Hofu ya Raila kuwa ‘kinyago’ au dikteta akishinda urais



HUENDA KIONGOZI WA ODM, Bw Raila Odinga, akageuka kuwa rais asiye na mamlaka yoyote, ikiwa ataibuka mshindi kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Kulingana na wadadisi wa siasa, hili ni kutokana na msukumo mkubwa atakaokuwa nao kutimiza na kulinda maslahi ya kisiasa na kiuchumi ya makundi mbalimbali ambayo yanampigia debe kuwa mrithi wa Rais Uhuru Kenyatta.

Kufikia sasa, baadhi ya makundi muhimu ambayo yamejitokeza kuunga mkono azma ya Bw Odinga kuwa rais ni mabwanyenye wenye ushawishi kutoka eneo la Mlima Kenya chini ya Wakfu wa Mlima Kenya (MKF).

Kundi hilo linawashirikisha mabwanyenye maarufu na wenye ushawishi, waliowekeza katika sekta muhimu za kiuchumi kama kilimo, majumba ya kifahari, hisa, bima, benki, vyombo vya habari miongoni mwa nyingine.


 
Bw Odinga pia anaungwa mkono na wanasiasa wenye ushawishi kama magavana, hatua inayotajwa kuwa muhimu sana kwenye azma yake kuwania urais.

Wiki iliyopita, karibu magavana 30 walitangaza kuunga mkono azma ya Bw Odinga, wakimtaja kama “mpiganiaji wa demokrasia, na kiongozi bora zaidi kumrithi Rais Kenyatta”.

Hata hivyo, wadadisi wanasema kujitokeza kwa makundi hayo yote kunasukumwa na maslahi yao binafsi, ambapo nia ni kumtaka Bw Odinga kuyalinda ikiwa atafanikiwa kushinda uchaguzi huo.


“Lengo kuu la makundi hayo ni kuhakikisha kuwa Bw Odinga atalinda maslahi yake ya kisiasa na kiuchumi. Ni kama hali ya nipe-nikupe. Nifanyie hili nikutumizie lile. Lazima pawepo makubaliano ya siri yaliyofikiwa na pande zote mbili,” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Kulingana na mchanganuzi huyo, kuna uwezekano baadhi ya “makubaliano” hayo yanajumuisha kumtaka Bw Odinga kuwateua watu fulani katika nyadhifa muhimu serikalini, kutoa kandarasi kwa baadhi ya kampuni na kuhakikisha sera za kiuchumi za serikali haziathiri biashara zao.

Hata hivyo, wadadisi wanaonya kuwa ingawa mikataba hiyo imekuwa ikitumika kwingi duniani, hasa barani Afrika, baadhi ya viongozi wameikiuka na hata kuwageuka baadhi ya washirika wao wa karibu waliowasaidia kutwaa uongozi.

Mfano ni nchini Tanzania, ambapo Rais Samia Suluhu ameanza kuwaondoa serikalini baadhi ya mawaziri walioonekana kuwa washirika wa karibu wa mtangulizi wake, marehemu Johh Magufuli.


 
Akifanya mabadiliko kwenye baraza la mawaziri wiki mbili zilizopita, Rais Suluhu alisema “hatamvumilia yeyote ambaye anahujumu serikali yake.” Nchini Zambia, aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Levy Mwanawasa alimfungulia mashtaka mtangulizi wake, Frederick Chiluba, licha ya Chiluba kumsaidia sana kutwaaurais. Mwala 2009, Chiluba alikwepa kufungwa jela kwa miaka 15 baada ya kupatikana na hatia ya kushiriki ufisadi.

Novemba mwaka uliopita, Mahakama ya Juu nchini Angola ilimhukumu mwanawe aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Jose Eduardo dos Santos, Jose Filomeno dos Santos, miaka mitano gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kujaribu kuipora nchi hiyo hadi Sh150 bilioni kati ya mwaka 2013 na 2018. Alikuwa akisimamia hazina maalum ya kifedha nchini humo.

Alipochukua uongozi mnamo 2017 kutoka kwa Dos Santos, Rais Joao Lourenco aliapa kukabiliana vikali na ufisadi, bila kujali hadhi ya mhusika Nchini Zimbabwe, Rais Emmerson Mnangagwa ndiye aliyeendesha mapinduzi dhidi ya marehemu Robert Mugabe, licha ya wawili hao kuwa washirika wa karibu.

Mfano mwingine ni nchini Congo (DRC) ambapo Rais Felix Tshisekedi ameripotiwa kukosana vikali na mtangulizi wake, Joseph Kabila, Katika hali hiyo, wadadisi wanasema makundi yanayomuunga mkono kigogo yeyote wa kisiasa kuwania urais ili kulinda maslahi yake yanapaswa kutahadhari sana
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad