Miezi Miwili Kamili Toka Aje Nchini Hizi Hapa Panda Shuka za Pablo Ndani ya Simba...Afunguka Haya



LEO imetimia miezi miwili kamili tangu Kocha Mkuu Pablo Franco ajiunge na Simba akitokea Al Quadsia ya Kuwait ndani ya muda mfupi amefanya mambo matatu makubwa.
Jambo la kwanza ambalo Mhispania huyo amelifanya ndani ya Simba ni kuongeza maradufu makali ya ushambuliaji ambayo mwanzoni mwa msimu ilipotea.

Katika mechi nane za mashindano ambazo ameiongoza ndani ya muda huo, timu hiyo imekuwa tishio katika kufumania nyavu tofauti na ilivyokuwa katika mechi nane kabla yake. Jumla ya mabao 16 yamefungwa na Simba ikiwa ni wastani wa mawili kwa kila mchezo wakati kabla yake ilifunga sita katika mechi nane ambayo ni wastani wa bao 0.75 kwa mechi.

Ndani ya kipindi hicho ni mechi tatu ambazo Simba ilifunga idadi ya mabao chini ya mawili- dhidi ya Yanga iliyomalizika kwa sare tasa na wa ugenini Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Red Arrows ya Zambia walikopoteza kwa bao 1-0 na mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam waliopata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania.

Kabla ya ujio wa Franco, Simba ilipata ushindi wa kuanzia mabao mawili mara moja tu katika mechi ya ugenini ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy ambako ilishinda 2-0, huku wakifunga bao mojamoja katika michezo minne na mechi tatu walimaliza bila kufunga.

Jambo la pili ambalo amelifanya ni kuipa makali timu hiyo katika kipindi cha kwanza tofauti na hapo awali.

Takwimu za idadi kubwa ya mabao ambayo Simba imefunga na kufungwa katika kipindi cha kwanza ni uthibitisho tosha wa jinsi kocha huyo alivyoanza kuijenga iwe na uwezo wa kumaliza mechi mapema.

Kati ya mabao 16 iliyofunga, tisa yamepatikana kipindi cha kwanza huku saba yakipachikwa kipindi cha pili, ilhali katika mabao ya kufungwa mawili tu yamefungwa kipindi cha kwanza na manne kipindi cha pili.

Ukiondoa hayo, kocha huyo ameonekana kutoa nafasi ya kucheza kwa idadi kubwa ya wachezaji ndani ya mechi nane lakini pia amewapa uhuru mkubwa wa kushambulia jambo lililoifanya Simba ipate mabao kutokea maeneo tofauti uwanjani.

Tofauti na awali ambapo mabao ya Simba yalionekana kutoka kwa wachezaji wa nafasi za mbele zaidi, chini ya Pablo, Simba imekuwa ikipata mabao hadi kwa wachezaji wa kiungo na ulinzi. Kabla ya ujio wa Pablo ni wachezaji wanne ndio walikuwa wamefungia mabao ambao ni John Bocco, Rally Bwalya, Medie Kagere na Lwanga Taddeo wakati chini yake wachezaji tisa tofauti wameifungia Simba ambao ni Bernard Morrison, Mohamed Hussein, Joash Onyango, Kibu Denis, Peter Banda, Sadio Kanoute, Hassan Dilunga, Mzamiru Yassin na Pape Osmane Sakho.

Hata hivyo, soka la kushambulia ambalo Pablo amekuwa akilipendelea, limeonekana kuiathiri Simba kwenye ulinzi tofauti na watangulizi wake ambapo timu hiyo chini yake imeruhusu idadi kubwa ya mabao tofauti na alivyoikuta.

Simba imeruhusu mabao sita ikiwa chini ya Pablo wakati katika mechi nane kabla yake, iliruhusu nyavu zake kutikiswa mara tatu tu.

Akizungumzia maendeleo ya Simba chini yake, kocha huyo alisema kwa kiasi kikubwa yanachangiwa na utayari wa wachezaji wake.

“Simba ina wachezaji wazuri ambao kila mmoja amekuwa na kiu ya kutaka kufanya vyema na kuisaidia klabu. Hili ni jambo kubwa kwa timu.

“Malengo yetu ni kufanya vizuri katika ligi na mashindano ya kimataifa na kila mmoja anayafahamu hivyo naamini kama wachezaji wakiendelea kujituma yata-timia,” alisema Pablo
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad