Inatisha Mauaji Tanzania..Yawaweka Mtegoni Vigogo



Dar/Mikoani. Siku tatu baada ya Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango kumwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, kukomesha mauaji ya kikatili yanayoendelea kufanyika nchini, watu wengine kadhaa wameuawa, hatua inayoonyesha dalili za kuwaweka mtegoni vigogo wa jeshi hilo.

Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime alisema agizo hilo wameshaanza kulifanyia kazi kwa kubuni mikakati mipya ya kiutendaji ikiwamo kuongeza kasi katika ufuatiliaji likiwamo tukio la mauaji ya Bahi.

Januari 24, watu watano wa familia moja walikutwa wameuawa ndani ya nyumba waliyokuwa wakiishi iliyopo katika kijiji cha Zanka kilichopo wilayani Bahi mkoani Dodoma, huku jeshi hilo likiahidi kufanya uchunguzi wa mauaji hayo.

Mauaji hayo yalimgusa Dk Mpango na kumfanya aende kutoa pole kwa familia iliyopoteza watu hao waliodaiwa kuuawa na watu wasiojulikana, huku akiagiza vyombo vyote vya dola nchini kufanyia kazi matukio hayo na taarifa rasmi iwasilishwe kwa Rais Samia Suluhu Hassan ndani ya siku saba.


“Tukio hili halikubaliki. Zizi liko hapa, nyumba ziko karibu, inawezekanaje jirani asijue huyu jirani hajatoka kweli? Wasakwe wote kokote walipo. Hatuwezi kwenda namna hii,” alisema Dk Mpango.

Matukio mapya

Juzi Jeshi la Polisi mkoani Mara lilisema linamshikilia Kija Juma (30), mkazi wa kijiji cha Rigicha wilayani Serengeti na watu wengine watano kwa tuhuma za kumuua mama mkwe wake, Wankuru Mwita (88) kwa imani za kishirikina.

Pia, watu wengine watano, wakiwamo viongozi wa kitongoji na kijiji wanashikiliwa na jeshi hilo mkoani Songwe kwa tuhuma za kuwaua watu wawili wa familia moja (baba na mtoto) katika kijiji cha Mpuwi wilayani Momba.


Mauaji haya ni mwendelezo wa matukio mengine ya mauaji ya watu yaliyotokea hivi karibuni na kuibua simanzi kwa ndugu, jamaa na marafiki wanaopoteza wapendwa wao, lakini pia kuibua hofu kwa jamii kwa jumla.

Huko Mtwara, mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis anadaiwa kuuawa na maofisa wa Jeshi la Polisi huku ofisa wa jeshi hilo, Grayson Mahembe aliyekuwa akishikiliwa kwa tuhuma hizo akidaiwa kujinyonga hadi kufa akiwa mahabusu.

Mauaji Mara

Mbali ya Kija, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Longinus Tibushubwamu aliwataja watuhumiwa wengine wanaoshikiliwa kwa mauaji hayo yaliyofanyika Januari 5, 2022 kuwa ni Peter Masalu (45), Emmanuel Juma (38), Manoni Sumaku (38) wote wakazi wa kijiji cha Rigicha.

Jeshi hilo pia linawashikiliwa waganga wawili wa kienyeji waliopiga ramli chonganisha iliyosababisha mauaji hayo waliotajwa kuwa ni Makeremo Paulo (47) na Mageni Itegwa (40).


Kabla ya kutekeleza mauaji hayo, mtuhumiwa Kija anadaiwa kwenda kwa mganga wa kienyeji, Makeremo, mkazi wa kijiji cha Rigicha ili kutatuliwa tatizo la watoto wake kuugua mara kwa mara.

“Huko kwa mganga ndiko alikoelezwa kuwa mama mkwe wake ndiye anahusika na kuugua kwa watoto wake. Mtuhumiwa alienda kwa mganga mwingine anayejulikana kwa jina la Mageni Itegwa ambako pia aliambiwa mhusika wa maradhi ya watoto wake ni mama mkwe wake,” alisema Kamanda Tibushubwamu.

Alisema baada ya majadiliano, mganga huyo wa pili aliahidi kumtafutia mtuhumiwa Kija watu ambao wangetekeleza mauaji ya mama mkwe wake kuwanusuru watoto wake wanne waliokuwa wakiugua mara kwa mara.

“Kwa makubaliano ya malipo ya Sh500,000, mganga huyo aliwatafuta vijana watatu wa kutekeleza mauaji hayo ambapo aliwaosha kwa dawa aliyodai ni ya kuondoa mikosi ya kukamatwa na polisi baada ya mauaji,” alisema.


Alisema wauaji hao wa kukodishwa walilipwa kianzio cha Sh50,000 ambazo ni malipo ya fedha za Tasaf alizopokea Kija ambaye aliahidi kumalizia Sh450,000 zilizosalia.

Mauaji Songwe

Huko Songwe, Jeshi la Polisi mkoani humo linawashikilia watu watano, wakiwemo viongozi wa kitongoji na kijiji kwa tuhuma za kuwaua watu wawili wa familia moja (baba na mtoto) katika kijiji cha Mpuwi wilayani Momba.

Kamanda wa Polisi mkoani wa Songwe, Janeth Magomi alisema wanaoshikiliwa ni pamoja na viongozi wa kitongoji cha Ntekwe na kijiji cha Mpuwi ambao majina yao yamehifadhiwa kwa sasa.

Alisema waliokamatwa wanatuhumiwa kuchangia, kushiriki au kuwaua watu wawili ambao ni Juma Sekesi na mtoto wake Yohana Sekesi katika tukio lililotokea usiku wa kuamkia Januari 24, mwaka huu.

Magomi alisema uchunguzi wa awali unaoonyesha chanzo cha mauaji hayo ni tuhuma za kishirikina zinazotokana na mke mkubwa wa marehemu Juma kuugua na hatimaye ndugu kumtuhumu marehemu na mke mdogo kwamba wanamloga.


Alisema tuhuma hizo zilichochewa na wapiga ramli pamoja na wachonganishi wa jamii wanaojiita lambalamba.

“Nasisitiza agizo la Mkuu wa Mkoa, Omary Mgumba kupiga marufuku vitendo vya lambalamba mkoani hapa, polisi wataendelea kuwasaka wahusika na pia itawakamata viongozi wa vijiji kila kukitokea mauaji yenye chanzo cha ushirikina,” alisema.

Mapema wiki hii, Mkuu wa Mkoa wa Songwe alipokuwa akizindua Wiki ya Mahakama mjini Tunduma, alitoa taarifa za baba na mtoto kuuawa Momba na kuagiza wahusika wote wakamatwe.

Kufuatia agizo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Momba, Fakii Lulandala alisema alishirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama na hatimaye kufanikiwa kuwakamata watu watano.

Lulandala alisema kuanzia sasa hatavumilia kusikia lambalamba au taarifa za kuuawa watu kwa tuhuma za kijinga kama ushirikina.

LHRC yalaani mauaji

Juzi, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kililaani mauaji ya kikatili yanayoendelea kutokea sehemu mbalimbali nchini.

Vilevile, kililipongeza Jeshi la Polisi kwa kuchukua hatua dhidi ya maaskari wake saba wanaotuhumiwa kumuua mfanyabiashara Mussa Hamisi mkoani Mtwara na kuwafikisha mahakamani.

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga alisema katika kipindi cha Januari pekee, kumeripotiwa matukio mbalimbali ya mauaji ya kikatili ambayo yameleta huzuni na kusababisha ukiukwaji wa haki za binadamu.

Alisema LHRC imekusanya takribani matukio 20 ya mauaji hayo yaliyoripotiwa katika mikoa ya Mtwara, Rukwa, Njombe, Katavi, Mwanza, Dodoma, Ruvuma, Dar es Salaam na Mara.

Henga aliyataja baadhi ya matukio kuwa ni pamoja na la mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis, mkazi wa kijiji cha Ruponda wilayani Nachingwea mkoani Lindi pamoja na lile lililotokea mkoani Mwanza, ambako wanawake watatu waliuawa na miili yao kutupwa katika eneo la Mecco Kusini, wilayani Ilemela jijini Mwanza.

“LHRC inalaani kitendo hiki cha ukatili dhidi ya wanawake na tunatoa rai kwa Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi na kuhakikisha watu waliofanya vitendo hivi vya ukatili wanafikishwa mahakamani,” alisema Henga.

Wataalamu wa saikolojia na afya ya akili

Ofisa Ustawi wa Jamii na Mratibu wa Kituo cha Mkono kwa Mkono katika Hospitali ya Rufaa Mwananyamala, Asia Mkini alishauri kufanyika kwa tafiti mbalimbali kwa kina itakayowezesha kupata sababu halisi juu ya kuongezeka kwa matukio ya ukatili na mauaji.

“Wakati umefika kama Serikali na wanajamii kwa ujumla kuingia katika kufanya tafiti kujua sababu hasa za matendo ya ukatili kuendelea kuongezeka, suala hili linahitajika kuchambuliwa kitaalamu, hivyo ni vyema mbali na jitihada nyingine zinazofanyika, vilevile ni muhimu kuwekeza katika tafiti,” alisema.

Mtaalamu wa Afya ya Akili, Dk Philimina Scarion kutoka Mental Health Tanzania alisema matukio kama haya huweza kusababishwa na mhusika kuwa na matatizo ya akili (kuchanganyikiwa) au mrundikano wa msongo wa mawazo ndani ya kichwa chake.

Alisema mtu akikosa mbinu sahihi za kukabiliana na msongo ambazo kitaalamu hujulikana kama ‘stress management’ hushindwa kuzuia hasira zake pale anapofanyiwa maudhi fulani na kujikuta amesababisha majeraha au kifo kwa mtu.

Aliongezea kuwa kwa mtu aliyepata tatizo la kuchanganyikiwa huweza kumsababishia kufanya matukio ya kikatili na kwa mujibu wa mtaalamu huyo, baadhi yao kusukumwa na sauti wanazokuwa wakizisikia zikiwaamuru kufanya jambo fulani.

“Wakati wa matibabu kuna baadhi ya wagonjwa nikizungumza nao wananiambia kuna sauti zimekuwa zikiwashinikiza kufanya mambo fulani na kutokana na shinikizo la sauti hizo wanajikuta wamefanya hayo,” alisema.

Kwa upande wa matibabu, Dk Philimina alisema kuna aina mbili za matibabu ambayo hutolewa kulingana na hali ya mgonjwa. “Matibabu hayo ni pamoja na mgonjwa kukutanishwa na mwanasaikolojia na kuzungumza naye ambayo tiba hii kitaalamu hujulikana kama ‘stress and anger management’.”

Alisema kwa upande wa matibabu ya dawa, huhusisha madaktari wa afya ya akili ambayo hutolewa kulingana na hali ya mgonjwa.

Imeandikwa na Peter Elias, Tatu Mohamed, Beldina Nyakeke, Mariam Mbwana na Stephano Simbeye.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad