Dodoma. Diwani wa Kata ya Kiomboi, Omary Hassan na Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kinambeu, Godfrey Yohana wasimulia mkasa wa mwalimu kuuawa kwa kuchomwa moto kwa mafuta ya petroli.
Ni kisa kilichotokea mkoani Singida kwa mwalimu Simon Roman (33) kufa kutokana na madai ya kuchomwa moto na mkewe Mwanaisha Shamir (29).
Roman alikuwa ni mwalimu katika Shule ya Sekondari Kinambeu na wakati umauti unamkuta, alikuwa amerudi likizo baada ya kufungwa chuo. Roman anachukua shahada ya pili ya elimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Tukio hilo lilitokea Desemba 27, 2021 jioni baada ya Roman kurudi kutoka matembezini na ilidaiwa mke alitaka kujua kuhusu uhusiano wa mumewe na mmoja wa wanawake katika eneo hilo ambaye alikuwa akimtilia shaka.
Diwani afunguka
Diwani wa Kata ya Kiomboi, Omary Hassan alikiri kuwapo kwa tukio hilo na hawakutegemea kamalingetokea.
“Huyo mwalimu (Roman) nilikuwa namfahamu tangu siku nyingi, alikuwa anaishi New Kiomboi katika kitongoji cha Lulumba, lakini kituo chake cha kazi ni Sekondari ya Kinambeu, ndugu yangu hata uso wake haukutamanika jinsi alivyounguzwa yule mwanaume mwenzetu, hakika amekufa kifo kibaya sana,” alisema Hassan.
Diwani huyo alidai mkasa mzima ulikuwa ni ugomvi wa siku nyingi kwani wawili hao walikuwa na malumbano ya kutuhumiana kwa kutoaminiana, hivyo ndoa yao ikawa na migogoro mingi katika kipindi kirefu wakitaka kuachana.
Hassan alidai siku ya tukio wawili hao waligombana na kurushiana maneno, lakini baadaye mume (marehemu) alipitiwa na usingizi ndipo mwanamke akachukua mafuta yaliyochemka akaenda kumwagia usoni mumewe na kufanya aungue vibaya ngozi ya uso na macho yakatoka nje.
Alidai mara baada ya tukio hilo, mdogo wa marehemu Apolinary Roman, aliyekuwa akiishi hapo wakati akisubiri matokeo ya kidato cha nne, alipiga kelele za nguvu kuomba msaada, lakini milango haikufunguka ndipo majirani walibomoa ukuta na kuwanusuru baadhi ya watu waliokuwamo ndani.
Hata hivyo, kijana huyo naye ameunguzwa vibaya usoni na hali yake ilitajwa na Polisi kuwa siyo nzuri wakati watoto wawili Clara Anthony na Wisley Anthony hali zao zilikuwa na afadhali.
Marehemu alikuwa masomoni
Mkuu wa Shule ya Kinambeu, Godfrey Yohana alisema Roman alikuwa masomoni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alikuwa anachukua shahada ya pili ya elimu na hakujua kama alikuwa amerudi likizo hadi aliposikia tukio la msiba.
Akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili alisema Roman hakuwa na muda mrefu katika kituo hicho cha kazi, kwani alianza kufundisha hapo mwaka 2019 na mwaka jana akapata nafasi ya kusoma kwa ajili ya kuongeza maarifa.
“Katika utendaji kazi wake hakuwa na tatizo lolote kazini wala walimu wenzake, nilimuona mchapakazi aliyestahili katika nafasi yake. Kwa mambo ya kifamilia mimi sikujua kama alikuwa na ugomvi na mkewe huyo, labda kwa majirani zao mnaweza kupata habari kamili,” alisema Yohana.
Alisema tayari mwili wa mwenzao ulishapumzishwa katika nyumba yake ya milele huko Kibondo mkoani Kigoma ambako watumishi wenzake walishiriki kumsindikiza katika safari yake ya mwisho na hivyo wamefunga ukurasa wake na kutaka habari zingine waulizwe polisi.
Mmoja walimu waliosindikIza mwili huo, aliliambia Mwananchi kwa sharti la kutotajwa jina kuwa mwili wa mtumishi mwenzao huyo haukuwa ukitambulika hasa usoni kutokana na majeraha ya moto.
Mwalimu huyo alisema ilikuwa vigumu hata kuruhusu watu badala yake walitakiwa kuangalia picha kwani hata kama wangeangalia wasingeweza kumtambua kwa namna yoyote.
Taarifa za awali
Taarifa iliyotolewa awali na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Stella Mutabihirwa ilidai kifo cha Roman kilitokana na kumwagiwa maji ya moto na mkewe Mwanaisha Shamir kisha akamwagia mafuta ya petroli na kuwasha moto.
Kamanda Mutabihirwa alisema chanzo cha ugomvi kilikuwa ni wivu wa mapenzi baada ya mwanamke huyo kudai kuwa mumewe huyo alikuwa na uhusiano na mke mwingine nje ya ndoa yao jambo lililozua majibishano.
Polisi wanamshikilia
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Kamanda wa Polisi mkoa Singida, Stella Mutabihirwa alisema polisi bado inamshikilia mwanamke huyo na yupo kwenye ulinzi mkali wakati akiendelea na matibabu kabla ya kumpeleka mahakamani.
Kuhusu athari zilizotokana na moto huo, alisema uliunguza vitu vingi ambavyo thamani yake imekuwa ngumu kuipata mara moja, lakini hasara yake ni kubwa kwa miili ya binadamu na mali zilizokuwa ndani ya nyumba iliyoteketea kwa sehemu kubwa.
Kamanda alisema Roman alipoteza maisha wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Mkoa wa Singida ambako alifikishwa akiwa na hali mbaya ya majeraha makubwa yaliyotokana na moto huo.