Magufuli atajwa tena kesi ya Sabaya shahidi akitoa maelezo
AFISA Uchunguzi wa Takukuru ambaye ni Shahidi wa 13 upande wa Jamhuri katika kesi ya Uhujumu Uchumi inayomkabili Lengai Ole Sabaya amedai mshtakiwa alijitambulisha kama “Kikosi Kazi Maalumu” kilichoundwa na Hayati Rais John Magufuli kushughulikia wakwepa kodi alipokuwa kwa mfanyabiashara Fransis Mroso.
Ole Sabaya anatumikia kifungo cha miaka 30 gerezani kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha. Yeye na wenzake sita pia wanakabiliwa na tuhuma za uhujumu uchumi na shauri lao bado linaendelea katika Mahakama ya Hakimu Makazi Arusha.
Akitoa ufafanuzi mbele ya mahakama, Ramadhan Juma ameiambia Mahakama kuwa Sabaya alimwambia mfanyabiashara huyo kuwa yeye ni Kikosi kazi maalumu kilichoteuliwa na Rais na kwamba maneno hayo aliwaaminisha washtakiwa wengine kwenye kesi hiyo, John Odemba na Jackson Macha.
Juma ameendelea kutoa ushahidi akidai kuwa Sabaya alifanya tendo la utakatishaji fedha kwa kutoa mgao wa pesa kwa vijana wake katika Hoteli ya Tulia iliyopo Arusha majira ya Saa 2 usiku. Pesa hizo zilikuwa ni zile alizopata kutoka kwa Mfanyabiashara, Mroso.
Mahakama haikupokea ushahidi wa picha za video uliokuwa utolewe na Afisa mpelelezi huyo ambao unadaiwa video hiyo ilirekodiwa tarehe 22 Januari, 2021 siku ambayo indaiwa Sabaya alimlazimisha Mfanyabiashara huyo kutoa rushwa ya Sh milioni 90.
Kulingana na uchunguzi wake na mahojiano na watuhumiwa wengine, Nathan Msuya, Jackson Macha na John Odemba, Sabaya alitumia kiasi cha fedha kilichosalia baada ya mgao kununua gari binafsi yenye usajili T 222 BDY Toyota V8 kutoka kwa Mfanyabiashara Sabri Abdallah Sharif jijini Dar es Salaam.
Shahidi aliendelea kuieleza Mahakama kuwa, Sabaya hakuwa na chanzo kikingine kama biashara ama mkopo wa benki kumwezesha kununua gari hilo. Zaidi aliongeza kuwa mtuhumiwa alinunua gari hilo siku kumi baada ya kupokea rushwa hiyo kutoka kwa Mroso.
“Sabaya akiwa kama Mkuu wa Wilaya alitumia madaraka yake vibaya na hakua akiheshimu mamlaka yake ya juu ambayo ni Mkuu wa Mkoa,” Juma alisema katika ushahidi wake akisema taarifa hiyo ni kwa mujibu wa maelezo ya Katibu Tawala Msaidizi wa Wilaya ya Hai kwa wakati huo.