Dar/Mikoani. Nini kinaikumba jamii ya Kitanzania? Hilo ni swali linalogonga vichwa vya watu kwa sasa kutokana na kuongezeka matukio ya mauaji ya kikatili na mengine yakihusisha ndugu wa familia, wakiwamo mume, mke na watoto.
Swali hilo linakuja wakati Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Camillus Wambura akitaja mambo matano yanayosababisha kukithiri kwa mauaji alipozungumza na moja ya vyombo vya habari nchini hivi karibuni.
Mambo hayo ni pamoja na wivu wa kimapenzi, imani za kishirikina, migogoro ya ardhi, tamaa ya mali na migogoro ya familia.
Mwezi Januari pekee kumekuwa na mlolongo wa mauaji karibu kutoka kila kona ya nchi.
Mkoani Dodoma, kulitokea mauaji ya kikatili yaliyofanyika Januari 10, 2022 eneo la Miches ambapo muuguzi wa Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Rufina Komba alikutwa ameuawa nyumbani kwake na watu wasiojulikana.
Katika jiji la Arusha inaelezwa katika mwezi Januari 2022 pekee watu wanne waliuawa, huku Novemba na Desemba 2021 wakiuawa watu wawili na matukio hayo yameibua mijadala na kutaka uchunguzi wa visababishi ufanyike.
Awali wanawake wawili, Ruth Mmasi (46) na Janerose Dewasi (66) waliuawa katika mazingira ya kutatanisha eneo la Njiro jijini Arusha, huku Ruth akidaiwa kuuawa kikatili na mwanawe na kutumbukizwa katika chemba ya choo.
Wakati uchunguzi wa mauaji hayo ukiendelea, vijana wawili, Anold Mushi (19) na Jumanne Selemani (17) wote wakazi wa eneo la California Sombetini jijini Arusha, wanadaiwa kuuawa baada ya kufanya tukio la kukwapua pochi ya mwanamke mmoja.
Katika mkoa mkoa wa Kilimanjaro, mwaka 2021 ulitikiswa na mauaji ya kikatili yanayofikia zaidi ya 20, huku mengine yakihusisha walinda usalama wa Jeshi la Polisi kupigana risasi na wale walinzi wa Suma-JKT nao kutwangana risasi.
Mauaji hayakuishia tu kwa raia, kwani Mei 31, 2021, Askari wa Upelelezi wilayani Mwanga, Linus Nzema aliuawa kwa kupigwa risasi na askari mwenzake na Juni 21, askari wa Suma-JKT, Emmanuel Mallya aliuawa kwa kumiminiwa risasi 4.
Katika mauaji yaliyotokea mkoani Kilimanjaro, wapo ambao walichinjwa kwa kutumia vitu vyenye ncha kali, huku baadhi ya waliouawa ikidaiwa yalihusisha vijana waliolipwa kutekeleza ukatili huo baada ya kutumia dawa za kulevya.
Kwa Januari 2022, ni tukio moja tu lililotokea Rau, nje kidogo ya mji wa Moshi baada ya mwili wa Patricia Ebreck (65) uliozikwa Februari mwaka jana kugunduliwa Januari 9, ukiwa umeshabakia mifupa mitupu.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi mkoa Kilimanjaro, Simon Maigwa ilisema uchunguzi wa awali ulidai mmoja wa watoto wa marehemu akishirikiana na waganga wawili wa kienyeji au jadi, ndio waliofanya mauaji hayo na kumzika kupoteza ushahidi.
Mauaji yalivyotikisa kanda ya Ziwa
Mkoani Mwanza matukio sita ya mauaji ya kikatili yaliripotiwa kati ya Februari, 2021 hadi Januari 19, 2022, huku baadhi ikihusishwa na wivu na wizi.
Katika tukio la Februari, 2021, mtu mmoja anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 40 hadi 42 aliuawa katika tukio lililotokea mtaa wa Kanyerere, jijini Mwanza ambapo wauaji ambao bado hawajajulikana hadi sasa waliacha ujumbe wenye maneno yanayosomeka “Mke wa mtu sumu”.
Mauaji mengine yaliyohusishwa na wivu wa mapenzi ni ya Zacharia Musa (26), mkazi wa mtaa wa Ibisabageni wilayani Sengerema yaliyotokea Februari 21 mwaka jana.
Aprili, mwaka jana Kusekwa George (18) alidaiwa kuuawa kwa kipigo kutoka kwa viongozi na mgambo wa mtaa wa Ihushi Kata ya Kishiri jijini Mwanza, baada ya kutuhumiwa kwa wizi wa malapa.
Mbali na hayo, lakini Aprili 15, 2021 watu wawili waliuawa kwa kushambuliwa na miili yao kuchomwa moto na watu wenye hasira kwa tuhuma za kuiba kuku katika Mtaa wa Bukaga Kata ya Kishiri jijini Mwanza.
