Dar es Salaam. Matukio ya ajali za moto katika masoko nchini yameibua maswali matano yanayokosa majibu kutoka mamlaka husika, huku yakizidi kuathiri maisha ya wananchi.
Wafanyabiashara na wadau wamehoji mambo yanayotakiwa kupatiwa majibu ili kuzuia matukio hayo au kuwapa wananchi unafuu pindi ajali hizo zinapotokea.
Miongoni mwa maswali yanayohojiwa ni kwa nini masoko hayo huungua usiku? Kwa nini moto haudhibitiwi na kwa nini ripoti za uchunguzi zinazofanyika haziwekwi hadharani?
Maswali mengine ni kuhusu bima za majanga ya moto na funzo linalopatikana baada ya kutokea kwa mfululizo wa matukio hayo.
Vipi kuhusu ripoti za uchunguzi?
Suala la kutowekwa wazi matokeo ya ripoti za uchunguzi zinazofanywa na kamati maalumu zinazoundwa ni jambo linalohojiwa na wananchi, wakitaka kufahamu kilichobainika.
Hali hiyo imesababisha baadhi ya wafanyabiashara kudhani kuna njama zinafanyika dhidi yao kwa madai ya kutaka kuhamishiwa kwenye baadhi ya maeneo.
Wafanyabiashara wadogo wamekuwa wakidai kupitia kipindi kigumu kuendesha biashara baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa maelekezo watengewe maeneo maalumu kwa ajili ya biashara zao.
Wakati agizo hilo likitekelezwa, zimetokea ajali kadhaa za moto kwenye masoko mkoani hapa na mikoa mingine, jambo linaloibua hisia tofauti kwa wafanyabiashara.
Tukio la kuungua kwa Soko la Karume linalotumiwa na wafanyabiashara zaidi ya 3,500. Soko hilo liliungua Jumamosi usiku wa Januari 15 mwaka huu na kuteketeza vibanda na mali zote zilizokuwamo.
Ajali hiyo ilisababisha vilio na simanzi kwa wafanyabiashara hao waliokuwa wakisubiri kauli ya Serikali iwape matumaini.
Kutokana na soko hilo kuungua, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla alitangaza kuunda kamati ya kuchunguza tukio hilo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Innocent Bashungwa alitembelea eneo la tukio na kuagiza uchunguzi huo ukamilike ndani ya siku saba ili chanzo kifahamike.
Hata hivyo, wafanyabiashara wa Karume hawajafurahishwa na mpango wa Serikali kuunda kamati kwa madai uzoefu unaonyesha zinaundwa, lakini hakuna chochote wanachoambiwa.
Najma Malick, ambaye ni mfanyabiashara katika soko hilo, alisema wamechoshwa na utaratibu wa Serikali kuunda kamati kila linapotokea janga la moto huku akikumbushia kuwa, mwaka 2014 soko hilo lilipoungua walifanya hivyo, lakini majibu hayakurudi.
“Mwaka 2014 lilipoungua hili soko, kuna kamati iliundwa lakini hadi sasa hatujapata majibu yoyote, sasa hii nyingine wanaunda ili kutoa majibu gani? Naona wanatupotezea muda tu,” alisisitiza Najma.
“Mtu ambaye yuko ofisini hajui machungu tunayoyapitia sisi, mimi nina watoto watatu wananitegemea kwa kila kitu. Wengine sisi maisha yetu ndio hapa, sasa unatupa siku saba tufanyaje.”
Usiku wa Jumamosi ya Julai 10, 2021, Soko Kuu la Kariakoo liliungua na kusababisha hasara kwa wafanyabiashara wa soko hilo. Wakati wakiomboleza kupoteza mitaji yao, Serikali ilichukua hatua ya kuwahamishia kwenye masoko mengine ya Kisutu na Machinga Complex.
Rais Samia aliviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina kujua chanzo cha moto uliotokea usiku huo katika Soko la Kariakoo ambalo limekuwa kitovu cha biashara nchini.
Julai 27, 2021 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokea taarifa ya kamati ya uchunguzi wa tukio la moto uliotokea katika soko la kimataifa la Kariakoo na kuahidi kuiwasilisha taarifa hiyo kwa Rais Samia kwa sababu tukio hilo limewagusa watu ndani na nje ya nchi.
Tangu siku hiyo, ripoti ya uchunguzi wa chanzo cha ajali ya moto katika soko hilo haijatolewa, badala yake Serikali imetoa Sh32 bilioni kwa ajili ya kukarabati soko la zamani na kujenga soko jipya.
Kwa nini yanaungua usiku?
Wananchi wanahoji mfululizo wa masoko kuungua usiku huku wakihusisha matukio hayo na hujuma dhidi yao kwa sababu wako kwenye mgogoro na Serikali inayotaka kuwahamisha.
Tukio la kuungua kwa Soko la Karume lilitokea Jumamosi usiku na Soko Kuu la Kariakoo pia liliungua Jumamosi. Pia, masoko mengine likiwamo la Mwenge liliungua Jumamosi.
Mfanyabiashara katika Soko la Karume, Anneth Haule alihoji sababu za masoko mengi kuungua Jumamosi usiku, siku ambayo wafanyabiashara wanapumzika na kukaa na familia zao Jumapili.
“Lakini tunajiuliza kwa nini soko linaungua kila Jumamosi? Mwaka 2014 ilikuwa pia Jumamosi, nadhani kuna kitu kinaendelea hapa, kwa sababu wafanyabiashara wengi huwa Jumapili hawaji na ndiyo maana wanafanya hivi ili kusiwe na uokoaji wa haraka,” alidai Anneth.
Kwa nini moto haudhibitiwi?
Hili ni swali jingine linaloibuliwa na wafanyabiashara na wadau, huku wakikitupia lawama Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji kwa kuchelewa kufika na wakifika hawana maji kwenye magari yao.
Mfanyabiashara katika soko la Karume, Anneth alihoji sababu za kikosi hicho kuchelewa kufika eneo la tukio na hata wanapofika wanadai magari yao hayana maji, hivyo kukwamisha juhudi za uokoaji.
“Wamepigiwa simu moto ulivyoanza kuwaka tu, lakini wamekuja kufika baada ya saa mbili tena wanasema gari halina maji. Yaani kama wangewahi, kuna baadhi wangeweza kuokoa vitu vyao,” alisema Anneth, ambaye amepoteza mali zenye thamani ya zaidi ya Sh20 milioni katika tukio la moto soko la Karume.
Hata hivyo, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Ilala, Elisa Mugisha alisema taarifa za moto huo walizipata mapema baada ya kupigiwa simu na mtu mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Hellen Mlay.
“Na kwa bahati nzuri wakati huo tulikuwa tunatoka Mabibo ambako kuna nyumba ilikuwa inaungua moto, tulifika hapa ndani ya muda mfupi,” alisema Kamanda.
“Tulifika eneo la tukio lakini moto ulikuwa mkali kutokana na asili ya bidhaa wanazouza hapa...kuna mbao (meza na vibanda), maturubai na nguo...na vinasambaza moto kwa haraka, tulijitahidi kuzunguka soko na kuanza kuzima,” alisema.
Kamanda huyo alisema vibanda vimeungua kwa asilimia 98 na mali zilizokuwamo, ni wachache waliofanikiwa kuokoa bidhaa zao, hasa walioko pembezoni mwa soko. “Tunachoshukuru Mungu hakuna madhara kwa binadamu na wala moto haukuvuka kwenda kwenye nyumba na wananchi kwa sababu tulikuwa na gari nne, moja kutoka Kinondoni, Ilala, Bandari na Airport,” alisema Kamanda Mugisha.
Vipi kuhusu bima?
Suala la bima lina nafasi kubwa katika biashara hizi, ili yanapotokea majanga kama haya wahusika wanafidiwa mali walizopoteza.
Hata hivyo, wafanyabiashara wameeleza kwamba hawana elimu ya kutosha kuhusu bima.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Ismail Feisal alisema asilimia kubwa ya wafanyabiashara wa Soko la Karume hawana bima kwa kuwa hawana elimu kuhusu masuala hayo. “Hatuna elimu ya masuala ya bima na wala hakuna kampuni yoyote ya masuala ya bima iliyokuja kutupa elimu hiyo. Nadhani ni wakati mwafaka wa sasa kampuni hizo kuja kutusaidia,” alisema Feisal.