Dar es Salaam. Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia ametia mguu sakata la kutofautiana katika suala la nchi kukopa kati ya Rais Samia Suluhu Hassan na Spika Job Ndugai, akisema sio sahihi Ndugai kushambuliwa bali hoja yake ichukuliwe na kujadiliwa kwa mtazamo chanya.
Pia, amesema mihimili ya Bunge na Serikali ikisigana ndiyo afya katika Taifa.
Mbatia ambaye ni mbunge wa zamani wa Vunjo mkoani Kilimanjaro ameeleza hayo leo Januari 2, 2022 wakati akitoa salamu za NCCR-Mageuzi za kufunga mwaka 2021 na kufungua mwaka 2022, katika mkutano wake na wanahabari uliofanyika makao makuu wa chama hicho, Ilala Dar es Salaam.
Kwa takribani siku kadhaa kumekuwa na mjadala hasa katika mitandao ya kijamii uliosababisha baadhi ya wanaCCM wakiwemo viongozi wa mikoa na jumuiya wa chama hicho, wakimpinga Spika Ndugai kuhusu kauli yake kutounga mkono uamuzi Serikali wa kukopa huku wakimtetea Rais Samia.
Desemba 28 mwaka huu, akiwa Jijini Dodoma katika mkutano wa pili wa wanakikundi cha Mkalile Ye Wanyusi Spika Ndugai alitetea uamuzi wa Bunge wa kuanzisha na kupitisha tozo za miamala ya simu kuliko kuendelea kukopa.
Siku iliyofuata katika utiaji wa saini wa mkataba wa ujenzi wa reli ya kisasa wa SGR uliofanyika Ikulu Dar es Salaam, Rais Samia alisema Serikali itaendelea kukopa ili kukamilisha ujenzi wa reli hiyo kwa awamu nyingine.
Lakini leo Mbatia amewaambia wanahabari, “Haya mambo sio chama kimoja wala mambo ya jikoni, wengine wanasema Ndugai alitakiwa akamnong’oneze Rais Samia. Je akifanya hivyo nani atalipa hilo deni? Haya ni mambo ya maslahi ya umma” amesma Mbatia.
Mbatia amesema sio jambo sahihi Ndugai ambaye ni mbunge wa Kongwa mkoani Dodoma kushambuliwa na kutukanwa bali hoja yake ichukuliwe na kujadiliwa kwa mtazamo chanya.
“Migongana ya Bunge na Serikali ni afya kwa Taifa, mahali penye mawazo kinzani yanachangia Taifa kustawi.Ndugai ametoa hoja kuhusu suala la kukopa na ameonyesha taifa liko wapi katika mchakato huu sasa ni kweli? Amesema Mbatia.
Mbatia amewataka wananchi kutoangalia mtu bali waangalie na kujadali hoja iliyoko mezani badala ya kumshambulia mtu binfasi, “Ndugai wanamtukana tu na kumshambulia tu, lakini ametuamsha kutoka usingizi kwa kusema ukweli,” amesema
“Tusimtukane Ndugai bali tuchukue hoja na kuijadili kwa mtazamano chanya. Mawazo kinzani yenye ukweli yajadiliwe kwa mtazamo chanya. Spika Ndugai amefunguka kuzungumza ukweli hadharani, ” ameeleza Mbatia.