KIUNGO wa Simba, Jonas Mkude ametangazwa mchezaji bora wa Desemba wa timu hiyo na kuzawadiwa kitita cha Sh. milioni mbili kutoka kwa wadhamini wa klabu hiyo, Emirate Aluminium ACP.
Mkude ameibuka mshindi baada ya kuwabwaga mabeki wawili wa kati wa timu hiyo, Joash Onyanga na Henock Inonga 'Varane' waliokuwa wakiwania tuzo hiyo kwa Desemba.
Mbali ya Desemba kuonyesha kiwango cha juu, pia Mkude amecheza mechi nne kati ya tano na kuhusika katika mabao mawili kwa kutoa pasi za mwisho.
Katika kura zilizopigwa na mashabiki wa klabu hiyo, Mkude amepata kura 2,397 sawa na asilimia 43.93 ya kura zote huku Onyango akipata kura 2,393 (43.85%) na Inonga akiambulia kura 667 sawa na asilimia 12.22.
Tangu kuumia kwa Taddeo Lwanga, Mkude ndiye anayetawala kiungo cha ulinzi cha Simba akisaidiana na Sadio Kanoute, kwa pamoja wakionyesha uwezo mkubwa wakuwalinda mabeki wa timu hiyo.
Uwezo wao umechangia kwa kiasi kikubwa Simba kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 24, tano nyuma ya Yanga iliyopo kileleni lakini ikiwa mchezo mmoja mbele.