Yanga na Azam FC zilimaliza mchezo kwa kutofungana kwa dakika 90 za kawaida.
Zanzibar. Yanga imetema taji la Kombe la Mapinduzi baada ya kufungwa kwa mikwaju ya penalti 9-8, wakati dakika 90 za mchezo wa nusu fainali ukimalizika kwa suluhu.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo, kocha msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze alisema vijana wake walichoshwa na kucheza mechi mfululizo huku akitumia vijana wengi waliokuwa wakikosa nafasi katika mechi nyingi za Ligi Kuu msimu huu.
Kaze alisema alilazimika pia kutumia wachezaji ambao walitoka mapumziko na kushindwa kuwa na utimamu wa mwili wa kutosha kwa ajili ya mchezo mgumu kama huo.
“Tulianza mashindano haya na vijana ambao walikosa nafasi mara nyingi katika mechi zetu za kimashindano lakini tukashindwa kuwa na wale wote wa kikosi cha kwanza ambao walikuwa mapumzikoni.
“Lakini mchezo umemalizika na tunawapongeza wapinzani, kwani hiyo si sababu ya kutosha kwa kupoteza mchezo, mwisho wa siku mshindi amepatikana na tutajipanga kwa mechi zetu zijazo za mashindano mengine,” alisema Kaze.
Kwa matokeo hayo kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, jana, Azam FC sasa itakutana na mshindi kati ya Simba na Namungo, mchezo ambao ulichezwa saa 2 usiku, jana.
Mkwaju wa penalti ya beki wa kushoto wa Yanga, Yassin Mustaph ulimpa nafasi kiungo wa Azam FC, Mudathir Yahya kushinda mkwaju wake wa ushindi na kuipa timu yake nafasi ya kutinga fainali ya saba ya Kombe la Mapinduzi.
Yanga haikuonekana kuwa katika ubora wake uliozoeleka tangu kipinddi cha kwanza na kuwa na hatari chache katika lango la Azam, huku ikikosa mashuti yaliyolenga lango.
Yanga ilimwanzisha Herritier Makambo mwenye mabao mawili ya mashindano hayo, ambaye hata hivyo hakuwa na nafasi mbele ya mabeki wa Azam walioongozwa na Aggrey Morris na Daniel Amoah.
Kocha wa Yanga, Kaze alikibadilisha kikosi chake kilichoanza katika mechi mbili zilizopita, akiwarudisha kikosini Yannick Bangala na Fiston Mayele, ambaye aliingia kipindi cha pili.
Lakini pigo kwa Yanga ni kumpoteza kiungo wake mshambuliaji, Feisal Salum, ambaye alishindwa kuendelea na mchezo baada ya kukaa chini mara mbili akilalamikia misuli ya paja.
Kwa upande wa Yanga, nyota wa zamani wa Simba, Ibrahim Ajibu alikuwa akiitumikia miamba hiyo katika mchezo wake wa tatu msimu huu, lakini bado hajafanikiwa kufanya makubwa.
Fainali ya Kombe la Mapinduzi inatarajiwa kuchezwa Januari 13, kwenye Uwanja wa Amaan.