Mwanamke mmoja amehukumiwa miaka 20 jela na baadaye kunyongwa hadi kufa na mahakama nchini Pakistani baada ya kukutwa na hatia ya kutuma jumbe za kufuru katika mitandao yake ya kijamii ya WhatsApp na Facebook.
Mwanamke huyo aliyejulikana kwa jina la Aneeqa Atteeq, 26, alipatikana na hatia na kuhukumiwa katika mji wa Rawalpindi, siku ya Jumatano baada ya kusikilizwa kwa mashitaka dhidi yake chini ya sheria ya makosa ya kimtandao na kufuru ya Pakistani.
Taarifa ya gazeti la Guardian, inasema Aneeqa alikutana mtandaoni na aliyemtuhumu ambaye pia ni mpakistani mwanaume, mwaka 2019 katika programu ya michezo ya kwenye simu ambapo waliendelea kuwasiliana katika mtandao wa kijamii wa WhatsApp.
Mshtaki huyo alisema kuwa Aneeqa alituma vikaragosi vya mitume na akatoa maoni kuhusu watakatifu katika mitandao yake ya WhatsApp na facebook akiendelea kusambaza kufuru hizo kwa watu wengi.
Hati ya mashitaka ya mahakama inasema “kwa makusudi alidhamiria kuwadhalilisha watukufu na kudhalilisha imani ya waislamu.”
Ateeq, ambaye ni muislamu mwenye imani kali, amekana mashitaka hayo, akiiambia mahakama kuwa mwanamue huyo alimvuta katika majadiliano ya kidini kwa makusudi ili apate ushahidi wa kumshtaki kama njia ya kulipiza kisasi baada ya kukataa kuingia kwenye urafiki naye.
Mwanasheria wa Aneeqa, Syeda Rashida Zainab, alisema kuwa hawezi kuzungumzia hukumu hiyo kwa sasa kwa kuwa mjadala huo ni nyeti. Hata hivyo hukumu hiyo ya kifo inatakiwa kuhakikiwa na makama kuu ya Lahore na anaruhusiwa kukata rufaa.
Katika jamii ya kipakistani kesi hizo za kukufuru dini huamsha hisia za makundi na hukumu yake ni kifo kwa yoyote anayekutwa na hatia ingawa mara nyingi hukumu hizo hupunguzwa hadi kuwa vifungo vya maisha.
Kulingana na sheria za haki za binadamu, kesi za kufuru huchukuliwa kama aina ya malipizi ambayo mtu binafsi huamua kumshitaki mwingine kwa ajili ya kufanikisha jambo.
Serikali ya Pakistani imekuwa katika mpango wa kubadili sheria zake zinazohusu kufuru lakini mpango huo unarudishwa nyuma na Waislamu wenye itikadi kali pamoja na Waziri mkuu wake Imran Khan.