KUTOKANA NA kifo cha aliyekuwa Ofisa wa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara, Grayson Mahembe, anayedaiwa kujinyonga akiwa mahabusu, baba yake mzazi ameeleza mambo manne yenye utata juu ya tukio hilo.
Mahembe alikuwa miongoni mwa maofisa wa polisi waliokuwa wanashikiliwa kwa tuhuma za mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamisi (25) mkazi wa Kijiji cha Ruponda, Nachingwea mkoani Lindi, aliyeuawa Januari 5, mwaka huu.
Inadaiwa kuwa askari hao walimpora mfanyabiashara huyo madini yenye thamani ya Sh. milioni 70 kisha kumuua kwa kumchoma kwa sindano ya sumu na hatimaye kumtupa katika kitongoji cha Majengo, kijiji cha Hiari wilayani Mtwara.
Kutokana na kifo cha ofisa huyo, baba yake mzazi, Gaitan Mahembe, amefunguka na kusema hajaridhishwa na taarifa za kifo cha mtoto wake, huku akimwomba Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Simon Sirro, kuingilia kati.
Akizungumza juzi Tabata Segerea jijini Dar es Salaam alipohojiwa na kituo kimoja cha televisheni, baba mzazi wa kijana huyo ambaye ni ofisa mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), alisema: “Nilipewa taarifa kwamba mwanao ameshikiliwa kwenye maabusu ya polisi tarehe 22 (Januari). Baadaye nikapigiwa simu kwamba bahati mbaya amefariki (dunia) amejinyonga akiwa maabusu. Ilinishtua kidogo.”
“Hatua ambazo walizochukua wao walifanya jambo haraka haraka. Kidogo wakaniuliza mwili upelekwe wapi? Ameandika kwao ni Iringa, nikawaambia ninakaa Dar es Salaam, uletwe Segerea.”
Kutokana na kauli ya mzazi, mambo kadhaa yameibua utata kuhusu kifo cha askari huyo yakiwamo;-
NDUGU KUTOSHIRIKISHWA
Mzee Mahembe ameibua hoja kwamba kuna usiri mkubwa juu ya kifo mwanawe ambaye ameacha mjane na mtoto mdogo kutokana na ndugu wa karibu kutokushirikishwa baada ya tukio la kujinyonga.
Alisema jambo lililoishtua famila ni kwamba walipewa taarifa baada ya kijana wao kuwa tayari amesghafariki dunia kwa kile kilichoelezwa na jeshi la Polisi kwamba amejinyonga.
Kutokana na hali hiyo, Mzee mahembe alihoji iwaje wapigiwe simu na kuelezwa kuwa tayari mwili uko katika chumba cha maiti katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Mtwara ya Igula wakati hata ndugu mmoja hakushirikishwa ili kuthibitisha kwamba kwamba alijinyonga.
MWILI KUTOPIGWA PICHA
Suala lingine alilohoji kutokana na utata wa kifo hicho ni mwili kutokupigwa picha kuthibitisha kuwa mtoto wake amejinyonga.
Mzee Mahembe alisema kutokuwapo kwa picha iliyopigwa na polisi na familia kuonyeshwa kuwa ali[oteza maisha kwa njia zilizoelezwa na polisi kunazidi kuleta utata na maswali yasiyo na majibu.
Alisema polisi walipaswa kupiga picha na upande wa ndugu wa marehemu kuitwa kushuhudia kabla ya kuondolewa.
“Polisi walete picha waonyeshe marehemu alikuwa amejinyonga. Ndiyo maana ninamwomba IGP alifafanue. Inasemekana ukweli wake ndiyo uliomponza na ukweli wake ndio uliosababisha hata hao wengine wasemwe,” alisema huku akifafanua kwamba Grayson alisema kwa nini ateseke peke yake wakati alikuwa anatekeleza maagizo ya wakubwa wake?
MKANGANYIKO MAJERAHA
Jambo lingine llinalozusha utata juu ya kifo hicvho, kwa mujibu wa baba wa marehemu ni mkanganyiko kuhusu majeraha shingoni waliyoonyeshwaq ndugu mwili ukiwa katika chumba cha maiti.
Polisi kaitika taarifa yao, walisema Grayson alifariki dunjia kwa kujinyonga kwa kutumia dekio lililokuwa ndani ya mahabusu hiyo huku ndugu wakitakiwa kushuhudia majeraha ya kamba shingoni wakati mwili uko mochwari.
“Lakini kwa ufupi ndugu waliitwa ikiwa tayari marehemu ametolewa kutoka kwenye tukio kupelekwa hospitalini. Ndugu yetu amekwenda kuona mwili ukiwa hospitalini na kuonyeshwa hapa (shingoni) kuna michubuko ya kamba.
“Hapo kukawa na mkorogano ya kwamba ni kamba si tambala la dekio kama walivyosema. Sasa kwenye maabusu kuna tambala la dekio, siyo maabusu ya uraiani ni maabusu ya wao wenyewe polisi.
Kidogo imenisumbua akili, sijaridhishwa na familia yote haijaridhishwa, ninaomba majadiliano, IGP afafanue ukweli, afuatilie na ukweli uwe wazi,” alisema Mzee Mahembe.
MWILI KUSHUSHWA HARAKA
Akisimulia zaidi, alisema watu hao walifika nyumbani kwake, Tabata Segerea, wakiwa na mkuu wa msafara na wakaingiza gari na kutaka mwili ushushwe haraka haraka. Hatua hiyo pia inaibua utata kwa nini jambo hilo lifanyike kwa namna hiyo?
“Niliwaambia hatuupokei. Ilikuwa vurugu nusura tuanze kupigana, nikawaambia tunaomba mwili huu ukahifadhiwe halafu waje tuzungumze hapa. Wakaenda kuuhifadhi Hospitali ya Jeshi la Polisi iliyoko eneo la Kilwa Road.
“Tuliwaambia safari yetu ni Iringa lakini hatutaupokea mpaka tupate ukweli wa tukio lenyewe. mbaya zaidi ninajua sharia,” alisema.
KUSAFIRISHWA, KUZIKWA KIRAIA
Mzee mahembe pia alisema kilichowashangaza zaidi ni mwili wa kijana wao ambaye ni ofisa wa polisi kusafirishwa kiraia wakati alipaswa kusindikizwa kijeshi kama sharia na taratibu zinavyotaka.
“Hata IGP aseme yule ni ofisa wa jeshi, ilitakiwa asindikizwe kijeshi na akazikwe kijeshi. Hilo halikufanyika amekwenda kama mtu wa kawaida. Ninachoomba uchunguzi ufanyike,” alisisitiza.
Kutokana mkanganyiko huo, Mzee Mahembe alisema kama kuna uwekezano, wanaomba kumpata mwanasheria awasaidie kupata ukweli kwa sababu hakuna picha hata moja inayoonyesha Grayson alikuwa amening’inia amejinyonga.