MGEJA : Mabaki ya Genge la Ndugai Yajitathimini , Mabango Yake Yanatia Kichefuchefu




Mwanasiasa Mkongwe nchini Tanzania Khamis Mgeja akizungumza na waandishi wa habari mjini Shinyanga.

Mwanasiasa Mkongwe nchini Tanzania Khamis Mgeja amewapongeza Watanzania kuandika Historia ya pekee kumlinda Rais Samia Suluhu Hassan akibainisha kuwa nguvu ya umma ikiamua inaweza kukutoa hata kama utakuwa ni mbabe na mwenye jeuri huku akiyataka mabaki ya genge la Job Ndugai kujitathmini na kuchukua hatua.

Mgeja ambaye ni Kada wa Chama cha Mapinduzi na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mzalendo Foundation inayojihusisha na masuala ya haki, utawala bora na demokrasia amesema nchi iliingia katika mtafaruku mkubwa kuhusu kauli za aliyekuwa Spika wa Bunge Job Ndugai alipofikia hatua ya kueleza Tanzania kupigwa mnada na kutotambua jitihada kubwa zinazofanywa na Mhe. Rais katika kupata misaada ya kuja kusaidia nchi.


 
“Ndugai alibeza hali iliyosababisha wote tupate mashaka na hatukuamini hayo maneno yanaweza kutolewa na ndugu yetu Ndugai. Lakini inawezekana kuna tatizo la kiafya au ulevi wa madaraka lakini Waswahili wanasema ukilikoroga basi baadae unalinywa mwenyewe, kwa hiyo uamuzi huu aliochukua wa kujiuzulu ni uamuzi tuliotarajia wengi kwamba hana namna kwa sababu presha ya wananchi, nguvu za umma kila kona zilikuwa zikitaka kumshinikiza ajiuzulu, viongozi wenzake, wabunge wenzake, viongozi wa dini na wananchi kada mbalimbali”,ameeleza Mgeja.

“Kwa kweli Watanzania wamepata ushindi, ushindi ambao wametumia haki zao za kikatiba kama Watanzania, kama wenye nchi wamelinda taasisi ya Ikulu, wamemlinda Rais wao na wote tumempigania kuhakikisha kuwa yeyote yule hatutakii mema basi Watanzania watakufa naye, watakula sahani moja nae”,amesema Mgeja.

“Nchi ya Tanzania tumeandika historia, historia inaandikwa kwamba nguvu ya umma ikiamua inaweza kukutoa hata kama utakuwa ni mbabe, utakuwa na jeuri utakuwa vyovyote vile. Nguvu hii ya umma iwafanye viongozi wawe makini wanapopewa dhamana wazitumie nafasi zao vizuri Watanzania wasisahau kuwa watanzania ndiyo wanaowapa dhamana hao viongozi”,amesema.


Mgeja ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga amesema Job Ndugai hakuidharau tu Ikulu, hakumdharau tu na kumkejeli Rais Samia Suluhu Hassan bali aliwadharau Watanzania wote kwani unapomgusa Rais umewagusa Watanzania na Watanzania hawatapenda hata kuona hilo bango la Job Ndugai lililopo katika Soko Kuu la Dodoma akishauri bango lake liondolewe.

“Kwa makosa hayo aliyoyafanya Ndugai kwa kweli hata kama kutakuwa na kumbukumbu zake zilizoandikwa ziondolewe. nchi zingine hata mabango, sanamu za viongozi wanaofanya mambo ya hovyo huwa zinaharibiwa na wananchi lakini kwa sababu sisi ni wastaarabu mimi nashauri hata lile Soko la Dodoma lililopewa jina la Ndugai niiombe serikali lile bango liondolewe kwa sababu litaleta kichefu chefu kikubwa kwa sababu Ndugai alidhalilisha nchi, aliwadhalilisha Watanzania”,ameongeza

Mgeja amewataka walio nyuma ya Job Ndugi wajitathmini haraka na wao wachukue hatua kama alivyofanya Nahodha wao Job Ndugai ya kujiuzulu na wajiuzulu ili kazi ziendelee nchini.

