BEKI mpya wa Yanga, Ibrahim Abdallah ‘Bacca’ amesema licha ya kutua kwenye timu hiyo huku ikiwa na nyota kadhaa wa nafasi anayocheza, lakini bado anaamini kwa kipaji alichonacho atapambana na uamuzi wa mwisho utakuwa kwa kocha wao.
Akizungumza hivi karibuni Bacca alisema anaifahamu Yanga na hajakurupuka kumwaga wino, ila ameona nafasi yake ya kucheza nddio maana akajiunga timu hiyo huku akiweka wazi kuwa anawaheshimu wachezaji wote wa timu hiyo.
“Yanga ni timu ya presha kubwa kutokana na kuwa na mashabiki wengi ambao wanahitaji matokeo mazuri, hilo nalifahamu ila sitafanya makosa nawaomba wanipokee na kunipa ushirikiano ili niweze kuwa miongoni mwa wachezaji ambao watafanikisha malengo ya klabu,” alisema Bacca na kuongeza;
“Naheshimu uwezo wa Dickson Job, Bakari Mwamnyeto na kaka yangu Abdallah Shaibu ‘Ninja’ kila mmoja ana namna yake ya uchezaji na umuhimu wake kikosini kocha ndiye atakayeamua amtumie na amuache nani kwani hatuwezi kucheza wote.”
Beki huyo kutoka KMKM na aliyeng’ara katika michuano ya Mapinduzi alisema ametumia muda mwingi kuwafuatilia mastaa wanaocheza nafasi yake kwa kuangalia ubora wao na mapungufu yao ili aweze kuwa na vitu vya tofauti vitakavyompa ushawishi kocha kumpa nafasi anaamini hivyo ndio vitampa namba.
“Kucheza timu kama Yanga inahitaji ubunifu kila mchezaji anatamani kupata nafasi kama niliyoipata kwa kusajiliwa kinachofuata ni kujituma na kufanya vitu tofauti na waliokutangulia najiona nikiwa bora na kufanya tofauti,” alisema Bacca.