BAADHi ya wadudu hutajwa kuwa chakula bora chenye protini na kilicho chenye ladha nzuri katika jamii mbalimbali. Takriban spishi 20,000 za wadudu huliwa na mataifa kama ya Asia, Amerika Kusini na hata sehemu zingine za Afrika.
Nchini Tanzania, kuna jamii ambazo kula wadudu kama senene, panzi na kumbikumbi ni jambo la kawaida, lakini ukiuliza juu ya mende kuwa chakula ni jambo la kustaajabisha. Saumu Hamisi ambaye anajulikana kama Ummy Doll, ni msichana mwenye miaka 20 kutoka nchini Tanzania, anayeishi Kigamboni Dar es salam.
Msichana huyu amewashangaza watu katika mitandao ya kijamii na hata majirani zake hawaishi kustaajabu na kile ambacho anakifanya kwa jinsi anavyofuga mende sawa kabisa na wanavyofungwa kuku na mifugo mingine mbalimbali.
Mende ni kitoweo chake ambacho anakula kila wiki yaani ni sawa na mtu akiamua kula dagaa au nyama. Kwanini Saumu aliamua kupenda kula mende; “Mimi ni mjasiriamali ninayejishughulisha na biashara ya kufuga na kuwauza mende.
Kutokana na umri wangu kuwa mdogo, kumefanya wengi kushangaa sana na hata wengine kuhoji juu ya afya yangu ya akili. Wengine wanadhani sina akili timamu lakini kwangu mimi naichukulia hii kama biashara na kwa hiyo kila kitu kiko sawa kwangu,” anasema Ummy.
Licha ya kuwa mjasiriamali , msichana huyu ni miongoni mwa watu wanaofuatiliwa kwa karibu katika tasnia ya burudani hasa upande wa ulimbwende na uimbaji. Nyimbo nyingi za Ummy zinagusia masuala ya mahusiano ya kimapenzi hasa ya maisha yake na maswala mengine katika jamii.
Lakini amepata umaarufu kutokana na kuwa mlimbwende anayefurahia kula mende. Mrembo huyu kupenda kula mende kumeibua hisia mbalimbali kutoka kwa jamii inayomzunguka kutokana na tabia yake ya kula mende, na yeye bila kujali maoni ya watu.
“Mimi nakula mende , ni chakula muhimu sana kwangu kwa sababu mende ni mtamu , cha pili mimi kama mjasiriamali wa mende niliona kwamba ni lazima nile ili kuwaridhisha wateja wangu kwamba hiki ni chakula kama chakula kingine, kwa hiyo nakula pia kumhamasisha mwingine aweze kula mende na kuona kuwa ni kama chakula kingine,” Ummy anasema.
Je hao mende huwa anakula na chakula gani?
“Kwanza mende anaweza kumpika kwa namna mbalimbali , unaweza kumuunga kwa nazi , unaweza kumpika kama rosti na unaweza kumchoma kama mshikaki na pia unaeza kumkaanga -unaweza kula menge kwa ugali , wali au hata ndizi zilizochomwa.
Ni sawa kabisa na chakula kingine chochote kile, yaani mende ni kama mboga nyingine ambayo umezoea kula kawaida, kwangu mimi nasikia ladha ya mende ikinijia kama samaki wa kukaanga au kuku aliyekaangwa,” Ummy anaeleza.
Mende ni miongoni mwa wadudu ambao wanakaa katika mazingira ya maliwatoni, na kwa kawaida kutokana na mazingira ambayo huwa wanakaa watu hufanya jitihada za kuhakikisha kuwa hawapo katika mazingira ya nyumbani kwa kuuliwa na kufukuzwa kwa dawa na hata kuweka mazingira ambayo mende hawawezi kuishi.
Wanasayansi wa wadudu wameorodhesha mende kuwa wa aina mbali mbali -na kama ambavyo Ummy alielelezea aina ya mende anaowafuga sio wale ambao wanakuwa kwenye mazingira ya uchafu kwenye makaazi ya watu.
Hata hivyo licha ya kuwa Saumu ni mlaji wa mende lakini ametoa angalizo kwa watu kutookota mende katika mazingira yao machafu kwa mfano mitaro ya maji machafu au sehemu za kabati zilizoachwa vyakula kama unga kwani kuna mchakato ambao mtu anapaswa kuupitia kabla ya kuanza kufuga mende.
“Mende hawa niliwachukua kutoka Morogoro kutoka chuo cha kilimo cha SUA, huko ndiko nilichukua mbegu na kuanza kuwafuga.
Mende hawa ni tofauti sana na wale wa nyumbani , mende hawa ni aina ya Periplaneta americana (American cockroach) – .wanatokana na aina ya mende lakini wao ni tofauti na ndio maana tunawaweka kwenye mazingira ya usafi na ndio maana wanafaa kuliwa.
