USHINDI wa mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union ugenini juzi huko Tanga umeifanya Yanga izidi kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ikifikisha jumla ya pointi 32.
Matokeo hayo hapana shaka yamezidi kuongeza matumaini ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kulikosa taji hilo katika misimu minne mfululizo iliyopita.
Baada ya kuutafuna mfupa mgumu dhidi ya Coastal Union, huku mahasimu wao Simba jana wakipasuka 1-0 ugenini dhidi ya Mbeya City, Yanga sasa imebakiza mechi saba ngumu ambazo kwa kiasi kikubwa zitaiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu ikiwa itafanikiwa kuibuka na ushindi katika michezo hiyo yote.
Kati ya michezo 18 ambayo Yanga imebakiza, mechi hizo saba ndizo zinaonekana kuwa na presha kubwa kwao kutokana na ushindani wa timu husika pindi zinapokutana na mabingwa hao mara 27 wa Ligi Kuu, ubora zilizo nao sasa pamoja na viwanja ambavyo vitatumika kwa mechi baina yao.
Mechi nyingine 12 hazionekani kama zitakuwa ngumu sana kwa Yanga kulinganisha na hizo sita ambazo bila shaka hata washindani wao wakuu Simba wanazitazama kama fursa kwao ama kuifikia au kuipiku Yanga kileleni mwa msimamo wa ligi.
Mechi hizo saba ni dhidi ya Polisi Tanzania, Mtibwa Sugar, Simba, Azam, Namungo, Biashara United na ugenini dhidi ya Mbeya City.
Licha ya kuwa na mechi moja nyumbani ambako imekuwa haisumbuliwi sana na Polisi Tanzania, Yanga ina mtihani mgumu dhidi ya Maafande hao katika mechi ambayo watacheza huko Moshi kwenye Uwanja wa Ushirika Jumapili hii
Yanga imeonekana kupata wakati mgumu inapokabiliana na Polisi Tanzania ugenini ambapo katika mechi mbili zilizopita za Ligi Kuu ambazo ilicheza hapo, haijawahi kupata ushindi ikishiia kutoka sare tu.
Baada ya hapo itakuwa na mechi nyingine ya ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar ambayo licha ya kutofanya vizuri katika msimu huu, imekuwa na historia ya kuvimbia timu kubwa pindi inapocheza nazo ikiwa nyumbani.
Mechi nyingine ngumu kwa Yanga ni tatu itakazocheza kwenye Uwanja iliouzoea wa Benjamin Mkapa dhidi ya Azam FC, watani wao Simba pamoja na Namungo FC.
Azam FC imeonekana kuzidi kuimarika siku za hivi karibuni na iliwafunga Yanga kwenye Kombe la Mapinduzi huku Simba sio tu ikiwafukuza kwa ukaribu katika msimamo wa ligi bali pia imekuwa na kikosi chenye uzoefu wa mechi ya watani halikadhalika imekuwa moto wa kuotea mbali siku za hivi karibuni.
Mchezo dhidi ya Namungo ni mtihani mwingine kwa Yanga kwani timu hiyo imekuwa na hulka ya kuwavimbia katika uwanja wowote ule wanaokutana na kumbukumbu zinaonyesha katika mechi tano zilizopita za ligi baina yao, hakuna iliyoibuka mbabe na mara zote timu hizo zilitoka sare.
Kibarua kingine kigumu ni mchezo dhidi ya Biashara United wa mzunguko wa pili ambao Yanga itaenda kucheza ugenini kwenye Uwanja wa Karume, Mara.
Mechi tatu zilizopita katika uwanja huo, Yanga imeshinda moja, kutoka sare moja na kupoteza moja na katika mchezo uliopita kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, nusura Biashara iilazimishe sare Yanga ambayo ilisubiria bao la dakika za lala salama la mkwaju wa penalti, kupata ushindi wa mabao 2-1.
Ukiondoa mechi hizo sita, mechi nyingine 12 hazionekani kama zitakuwa kikwazo kikubwa kwa Yanga kwani nyingi itacheza nyumbani na hata zile za ugenini, hazionekani zina ugumu kama wa hizo sita za juu.
Kati ya mechi hizo 12, nane itacheza nyumbani ambazo ni dhidi ya Mbeya City, Kagera Sugar, KMC, Prisons, Mbeya Kwanza, Coastal, Polisi Tanzania na Mtibwa Sugar.
Tatu za ugenini ni dhidi ya Ruvu Shooting, Dodoma Jiji, na Geita Gold.
Urahisi kwa Yanga unaweza kupatikana kutokana na kuwepo pia kwa mechi sita ngumu kwa watani wao Simba ambao ndio wanafukuzana kwenye mbio za ubingwa.
Mechi hizo sita za kibabe za Simba ambazo zinaweza kuirahisishia kazi Yanga ni dhidi ya Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, Polisi Tanzania na Coastal Union ugenini pamoja na mbili katika Uwanja wa Benjamin Mkapa dhidi ya Yanga na Azam FC.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Yanga, Senzo Mazingisa ametamba kuwa timu yake imejipanga kuhakikisha inatwaa ubingwa.
“Tuna timu bora na imara sambamba na benchi bora la ufundi. Yanga ni timu kubwa na itarudisha historia yake msimu huu. Tumejipanga na nina imani tutafanya vizuri,” alisema Mazingisa.
Nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto alisema kuwa mechi zote wanazipa uzito mkubwa na wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi.
“Malengo yetu ni kutwaa ubingwa msimu huu na hakuna mechi nyepesi hasa timu zinapocheza na Yanga hivyo sisi kwa upande wetu hatutodharau mechi yoyote.”