“Katika Mtafaruku huu bado mabaki ya Ndugai yapo,watu wake na genge lao lipo. Genge hili tulilisema huko nyuma tulipozungumza kumuonya Polepole na Genge lake. Sasa dalili hii iliyojitokeza wasisubiri tena wananchi waanze kuwanyoshea vidole, walinde heshima zao, wachukue hatua. Hilo genge wapo waliokuwa wakijipambanua kwa kuzungumza lakini wapo wa kimya kimya ambao hawakupenda kujionesha”,amesema Mgeja.


 
“Nakumbuka huko nyuma sisi kama wazee wa Shinyanga tulikemea sana tabia ya Humphrey Polepole na wenzake na tukazungumza nyuma ya pazia kuna jambo, na wala siyo Polepole peke yake, kulikwa kuna genge. Sasa hili genge ambalo tayari nahodha wake ndugu Job Ndugai alishajipambanua, wale waliobaki wajitathmini na wao, wasisubiri kunyooshewa vidole na waitathmini sana”,ameeleza Mgeja.

“Ile hotuba ya Mhe. Rais aliyozungumza hivi karibuni, Wajitathimini na wananchi wanawajua mmoja mmoja, wote tunajua siyo Polepole peke yake, akina Bashiru siyo peke yao, kuna kundi ambalo lilitaka kufanya kama yaliyotokea kule Malawi kwa aliyekuwa Rais Joyce Banda”,amesema

“Nimpongeze sana Mhe. Rais Samia juzi alipozungumza kuwa chokochoko hizi ni za mwaka 2025, nafikiri jipu hilo amelipasua na kweli kilichokuwa kikituyumbisha hapa ni 2025, kwa hiyo sasa tuombe Watanzania tuchape kazi,tumuunge mkono Mhe. Rais tujiletee maendeleo sisi wenyewe na tumpongeze mhe. Rais katika kipindi hiki cha chokokocho ameendelea kuwa imara na wala hakutetereka na taifa analipeleka vizuri sana kwa hiyo tuendelee sisi kama Watanzania kumuunga mkono”,amesema Mgeja.

“Wapo watu walikuwa wakijitokeza wengine kumuomba radhi Ndugai,kwa kweli hakukuwa na namna, alikuwa hasameheki kwa kosa la kulinajisi taifa, kwa kweli makosa hayo hayakuwa na msamaha,alitakiwa kuweka utulivu katika nchi ili kazi ziendelee.

Sisi kama wazee, wanasiasa wakongwe katika nchi hii tunasema hatua zaidi baada ya Ndugai na genge lake na hata wale waliozungumzwa kuwa na shati za kijani na wenyewe tunawajua wachukue hatua wasisubiri kuchukuliwa hatua”,amesema Mgeja.

“Nasikitika, hivi hii nchi wazee wako wapi?mpaka mtafaruku mkubwa unatokea hakuna wazee wanaoweza kusimama kuyakemea masuala haya na kuwashauri hawa, kwa sababu nchi ikikosa wazee tutayumba sana,tukikaa kwa kutegeana tutayumba sana.niwaombe wazee tubadilike huu mtikisiko uliotokea wazee wamekaa kimya na watu mbalimbali wamekaa kimya”,ameeleza.

“Wameanza akina Polepole, wamezanza akina Bashiru wanazungumza chini kwa chini lakini watu wakafika mahala wakajitokeza wakazungumza kwa kweli lazima iwepo timu ya wazee kama taifa tunapoona watu au viongozi wanakengeuka basi haraka lile baraza la wazee linachukua hatua kumshauri au kukemea au kutuelekeza.

Yaliyopita si ndwere na sasa tugange yajayo na watu wanaopaswa kujitathmini, lile genge lililobaki lenye mitazamo ya 2025 basi wajitathmini kama alivyosema Mhe. Rais kwamba wapishe waende na harakati zao wamuache Rais afanye kazi za kuwatumikia Watanzania na wote tumesema tunamuunga mkono Mama kwa nguvu zetu zote”,amesema Mgeja.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad