Maafisa saba wa Polisi wapandishwa kizimbani kwa tuhuma za mauaji
JESHI la Polisi Mkoani Mtwara limewakamata na kuwafikisha mahakamani Maafisa wa Polisi saba kwa tuhuma za mauaji ya Mussa Hamisi Hamisi (25) mkazi wa Kijiji cha Ruponda wilayani Nachingwea Mkoani Lindi aliyekuwa akiwadai askari hao zaidi ya Sh milioni 33.7.
Inadaiwa maafisa hao wa polisi walijipatia kiasi hicho cha pesa wakati wakimfanyia upekuzi mfanyabiashara huyo.
Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara, ACP Marck Njera imesema mauaji hayo yalifanyika Januari 5, 2022 na mwili wa marehemu ulitupwa kitongoji cha Majengo kijiji cha Hiari Wilayani Mtwara.
Maafisa wanaoshikiriwa ni Mrakibu wa Polisi Gilbert Kalanje -Mkuu wa Upelelezi wa wilaya ya Mtwara, Mrakibu Msaidizi wa Polisi Charles Onyango - Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtwara, Mrakibu wa Polisi Msaidizi Nicholaus Kisinza - Mkuu wa Kikosi cha Intelejensia ya Jinai mkoa wa Mtwara, Mkaguzi wa Polisi John Msuya Mganga - Mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara, Mkaguzi wa Polisi Msaidizi Marco Mbuta, Mkaguzi wa Polisi Shirazi Mkupa na Koplo Salimu Juma Mbalu.
Uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea.
Source: habarileo.co.tz