Ila mende ni mende isipokuwa wale wa nyumbani ni vitu viwili tofauti na wale wa nyumbani hawa hawana madhara , hawana magonjwa katika miili yao kwa sababu mende hazalishi magonjwa isipokuwa mazingira anayoyaishi kutembea tembea kwenye mazingira ya nyumbani ndio maana anabeba baadhi ya vimelea ambavyo vina magonjwa “anasema Ummy.
Mwanadada huyu anasema kuwa kwa upendo wake wa mende anahakikisha kwamba wanaishi kwenye mazingira yanayomfaa kwa mfano anasema kwamba mende wa kufugwa wanafaa kuwa kwenye mazingira ambayo ni giza na pia anahitaji kuwa kwenye joto na chakula cha kutosha wakiwa kwa hali hio hawachukui muda sana kwa kukua na kutaga mayai mengi sana.
“Mende anakula chakula kama kile ninacho kula mimi nampatia wakati mwingine nampatia maharage nasiaga , mara nyingine biriani, mkate na kadhalika yaani wanakula kila chakula” anasema Ummy.
Ummy anafanya biashara hii ya kuuza mende , ambao anasema kwamba anawatoa mbali na maakazi yake hapo Kigamboni huko maeneo ya Morogoro.
Je mrembo huyu alianzaje wazo hili la kuuza mende ?
Ummy anasema kwamba kutokana na muonekano wake na hali ya kuwa msanii watu wengi wanamuona kuwa mtu wa ajabu sana kwa hali hii ya kufuga mende.
“Kwanini niliamua kufuga mende , ni kwasababu niliwahi kufuga kuku na pia bata lakini wakawa wana changamoto nyingi kwa mfano magonjwa ya kila siku , wakawa wananipa hasara sana nikaona kwamba mende hawana kazi nyingi na pia niliona kwamba kwa nchi yetu kuna baadhi ya watu wanawapenda kama kitoeo kwa hiyo nikachangamkia soko.
Hapa kwangu majirani wamenizoea na hawaoni shida kwangu kuwafuga mende au kuwala , kwasababu ni biashara yangu , mwanzo kabisa walishituka sana , hata kwa familia yangu walishangaa lakini sasa wameona ni kitu cha kawaida chenye kunipa mapato “anasema Ummy.
Mwanadada huyu anasema kwamba kumekuwa na faida kubwa ya biashara hii anayoifanya kando na kwamba anajiona kama mjasiriamali mwanamke ambaye anatafuta kujiendeleza kwa hali na mali na kwa hivyo anapopanga ratiba ya jinsi siku yake itakavyokuwa – hupangia pia mende wake watakula nini na wataishi vipi.
“Wanunuzi wangu ni wa aina tatu raia wa China , baadhi ya watanzania na pia wafugaji wa kuku , wakati mwengine kuku wanakula mende kwani wana protini nyingi kuliko dagaa , wanafunzi wanatumia mende kwa ajili ya mazoezi yao shuleni na kwa hiyo nina makundi mbalimbali ambayo ni wateja wangu wa mara kwa mara .Kwa hivyo hii biashara yangu ni kubwa sana”
Yote tisa kumi ni kuwa Ummy amejituma kama kijana wa kike kuhakikisha kwamba anaendeleza ndoto zake katika kutumia talanta zake , pamoja na kibiashara kwa kufanya mambo ambayo huenda yakaonekana kuwa ya ajabu ila yamekuwa na uwezo wa kumpa riziki yake.
Lakini wataalamu wanasema nini kuhusu matumizi ya mende na wadudu wengine ?
Kulingana na jarida la Wikipedia sekta ya dawa huko Asia na kampuni za vipodozi ndio wanunuzi wakuu wa wadudu. Mende ni chanzo cha bei nafuu cha protini, na, kama wadudu wengine, wanapendekezwa kama mbadala wa nyama.
Makampuni ya vipodozi yanathamini ubora unaofanana na selulosi wa mbawa za mende. Wakulima wa mende wanaeleza wadudu hao kuwa “rahisi kufuga na wenye faida”.
Nalo jarida la thehansindia linasema kwamba imethibitishwa kisayansi sasa kwamba mende wanaweza kuliwa na wana afya nzuri na wana kiwango kikubwa cha protini. Lakini lazima apikwe vizuri ili kuua bakteria wake waliopo kwenye mwili wake. Pengine katika jamii za magharibi hili bado ni swala geni.
Lakini katika tamaduni nyingi, hasa watu wa bara la Asia wanawashirikisha katika milo yao pamoja na wadudu wengine sehemu nyingine ni Huko Thailand wanaona Mende kuwa chakula kitamu haswa ikiwa imekaangwa sana kwenye mafuta ili kupata umbile na ladha hiyo iliyochanika, Katika nchi mbali mbali za Asia na hata barani afrika aina fulani ya wadudu huuzwa katika masoko kama chakula cha kawaida .