Tukio la hivi karibuni lililoibua taharuki jijini Mwanza ni lile la mauaji ya wanawake watatu wanaokadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 18 hadi 30 ambao miili yao ilikutwa pembezoni mwa mto eneo la Nyakato-Buzuruga jijini Mwanza.
Wilayani Misungwi kijana Herman Emmanuel (25), mwendesha bodaboda, mkazi wa kijiji cha Mbele aliuawa na watu wasiojulikana katika tukio lililotokea Desemba 16 mwaka jana.
Wilayani Nzega mkoa wa Tabora kuliripotiwa tukio la mlinzi wa kiwanda cha Machapati, Juma Mgunda (75) kudaiwa kuuawa Januari 4, ambapo sababu ya mauaji hayo ilidaiwa ni kisasi cha mtu aliyetajwa kwa jina la Juma Lyamba aliyekuwa akimtuhumu marehemu kushirikiana na mganga wa kienyeji ambaye hakutajwa kumtorosha mke wake.
Kati ya Juni hadi Agosti, 2021 wilaya za Tarime na Rorya mkoani Mara zilishuhudia matukio mawili ya mauaji, ambapo walinzi wawili wa maeneo ya biashara waliuawa na watu wasiojulikana kwa kukatwa na vitu vyenye ncha kali.
Wilayani Rorya, mchunga mifugo, mkazi wa kijiji cha Ingri Chini aliuawa na watu wasiojulikana akiwa machungani na hivyo kuibua taharuki katika jamii.
Akizungumzia matukio ya mauaji ya kikatili, ikiwemo ya kulipa visasi, wivu wa kimapenzi na kujichukulia sheria mkononi, Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora, Richard Abwao alisema pamoja na matumizi ya sheria kukabiliana na uhalifu, Jeshi hilo pia linatumia kitengo chake cha Polisi Jamii kutoa elimu kwa umma kama njia ya kukabiliana na ukatili ndani ya jamii.
Mauaji yawaibua viongozi wa dini
Kutokana na kukithiri kwa mauaji, hasa mwaka 2021 na mwezi Januari 2022, baadhi ya viongozi wa dini, wamepaza sauti zao wakitaka kuwapo kwa mjadala wa kitaifa wa kujadili sababu za mauaji na ufumbuzi wake.
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo amekwenda mbali na kutaka roho ya ukatili inayojengeka kwa watu wengi sasa, ikemewe kwa nguvu zote akisema uhai wa mwanadamu hauwezi kununuliwa dukani kama pipi.
Akizungumza na gazeti hili jana kuhusiana na mwangwi wa mauaji ya kikatili kusikika kuanzia Kusini hadi Kaskazini mwa Tanzania na Magharibi hadi Mashariki, Askofu Shoo alisema laana ya mauaji haitaishia tu kwa wanaoua wenzao.
“Ni jambo la kukemea, lakini ni jambo la kuchukulia hatua na kutafiti nini kinatokea na hatua gani zichukuliwe kuondoa ukatili katika jamii yetu. Watu wakuzwe na kusisitiziwa kuwa uhai wa mwanadamu haununuliwi dukani,” alisema Askofu Shoo.
Naye Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Alhaji Sheikh Mustapha Shaban alisema kukosa imani, huruma, ucha Mungu na kutopata maneno ya Mungu, ndiyo sababu ya mauaji ya kikatili ambayo yamekuwa yakifanyika maeneo mbalimbali nchini.
“Kutohudhuria katika nyumba za ibada, kukithiri kwa vitendo vya ulevi, tamaa za mali na madaraka bila kujua mtoaji mali na madaraka ni Mungu anayeweza kukupandisha ama kukushusha,” alisema Sheikh Shaaban.
Kwa upande wake Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Tabora, Elias Chakupewa aliwaomba viongozi wa dini kuongeza mafundisho ya kiimani na maonyo kwa waumini kuepusha jamii na matukio ya mauaji.
Wanasaikolojia wafunguka
Mwanasaikolojia katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Erasto Kano alisema katika maisha kila mwanadamu ana matarajio yake katika maisha na kwamba matarajio yanapokuwa kinyume anaweza kupata msongo wa mawazo.
“Anapopata msongo wa akili anapata shida mbili, moja ni ya kisaikolojia na kibaolojia lakini hilo liko katika kibaolojia zaidi,” alieleza mtaalamu huyo.
Naye Julius Ngalema ambaye pia mtaalamu wa masuala ya saikolojia anasema mauaji yanatokana na msongo wa mawazo ambao unamfanya mtuhumiwa kushindwa kujua njia mbadala, huku akisema utumiaji dawa za kulevya na umaskini ni changamoto.
Imeandikwa na Daniel Mjema (Moshi), Sharon Sauwa (Dodoma), Mussa Juma Arusha, Saada Amir na Mgongo Kaitira (Mwanza), Twalad Salum (Misungwi), Daniel Makaka (Sengerema), Robert Kakwesi (Tabora), Beldina Nyakeke na Waitara Meng’anyi (Mara).
Mwananchi