Kumekucha..Kesi Kupinga Kujiuzulu Ndugai Kunguruma Kesho



MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam inatarajia kesho kuanza kusikiliza shauri la kikatiba la kupinga kujiuzulu kwa aliyekuwa Spika wa Bunge Job Ndugai na mchakato wa kupata mwingine kwa madai utaratibu ni batili.

Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia (wapili kushoto), akizungumza na mawakili wake katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam jana, baada ya kufungua kesi ya kupinga mchakato wa kujiuzulu kwa aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai. PICHA: JUMANNE JUMA
Uamuzi huo wa Mahakama ulitolewa jana mbele ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji John Mugeta.

Katika kesi hiyo iliyofunguliwa na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, mdaiwa namba moja ni Job Ndugai, wapili ni Bunge na wa tatu ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mdaiwa wa pili na watatu wanawakilishwa na Mawakili Wakuu wa Serikali, Mussa Mbura, Deodatus Nyoni, Andrew Chang'a na Wakili wa Serikali, Stanley Kalokola.

Shauri hilo lilitakiwa kuanza kusikilizwa jana, lakini Ndugai hakuwapo wala wakili wake.


Wakili wa Serikali Mkuu, Mussa alidai shauri lilikuja kwa ajili ya kusikilizwa, lakini mdaiwa wa kwanza Ndugai hakuwapo na upande wa serikali haukuandaa majibu ya kiapo kinzani kwa sababu walipata taarifa jioni.

Wakili Mussa aliomba wapewe siku 14 ili wajibu na kwamba tukio la kujiuzulu Spika lilitokea Januari 6, mwaka huu na kesi ilifunguliwa Januari 21, walalamikaji Mbatia walipata muda wa siku 14 kuandaa kesi na hawaoni kama kuna dharura.

Wakili Mpare Mpoki akijibu, alidai dharura ipo kwa sababu kuna uchaguzi wa Spika wanauwahi, akichaguliwa mwingine kutakuwa na maspika wawili.


"Tunachoharakia uchaguzi wa Spika usifanyike, busara ya mahakama hii inatakiwa itoke kabla ya uchaguzi wa spika Januari 31, mwaka huu.

"Mahakama pekee ndiyo inayoweza kusimamisha uchaguzi wa Spika, hati ya wito waliyopewa serikali ilikuwa kesi inasikilizwa (leo) jana, hivyo walipaswa kuandaa majibu ya kiapo," alidai Mpoki.

Mahakama ilizingatia hoja na umuhimu wa suala lililoko mbele yake, ikaagiza mjibu maombi wa kwanza Ndugai apelekewe hati ya wito mkononi sio kwa email kama ilivyofanyika, kabla ya leo saa 8.30 mchana, majibu upande wa serikali yafike muda huo.

Jaji Mugeta aliahirisha shauri hilo hadi kesho kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.


Mbatia anapinga utaratibu uliotumiwa na aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai kujiuzulu na mchakato wa kupata spika mwingine.

Kesi hiyo ya kikatiba namba mbili ya mwaka 2022 ilifunguliwa chini ya hati ya dharura na inasikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu.

"Katiba imeweka utaratibu, Spika akitaka kujiuzulu anatakiwa kwenda kufanya hivyo kwa watu waliomchagua ambao ni wabunge.

"Utaratibu uliotumiwa na Ndugai ni batili haukubaliki kikatiba," alidai Mbatia.


Mbatia anawakilishwa na jopo la mawakili 10 akiwamo Wakili Mpare Mpoki, Jeremiah Mtobesya.

Ndugai alijiuzulu uspika Januari 6, mwaka huu na Januari 21 mwaka huu, Dk. Tulia Ackson aliteuliwa kugombea nafasi hiyo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad