Job Ndugai Spika wa Bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania
NAFASI iliyoachwa wazi ya Uspika wa Bunge la Tanzania na Job Ndugai, imeendelea kushindaniwa na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao wamefikia 49. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma…(endelea).
Ndugai aliyeongoza muhimili huo wa Bunge kuanzia Novemba 2015, alitangaza kujiuzulu nafasi hiyo tarehe 6 Januari 2022 baada ya kauli yake kuhusu serikali kuendelea kukopa kuibua mjadala mkali ndani ya chama chake.
Wenyeviti wa mikoa, makada wa CCM na baadhi ya viongozi wa Serikali walipinga kauli hiyo na kumshinikiza kujiuzulu naye akafanya hivyo.
CCM ilitangaza kuanza mchakato wa ndani wa kupata mrithi wa Ndugai ambaye ni mbunge wa Kongwa mkoani Dodoma na kuanzia tarehe 10 hadi 15 Januari 2022 ni shughuli ya uchukuaji na urejeshaji fomu za kuomba kuteuliwa.
Ikiwa kesho Jumamosi ndiyo siku ya mwisho wa utolewaji fomu, tayari wanachama 49 wamechukua fomu na kukifanya chama hicho kujikusanyia Sh.49 milioni zinazotokana na fomu hizo ambazo gharama yake ni Sh.1 mlioni.
Idadi hiyo ya wanachama 49 ilifikiwa jana Alhamisi ambapo wanachama 19 walichukua fomu hizo zinazotolewa maeneo matatu, makao makuu ‘White House’ jijini Dodoma, Lumumba jijini Dar es Salaam na Ofisi Kuu ya CCM Zanzibar.
Katibu msaidi mkuu idara ya oganaizeshe wa CCM, Solomon Itunda aliwataja waliochukua fomu jana ofisi kuu Dodoma ni mbunge wa zamani wa Msalala mkoani Shinyanga, Ezekieli Maige, Emmanuel Paul Mng’arwe, Azizi Sadi Mussa, Onyango Otieno na Doto Balele Mgasa.
Wengine ni, Profesa Edson Lubua, Fikiri Avias Said, Dk. Itikija Elirehema Mwanga pamoja na Peter Wilbard Njemu.
Alisema waliochukua ofisi ndogo ya Lumumba ni, Ndurumah Majembe, Godwin Maimu, Johnsone Japhet, Mohammed Mmanga, Ester Mkazi, Mariam Koja, Joseph Anania, Samweli Xaday, Anold Peter na Joseph Sabuka.
Mara baada ya kuchukua fomu, Maige aliyewahi kuwa waziri wa maliasili na utalii alisema ana uzoefu bungeni kwa zaidi ya miaka 15 na kwa sasa linahitajika Bunge lisilo na ushabiki wala kubagaza serikali.
“Nina uzoefu bungeni, nimeziishi kanuni za Bunge, najua azma ya serikali ya kuleta maendeleo kwa nchi, nimeona ni muda sasa kuunga mkono chama kwa kuwajibika, nitaishauri Serikali kuhusu mipango mbalimbali,” alisema.
Kwa upande wake, Wakili Emmanuel Mng’arwe alisema ametafakari na kuona anafaa ndio maana amechukua fomu kugombea Uspika.
Alisema akipata nafasi huyo atahakisha analisaidia Bunge kutunga sheria za nchi kwa kuwa ana uzoefu na anakidhi matakwa ya kisheria na katiba inamruhusu kugombea.
Wakili Otiano kutoka Tarime alisema ameamua kuchukua fomu kwa sababu uwezo anao na kwa kuwa Bunge linaongozwa kwa mujibu wa sheria watashauri serikali kuhusu masuala mbalimbali kwa lengo la kuleta maendeleo na kwamba watafanya marekebisho yanayotakiwa kwenye sheria zetu zilizopo.
Mhadhiri mwandamizi kutoka Chuo Kikuu Cha Uhasibu Arusha, Profesa Edison Lubua alisema ana uzoefu na anakifahamu chama ndio maana amejitokeza kuchukua fomu kugombea nafasi hiyo.
“Najiamini naweza maana wananchi wanategemea sera zinazogusa maisha yao zilizochambuliwa kitaalamu na kufanyiwa kazi na bunge,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi wa zamani, Fikiri Said ambaye pia ni mwalimu alisema kilichomsukuma kuchukua fomu ni kutokana na kuyaishi maono ya Watanzania na ameona kuna masuala ambayo anaona anaweza kuyafanyia kazi bungeni kwa mujibu wa sheria na kanuni hivyi kuwaataka watanzania wategemee binge la kisayansi.
Naye Ofisa mwandamizi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Doto Mgasa alisema amevutiwa na namna ambavyo Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anafanya kazi hivyo kuwafanya wanawake kuwa na udhubutu.
“Rais Samia amenifanya nijiamini na kuja kuchukua fomu maana uwezo ninao na kwa sababu bunge linaongozwa kwa miongozo iliyowekwa naamini naweza,”alisema.