Dodoma. Mbunge wa Jimbo la Mvumi Mkoa wa Dodoma (CCM), Livingstone Lusinde amemtaka Spika wa Bunge Job Ndugai kujiuzulu kabla siku ya leo kuisha.
Akizungumza na Mwananchi leo Januari 6, 2022 Lusinde amesema anamtaka Ndugai kuchukua hatua hiyo baada ya kujiridhisha kwa kupitia video nzima ya hotuba Spika Ndugai aliyoitoa hivi karibuni kwenye mkutano wa Wagogo wa Kikundi kinachofahamika kama Wanyausi.
“Napenda kusisitiza hilo na namtaka leoleo kabla ya siku kuisha awe amejiuzulu kwasababu haiwezekani mtu unaomba msamaha kwa kujitetea.. msamaha hauombwi hivyo kwa kuanza kukanusha kosa ilibidi aongee maneno machache tu” amesema
Lusinde amesema mikopo aliyoizungumzia Spika Ndugai anayokopa Rais hatumii na familia yake bali hutumika nchi nzima kwenye kuboresha miradi ya maendeleo.
Aidha amesema ikiwa itapita siku ya leo Spika atazidi kuweka msuguano usio na sababu kwakuwa vikao vya Kamati ya Bunge vinatarajia kuanza hivyo si vema kuanza vikao hivyo kukiwa na mgogoro.
“Na kwakuwa hajachukua hatua siku zote ndo maana nimemtaka leo mimi kama mdogo wake atoke na kuchukua hatua mapema kwakuwa vikao vya Bunge muda si mrefu vitaanza”amesema
Pia amesema kitendo cha Ndugai kujiuzulu ni kuwaletea heshima viongozi wa Mkoa wa Dodoma na itasaidia viongozi wa mkoa huo kutokuchukiwa na Rais.
Lusinde amesema kama Ndugai hatajiuzulu mpaka kesho Ijumaa, atakusanya wazee maarufu wa Mkoa wa Dodoma kwenda nyumbani kwake kumuomba ajiuzulu.