelea,” alidai.

VIBANDA

Swabri Faruku, ambaye pia ni dereva wa gari binafsi alidai kuwa baadhi ya askari hao wanapokamata gari barabarani humtaka dereva aende kuweka fedha kwenye kibanda ambacho kipo karibu na eneo husika ili wasimuandikie cheti kulingana na kosa analokutwa nalo.


MAWAKALA

Alidai kuwa wengine hutumia watu tofauti na wao kupokea fedha kutoka kwa madereva na watu hao alidai kwamba wanakuwa wanasimama au wanaendesha biashara karibu na mazingira wanapolikamatia gari.

VIATU

Dereva Bajaji Shabani Juma, ambaye kituo chake ni Kimara alidai kuwa baadhi ya askari wanapomkamata mtu na kubaini kuwa chombo chake cha usafiri kina upungufu, badala wa kumuandikia faini alidai kuwa huwaambia waweke fedha kwenye viatu vyao.

“Kipindi hiki mvua zikinyesha wengi huwa wanakuwa wanavaa viatu virefu (Gumboot) kujikinga na mvua hivyo akikukamata anakuambia udumbukize fedha mule akienda sehemu ambayo haonekani anaitoa,” alidai.

LESO

Dereva wa bodaboda aliyejitambulisha kwa jina moja la Damas, alidai kuwa njia nyingine inayotumika na baadhi ya askari wa usalama barabarani kuchukua fedha ni vitaa vya kujifutia jasho (Lesso), ambacho alidai kuwa wakibaini kosa humtaka mtu kukunja fedha kwenye kutambaa hicho na kuidondosha kwenye faili wanalokuwa wamelishika.

Dereva wa basi la abiria wa mikoani ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alidai kuwa baadhi ya askari wanaokutana nao njiani hupokea rushwa kwa kutumia tissue (karatasi laini), akidai kuwa huwaambia madereva wakunje fedha kwenye hiyo tissue na kuitupa na baadaye huifuata na kuichukua.


WAZIRI ANENA

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni aliwataka watu wanaotoa taarifa au kuzungumzia suala hilo kuangalia pande zote, kwa mtoaji na mpokeaji pia, kwa kuwa wote wanafanya makosa kwa mujibu wa sheria.

“Matukio yote ya uvunjaji wa sheria tutajitahidi iwezekanavyo kuyadhibiti, kikubwa tunaomba ushirikiano kwa wananchi, rushwa ni kosa, halitazami wewe unafanya kazi gani, ukibainika utashtakiwa kwa mujibu wa sheria,” alisema.

KAULI YA JESHI LA POLISI

Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini, David Misime, alisema baada ya kupata taarifa za askari kuhusishwa na tuhuma za rushwa hatua za uchunguzi dhidi yake zilianza kuchukuliwa kwa kushirikiana na wadau wengine.

“Jeshi la polisi lingependa kutamka kuwa, hakuna aliyepo juu ya sheria hivyo hatua kali na stahiki kwa mujibu wa sheria, kanuni, utaratibu na ushahidi utakaopatikana zitachukuliwa,” alisema.

Hata hivyo Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Wilbroad Mutafungwa aliwataka askari wa usalama barabarani kutokwenda na magari kwenye sehemu zao za kazi akidai kuwa magari hayo yanatumika kupatania rushwa na kueleza kuwa kitendo hiko kinatengeneza taswira mbaya ya Jeshi hilo
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad