Mlinda mlango wa zamani wa klabu ya Azam FC, Razak Abalora anakaribia kukamilisha usajili wa kujiunga na klabu ya FC Sherif Tiraspol ya nchini Moldova. Taarifa kwa mujibu wa mtandao wa nchini Ghana wa GhanaSoccerNet.com zimeeleza kuwa, klabu ya Asante Kotoko imefikia makubaliano na klabu ya nchini Moldova ya FC Sherif Tiraspol juu ya kumuuza mlinda mlango wake mwenye umri wa miaka 25, Razak Abalora.
Mara baada ya vilabu hivyo viwili kufikia mwafaka, mchezaji Mghana Razak Abalora anatarajiwa kusafiri kwenda barani Ulaya siku chache zijazo kwa ajili ya zoezi la kufanyiwa vipimo vya afya na kukamilisha usajili wake katika klabu hiyo.
Dau lililotumika kumng’ oa Abalora katika klabu ya Asante Kotoko. Klabu ya FC Sherif Tiraspol imetoa kitita cha dola za Kimarekani laki 3 ambazo ni zaidi ya shilingi za Kitanzania milioni 600 kama ada ya uhamisho wa mlinda mlango wa Asante Kotoko Razak Abalora.
Akiwa nchini Moldova, Razak Abalora anatarajiwa kusaini kandarasi ya miaka mitano na klabu hiyo kubwa nchini Moldova. Klabu ya FC Tiraspol imewahi pia kutumikiwa na kiungo wa sasa wa Simba SC na timu ya taifa ya Malawi, Peter Banda.
Takwimu za Abalore akiwa nchini Ghana katika klabu ya Asante Kotoko (Oktoba 2020- mwanzoni mwa mwaka 2022). Razak Abalora alicheza michezo 27 ya ligi katika kipindi cha msimu mmoja na ½ alipokuwa katika klabu ya Asante Kotoko.
Katika michezo 27 aliyocheza, Abalora aliruhusu mabao 18 na kutoka uwanjani bila ya kuruhusu bao katika michezo 13. Historia fupi ya mchezaji Razak Abalora. Mlinda mlango Razak Abalora alizaliwa Septemba 4, 1996 huko jijini Accra nchini Ghana.
Razak Abalora alianza kucheza soka la ushindani mwaka 2013 alipoitumikia klabu ya West African Football Academy (WAFA) hadi mwaka 2017. Akiwa WAFA, Abalora alicheza michezo 24 ya mashindano. Mwaka 2017, Razak Abalora alisajiliwa na klabu ya nchini Tanzania ya Azam FC.
Akiwa Azam FC Abalora alicheza michezo 100 ya mashindano hadi alipoondoka Azam FC mwaka 2020. Na mwishoni mwa mwaka 2020, Abalora alisajiliwa katika klabu ya nchini kwao Ghana ya Asante Kotoko na kucheza michezo 36 ya mashindano.
Pia, kati ya mwaka 2020 hadi 2022, Abalora aliitwa na kuitumikia timu ya taifa ya Ghana, Black Stars katika michezo minne.