Madereva 31 wa mabasi ya abiria watozwa faini




Dodoma. Jeshi la Polisi mkoani Dodoma limewatoza faini madereva 31 kwa kuzidisha mwendo na kuyapita magari mengine bila tahadhari barabarani.

 Mabasi matatu yameondolewa vibao vya namba baada ya kubainika kuwa yanahitaji matengenezo kabla ya kuendelea kutoa huduma.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Januari 19, 2022 na Mkuu wa Kikosi cha Usalama wa Barabarani, Wilbroad Mutafungwa baada ya kufanya ukaguzi katika kituo kikuu cha mabasi yaendayo mkoani cha Nanenane.

Amesema madereva hao wametozwa faini mkoani Dodoma katika operesheni inayoendeshwa nchi nzima.


 
Pia amesema mabasi yanayomilikiwa na kampuni za ABC, Abood na Kapricon wamefungiwa leseni zao kwa kosa la kuzidisha mwendo.

Kwa kawaida mwendo unaotakiwa ni kati ya 80 kwa saa na 50 katika maeneo ya makazi ya watu.

Hata hivyo, Mutafungwa amesema mabasi yanayomilikiwa na Kampuni za Machame na Adventure yamekabidhiwa kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu (Latra) kwa ajili ya kuangalia mfumo wa udhibiti mwendo.


“Tumeshindwa kusoma vizuri speed (kasi) ya haya mabasi, tumeyakabidhi kwa Latra ili waangalie tusijekuwaadhibu kwa kuwaonea,”amesema.

Mutafungwa amewaonya madereva waliositishiwa leseni kuepuka kuendesha magari na kwamba wakikutwa wanaendesha magari watachukuliwa hatua za kisheria wao na wamiliki wa magari hayo.

Pia mkuu huyo aliwataka madereva nchini kuzingatia sheria za barabarani ili kuepusha ajali.

Ametaja mambo matatu yanayoonekana kusababisha ajali ikiwa ni mwendokasi, upitaji magari mengine kusiko sahihi na tamaa za kifedha ambazo hufanya dereva wa safari ndefu kuendesha kwa muda mrefu bila kupumzika.


 
“Wamiliki waache kujielekeza katika faida tu, wajali usalama wa abiria kwa kupanga madereva wawili kwa safari ndefu za vyombo vyao,” amesema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad