Ukiitazama hiyo picha inaweza kukushangaza kidogo, straika wa Cameroon anaonekana akiwa anakaribia kufunga, lakini kipa wa Comoros anaonekana akiwa ameweka mikono nyuma.
Ndiyo ameweka mikono nyuma kwa kuwa hajazoea kusimama langoni.
Kipa huyo aliyecheza katika mchezo huo wa Hatua ya 16 Bora ya #AFCON anaitwa, Chaker Alhadhur ambaye kiuhalisia ni beki wa kushoto na ndiyo maana hata wakati anamzuia mshambuliaji huyo alijisahau kama yeye ni kipa ndiyo maana akaweka mikono nyuma ili kutoushika mpira.
#Alhadhur alilazimika kusimama langoni katika mchezo huo kwa kuwa kipa chaguo la kwanza Salim Ben Boina ni majeruhi, makipa wawili wa akiba Moyadh Ousseini na Ali Ahamada wote hawakutakiwa kucheza kwa kuwa inaelezwa walikutwana maambukizi ya Covid-19.
CHAKER ALHADHUR NI NANI?
Beki huyu alizaliwa Ufaransa na akakulia huko katika maisha yake ya awali, akicheza katika timu za Nantes, Caen na Chateauroux kabla ya kutua Ajaccio mwaka 2021.
Umri wake ni miaka 30, alianza kuitumikia Comoros ambapo ni asili yake mwaka 2014.