MRAKIBU wa Polisi, Jumanne Malangahe, shahidi wa Jamhuri, katika kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake, amedai tukio la kupigwa risasi Tundu Lissu, sio ugaidi, bali ni uhalifu wa kawaida. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Malangahe ametoa madai hayo leo Jumanne, tarehe 11 Januari 2022, akiulizwa maswali na Wakili Peter Kibatala, katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, mbele ya Jaji Joachim Tiganga.
Ni baada ya Wakili Kibatala kumhoji, kwa nini njama za kutaka kumdhuru aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, wanazodaiwa kufanya kina Mbowe, ziitwe za ugaidi na tukio la kushambuliwa kwa risasi Lissu, aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, lisitafsiriwe kama la ugaidi.
Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi, yenye mashtaka ya ugaidi ni, waliokuwa makomandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Adam Kasekwa, Halfan Bwire Hassan na Mohammed Abdillah Ling’wenya.
Tukio la kupigwa risasi Lissu, ambaye kwa sasa ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, lililotokea jijini Dodoma, tarehe 7 Septemba 2017.
Mahojiano ya Wakili Kibatala na Malangahe yalikuwa kama yafuatavyo;
Kibatala: Jana nilisikia hapa unazungumzia kuhusu Lissu kupigwa risasi, je tukio la Lissu kupigwa risasi ni ugaidi au siyo ugaidi?
Shahidi: Siyo ugaidi, ni uhalifu wa kawaida
Kibatala: Kwa ushaidi wako kupigwa risasi kwa Lissu hakukuwatishia wananchi, hakukuwafanya kuwa na hofu kwamba mbunge anapigwa risasi hadharani?
Shahidi: Ugaidi unategemea na tukio
Kibatala: Mwambie Jaji kama umesema ulikuwa uhalifu kama uhalifu mwingine, nani aliyekufahamisha kusudio la waliompiga risasi Lissu mpaka kusema sio ugaidi?
Shahidi: Sio kufahamishwa na mtu, nilisikia
Kibatala: Ulisikia na nani?
Shahidi: Hata katika ofisi yangu, ni suala lililokuwa wazi nchi nzima
Kibatala: Kwa nini kupigwa risasi kwa Lissu isiwe ugaidi na Sabaya kutaka kudhuriwa ni ugaidi, hiyo midhaania uliiitoa wapi?
Shahidi: Sijayaona
Wakili Kibatala alimuuliza maswali hayo Malangahe, baada ya jana tarehe 10 Januari 2022, Wakili wa utetezi John Mallya, kumuuliza kuhusu tukio hilo, kama ifuatavyo;
Mallya: Ukiwa kwenye ofisi ya DCI Septemba 2017 kiongozi mwenzake anaitwa Lissu alishambuliwa na risasi za moto na ripoti za kipolisi zinasema ilikuwa mashine gun unafahamu kuhusiana na hilo?
Shahidi: Kuhusu kushambuliwa nafahamu, kuhusu ripoti sifahamu
Mallya: Ni sahihi hawa wanaotembea na hizo bunduki ni watu ambao wenye mafunzo ya kutumia silaha?
Shahidi: Si kweli, hata wahalifu wanazo
Mallya: Kiongozi mwenzake Mbowe ameshambuliwa na bunduki, Mbowe anatafuta walinzi ambao wanakabiliana na watu hao, wewe hutaki ajilinde na mambo kama hayo?
Shahidi: Kujilinda hili kitu siwezi kulizungumzia, yeye mwenyewe anaweza kuamua, ulinzi wa Polisi upo
Mallya: Wakati Lissu anashambuliwa Jeshi la Polisi lilienda likizo?
Shahidi: Hayo yanatokea na ni uhalifu kama uhalifu mwengine