Kumekucha...Vita urais 2025 kung’oa vigogo



RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema atafanya mabadiliko hivi karibuni katika nafasi mbalimbali ndani ya serikali yake ikiwamo Baraza la Mawaziri, ili kuondoa waliojiingiza kwenye makundi ya urais mwaka 2025.

Lengo la mabadiliko hayo, kwa mujibu wa Rais Samia, ni kuwapa nafasi ili kuendelea kujipanga na mbio zao badala ya kuharibu utendaji kazi. Hatua hiyo, amesema itampa nafasi ya kuwateua watu watakaomsaidia katika kuiongoza serikali ambayo aliapa kuwa atawatumikia Watanzania.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa kupokea ripoti ya utekelezaji wa miradi kupitia fedha za UVIKO -19, alisema kuna baadhi ya viongozi wa serikali, wakiwamo mawaziri, badala ya kutekeleza majukumu yao wanajipanga kwa ajili ya mbio za urais mwaka 2025.

Pia alisema safu za uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) zikiwamo za ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na wenyeviti wa ngazi mbalimbali zimeanza kuandaliwa lengo likiwa kujipanga kwa ajili ya urais.

“Baadhi ya mawaziri na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi wameanza kujipanga kwa ajili ya 2025 badala ya kujikita kwenye maendeleo ya Watanzania. Hao wanapiga kelele wala hawanisumbui. Watanzania wapuuzeni na kuwasamehe.


“Wanasema ‘don’t judge a book by its cover’ (usikitathmini kitabu kwa kuangalia sura yake), wamenitazama nilivyo wakasema wanijaribu. Wamekosea hapa sipo. Lakini uzuri ni kwamba nilitoa ufafanuzi siku moja kilichofuata wenye nchi wamejibu, hicho ndicho kilichonipa moyo na kuendelea,” alisema.

Rais Samia, ameweka watu katika nafasi mbalimbali kumsaidia kuwaletea wananchi maendeleo, wakiwamo mawaziri, wakuu wa mikoa na makatibu wakuu, lakini badala ya kufanya yale aliyokusudia wanafanya tofauti.

“Nimekaa ni mwezi wa nane sasa nilisema nilikuwa nawasoma nanyi mnanisoma na siku niliyofanya mabadiliko madogo nilisema hapa nimeweka nukta kazi inaendelea. Nataka niwaambie nitatoa ‘list’ (orodha) karibuni.


“Wale wote ninaohisi wanaweza kwenda na mimi kwenye kazi ya maendeleo ya Watanzania nitakwenda nao, lakini wale wote ninaohisi ndoto zao ni kule (urais), wanafanya kazi kwa ajili ya kule, nitawapa nafasi waendelee wakajitayarishe vizuri huko nje kwa sababu nikiwatuma ndani itawasumbua. Bora niwape nafasi wakajitayarishe tukutane huko mbele ya safari,” alisema.

Hata hivyo, aliwashangaa watu wanaojipanga na kuunda makundi kwa ajili ya urais mwaka 2025 kuwa muda bado ni mrefu labda wangesubiri kuliko kuanza sasa.

ANGEWASHANGAA

Katika hatua nyingine, Samia alisema: “Ukiona adui yako anapiga kelele, jua umemshika pabaya. Nisingeshangaa kama adui yangu asingepiga kelele.

“Inanikumbusha hadithi moja mtu mmoja wakati nikiwa Makamu wa Rais, nilivyotwishwa huu mzigo alinitafuta akaniambia nimekuja kukupa hongera, lakini pole. Lakini nataka nikwambie atakayekusumbua kwenye kazi yako na uongozi wako ni shati la kijani mwenzio na wala si mpinzani. Mpinzani atakutazama unafanya nini ukimaliza hoja zao hawana maneno. Lakini shati la kijani mwenzio anayetazama mwaka 2025 huyu ndiye atakayekusumbua.


“Nataka niwaambie ndicho kinachotokea kwa sababu huwezi kufikiria mtu niliyemwamini mshika mhimili aende akasimame aseme yake, ni stress (msongo wa mawazo) ya 2025. Lingine wakati mmenikabidhi huu mzigo (urais) nilianza kusikia serikali ya mpito! Serikali ya mpito! Bungeni kwa kina Kassim (Majaliwa) (Waziri Mkuu), nikarudi kwenye Katiba nikaangalia serikali ya mpito imeandikwa wapi, ikitokea nini kunakuwa na serikali ya mpito, sikuona.

“Lakini watu wakatazama mtu aliyeshika kitabu kuapa wakamfanyia tathmini, wakamfanyia yote waliyoyafanya wakampa daraja wakamuweka pale. Sasa yanayotokea hawaamini yule mtu waliyempa ile thamani ndiye anafanya, kwa maana hiyo hamu na tamanio lao la 2025 linaanza kuondoka.”

Alisisitiza kuwa atajitahidi kila fursa itakayoletwa kutoka duniani ambayo anaweza kuitumia kuleta maendeleo na kwamba atafanya hivyo kwa sababu aliapa kwa Mungu kuwatumikia Watanzania na wala hafanyi hivyo kwa ajili ya mwaka 2025.

“Ningeanza hivi 2023 ili niwaambie mmeona, nimeanza sasa miezi sita na 2025 iko mbali. Yanayofanyika sasa 2025 wananchi watakuwa wamesahau. Utaanza kuwakumbusha hadi koo (makoo) zitakauka (yatakauka).


“Lengo letu ni maendeleo kwa Watanzania, uongozi huletwa na Mungu, aliyepangiwa ndiye atakayekaa. Letu sisi ni kujenga Tanzania, twende tukajenga Tanzania,” alisisitiza.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad