MATUKIO ya mauaji yameendelea kwa kasi baada ya watu wasiojulikana kuua kwa kuchinga.
Kutokana na tukio hilo lililotokea Januari 17, mwaka huu, Jeshi la Polisi mkoani humo, limesema linawasaka watu hao kwa tuhuma za mauaji baada ya kutokomea kusikojulikana.
Jeshi hilo limesema tukio hilo linadhaniwa kutokea usiku wakati mama huyo na watoto wake wakiwa ndani ya nyumba yao, watu waliotekeleza mauaji hayo kuingia ndani.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa, Theopista Mallya, alisema mume wa mwanamke huyo ambaye yuko Dar es Salaam alianza kumtafuta mkewe Januari 21 kwa kumpigia simu, lakini ilikuwa inaita bila kupokelewa.
Alisema alipopiga kwa muda mrefu simu hiyo ilizima, hali inayoonyesha kuwa ilizima kwa kuishiwa chaji na kila alipojitahidi kupiga haikupatikana.
Baada ya hapo alimpigia rafiki yake, Paul Leonard, na kumwagiza aende akaione familia yake na alifika nyumbani hapo saa 2:30 usiku na alishangaa kukuta mlango umefungwa nje kwa kufuli, hivyo aliamua kuwaita viongozi wa kijiji na walipofika na kubomoa mlango na kuingia ndani walikuta mwanamke huyo aliyekuwa na ujauzito wa miezi minane akiwa amechinjwa pamoja na watoto wake Milliam (8) na William (4).
Mallya alisema wanatafuta ushahidi kwa kuwatafuta watu waliokuwa na mwanamke huyo kwa mara ya mwisho.
Katika toleo la jana Nipashe liliripoti watu watano wa familia moja, wakazi wa Kijiji cha Zanka wilayani Bahi mkoani Dodoma kuuawa kikatili na watu wasiojulikana huku miili yao ikikutwa ndani ya nyumba yao ikiwa imeanza kuharibika.
Waliouawa ni Hoseah Kapande ambaye ni baba wa familia hiyo na mkewe, Paulina Kapande. Wengine ni watoto wawili na mjukuu mmoja ambao ni Isack Kapande, mwanafunzi wa kidato cha kwanza, Agnes Kapande, mwanafunzi wa darasa la tatu na mjukuu aliyejulikana kwa jina la Heltony, mwanafunzi wa darasa la nne.