Mfanyakazi daraja la Magufuli afariki akiogelea ziwani



Mwanza. Mfanyakazi wa kampuni ya CCECC inayojenga daraja la Magufuli (Kigongo-Busisi) mkoani Mwanza, Sula Mramba amefariki baada ya kuzama ziwani akiwa anaogelea.

Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo, Alphonce Laurian amesema mkasa huo umetokea wakati alipokuwa akielekea katika eneo lake la kazi kwa ajili ya kuendelea na shughuli ya uchomeleaji wa vyuma katika daraja hilo ndipo aliposikia sauti ya Sula akiomba msaada huku akionekana kuzama majini.

"Ilikuwa saa 6:55 ndio nimefika hapa nikakuta jamaa anaogelea sasa ile hali ya kuogelea mimi si najua jamaa anajua kuogelea vizuri na nilishawahi kuona anaogelea, kukaa kidogo nashangaa anasema nisaidie nikaamua nimrushia life jacket (jaketi ya usalama) ile kumrushia moja kwa moja akapotea," amesema Laurian.

Alphayo Mtaki ameiambia Mwananchi Digital kwamba Sula ambaye ni mzaliwa wa Butiama mkoani Mara anakadiliwa kuwa na miaka kati ya 30 hadi 32.


 
"Sula alikuwa ni rafiki yangu na mimi ndiyo nilimtafutia kazi hapa, alipopata kazi hapa alikuwa akifanya kazi katika kitengo cha uchomeleaji wa vyuma," amesema Mtaki.

Ofisa rasilimali watu msadizi wa kampuni ya CCECC, Witness Bamkunga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akisema ajali hiyo imetokea Sula akiwa nje ya majukumu yake ya kazi.

Naye askari wa zamu wa kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, Said Sekibojo amesema uchunguzi uliofanywa eneo la tukio umebaini eneo alilozama lina kina kirefu na maji yaliyobadilika rangi kutokana na shughuli za ujenzi zinazoendelea katika eneo hilo.


"Tulipofika eneo la tukio saa 8 mchana baada ya hapo tulitafuta taarifa ili kufahamu sababu ya yeye kuzama kisha tukatafuta watu wa kusaidia nao kuutafuta mwili wake, hatimae kwa kushirikiana na watu wa hapa Busisi tulifanikiwa kuupata mwili wake, eneo hili lina kina kirefu na huenda ndicho kimesababisha akazama," amesema Sekibojo

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad