SIKU moja baada ya kuenea taarifa ya kuuawa kwa mfanyabiashara wa madini, Musa Hamis, anayedaiwa kuuawa na askari wa Jeshi la Polisi, Mkoa wa Mtwara, mmoja wa ndugu wa marehemu amedai wakati akifuatilia suala hilo alitakiwa akae kimya au angepewa kesi ya ugaidi.
mjomba wa marehemu, Salum Ng’ombo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mkoani hapa, mjomba wa marehemu, Salum Ng’ombo, alidai Januari 5, mwaka huu, alimsindikiza mwanawe Kituo cha Polisi Wilaya ya Mtwara baada ya kuelezwa akachukue vifaa vyake.
Hata hivyo, alidai alimtahadharisha wafuatane wasije wakampa fedha bandia na kumfungulia kesi nyingine.
Alidai walipofika kituoni walikutana na askari aliyejitambulisha kwa jina la Grayson, na kumueleza kuwa anamkabidhi mwanawe na kumuomba ahakikishe anarudishiwa vifaa vyake ikiwa ni pamoja na fedha alizokuwa akidai.
“Gryason ninamfahamu alipokuja nikamkabidhi mwanangu akiwa na barua ya mwanasheria baada ya kuona hiyo barua aliwasiliana na mwenziwe na kumwambia kuna barua kutoka kwa mwanasheria wa serikali inataka kijana arudishiwe mali zake,” alidai Ng’ombo.
Alisema baada ya muda kijana wake alifikishwa katika chumba cha mahojiano na alikaa kwa zaidi ya saa mbili hali iliyompa wasiwasi na kuamua kwenda kuangalia kinachoendelea.
Alisema alipofika kwenye chumba hicho alimkuta mjomba wake akiwa amekalishwa chini hali iliyomfanya ahoji kinachoendelea wakati aliitwa kwa ajili ya kuchukua mali yake.
Vile vile, alidai siku hiyo hiyo saa nane mchana alirudi kituoni na kuomba ampatie chakula ndugu yake, lakini hakufanikiwa na badala yake akaambiwa na mkuu wa upelezi wilaya kuwa aondoke eneo hilo vinginevyo atapewa kesi ya ugaidi.
Ng’ombo alidai siku ya pili alipata taarifa kuwa kuna mtu ameuawa na hakutilia maanani kama ni mjombake, hadi Januari 7, alipoenda kwa Mkuu wa Upelezi mkoa kwa ajili ya kufungua faili la kumtafuta nduguye pamoja na mali zake.
Alisema akiwa kwa RCO, wakati anatoa maelezo na mama wa marehemu, wakaelezwa kuwa suala hilo limehusisha mpaka ofisi ya mwanasheria wa mkoa kwa na kwamba kutakuwa na tatizo na kuombwa wavute subira lifuatiliwe.
Mama Musa
Mama wa Musa, Hawa Bakari, akizungumza nyumbani kwa ndugu zake, alisema kama sheria ingefuatwa kwa wakati mwanawe asingefia mikononi mwa polisi.
Alisema kwa mara ya kwanza polisi walipofika katika kijiji cha Luponda, Wilaya ya Nachingwea, walitaka waonyeshwe fedha zilipowekwa na kijana wake aliposita kuwaonyesha walimuelekezea bunduki.
Aliomba serikali isaidie haki kutendeka ikiwa ni pamoja na fedha za mtoto wake kurejeshwa.
IGP Sirro
Juzi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Mark Njera, akihojiwa na chombo kimoja cha habari aliahidi kulitolea ufafanuzi jana, hata hivyo ha kueleza chochote baada ya kuwa katika vikao na viongozi wa ngazi ya juu wa jeshi hilo wakiongozwa na IGP.
Kwa upande wake IGP Simon Sirro, alipoombwa na waandishi wa habari azungumzie tukio hilo, alieleza kuwa yupo na Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni na kwamba jambo lolote kwa wakati huo atalitolea ufafanuzi waziri huyo.