Morogoro. Miji mitano mikubwa nchini inatarajia kuanzishwa usafiri wa umma wa ‘mwendokasi’ baada ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuwakutananisha wadau mbalimbali kuandaa na kuwasilisha mapendekezo ya kutunga sheria ya usafiri wa umma mijini lengo likiwa ni kuweka mfumo rasmi wa kuboresha usafiri wa umma.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha kupokea maoni kutoka kwa wadau juu ya mapendekezo ya utunzi wa sheria ya kuboresha mfumo wa usafiri wa umma mijini Morogoro, Mkurugenzi msaidizi idara ya sheria Tamisemi, Eustard Ngatale amesema wadau wa kikao hicho wana wajibu wa kutoa mapendekezo ili kupata maoni ya upatikanaji wa sheria itakayokidhi mahitaji yanayorajiwa.
"Ripoti ya utafiti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2013 inaeleza kupata suluhisho la kuboresha usafiri wa umma mijini na kubainisha kuwa nusu ya watu katika dunia wanaishi mijini na tunaona Serikali ina wajibika kuboresha mfumo wa usafiri wa umma mijini kutokana na mikoa ya nchi yetu kuendelea kupanuka siku hadi siku." amesema Ngatale.
Akiwashilisha mada ya andiko la mapendekezo ya kutunga sheria hiyo, Kaimu mkurugenzi wa idara ya uendeshaji na usimamizi wa miundombinu kutoka Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Mhandisi Ahmed Wamala amesema mpango wa kupitishwa kwa sheria hiyo itatoa nafasi kwa miji kuanzishwa kwa usafiri wa umma kwa majiji yaliyopo na yaendelea kukua.
Majiji hayo ni Arusha, Mwanza, Mbeya, Dodoma na Tanga kutokana na miji hiyo kuwa na uhitaji wa usafiri wa umma ukiondoa jiji la Dar es Salaam ambalo tayari ina usafiri.
Usafiri huo ni mabasi yaendayo haraka, treni, feri kwa Bahari ya Hindi, cable car maeneo yenye milima ikiratibu usafiri huo na chombo kitakachoundwa kuendana na jografia ya miji husika.
Meneja wa kitengo cha sheria kutoka wakala wa mabasi yaendayo haraka (DART), Mwanasheria Domina Madeli amesema andiko hilo linalenga kuchambua na kuweka hoja ya kuboresha usafiri wa umma mijini kuanzisha sheria itayotungwa na Bunge.
Kwa mujibu wa hesabu ya magari ililofanyika kati ya mwaka 2005 na mwaka 2011 ongezeko kubwa la vyombo vya usafiri linatokea katika barabara kuu ambapo hali hiyo kwa kiasi kikubwa inachangiwa na usafirishaji wa mizigo kwenda nje ya nchi kutokea katika bandari nchini.