Mkuu wa Kanisa la KKKT Askofu Dk Shoo Ataja Spika Anayehitajika



Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk Fredrick Shoo
Mwanza/Bariadi. Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk Fredrick Shoo amezungumzia mchakato wa uchaguzi wa Spika wa Bunge unaoendelea hivi sasa hapa nchini, huku akitaja sifa tano za mtu anayestahili kuongoza mhimili huo wa dola.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu mjini Bariadi jana, Dk Shoo alisema Spika wa Bunge lazima awe mtu jasiri mwenye uwezo wa kusimamia, kulinda, kuheshimu na kufuata kanuni bila hofu wale upendeleo.

“Spika wa Bunge lazima awe mtu anayeweza kulinda heshima ya Bunge katika mijadala, maamuzi na kazi ya kuisimamia na kuishauri Serikali bila kuingiliwa na mihimili mingine ya dola. Awe mtu anayeamini katika mihimili kuheshimiana na kushirikiana bila kuingiliana,” alisema Dk Shoo.

Alisema Bunge ni mhimili muhimu kwa Taifa kama ilivyo mhimili wa Mahakama na Serikali (Utawala), hivyo wanaofanya uteuzi na kupiga kura wanapaswa kuhakikisha nafasi hiyo inashikiliwa na mtu ambaye siyo tu ana uwezo wa kuongoza mhimili huo, bali pia kulinda heshima ya Bunge katika kuisimamia na kuishauri Serikali.


“Tunamtaka Spika atakayelinda heshima ya Bunge kama mhimili unaojitegemea kwa kusimamia mijadala na maamuzi kwa haki,” alisema Dk Shoo.

Kiongozi huyo wa kiroho alitaja sifa nyingine ya mtu anayeshika nafasi hiyo kuwa ni uadilifu na weledi katika nyanja zote, uchaji Mungu, unyekevu na kujishusha.

Alisema nafasi ya Spika inatakiwa kushikwa na mtu asiyetumia vibaya madaraka kwa faida yake binafsi, chama chake wala makundi mengine ya kimaslahi.


Alitaja sifa nyingine ya Spika wa Bunge kuwa ni lazima awe mtenda haki kwa wabunge wote ndani na nje ya Bunge bila kujali itikadi za vyama vyao.

Mahalu afunguka

Akizungumzia sifa za mtu anayestahili kushika nafasi ya Spika wa Bunge, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (Saut), Profesa Costa Mahalu alisema ni lazima awe mtu asiyemezwa na ushabiki wa kisiasa wala makundi ya kijamii.

“Japo ushabiki wa vyama unakuwepo bungeni; lakini spika lazima awe mtu mwenye kusimamia na kufuata kanuni za Bunge. Lazima awe mtu anayeamini na kusimamia neutrality (kutoegemea upande) katika uongozi wake kuanzia kwenye mijadala na maamuzi ya Bunge,” alisema Profesa Mahalu.

Mwanazuoni nguli huyo wa sheria aliyewahi kongoza Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alitaja sifa nyingine ya spika kuwa ni mtu mwenye uwezo wa kuwaunganisha wabunge wote kutoka vyama vyote bila kujali tofauti zao za kiitikadi.


“Bunge lazima lionekane ni moja katika masuala na hoja za msingi zenye maslahi ya Taifa; kiti cha Spika ndicho chenye jukumu na wajibu wa kulifanya Bunge na wabunge wote kuwa wamoja,” alisema Profesa Mahalu, Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Italia.

Profesa Mahalu, aliyewahi kujitosa kwenye kinyang’anyiro cha uspika mwaka 2015 kabla ya kujitoa, aliwasihi Watanzania wote wanaoamini wanaweza kuongoza mhimili wa Bunge kujitokeza kuwania nafasi hiyo, inayoweza kugombewa na mtu yeyote mwenye sifa za kugombea ubunge kutoka ndani au nje ya Bunge.

Mchakato kwa vyama vingine

Akizungumzia mchakato wa kumpata Spika mpya wa Bunge baada ya Job Ndugai kujiuzulu Januari 6, Askofu Shoo alivishauri vyama vingine vya siasa kufungua milango ya mchakato huo kuwezesha wanachama wao kujitokeza ili watambulike na kupimwa na umma wa Watanzania.

“Uspika ni nafasi ya wazi kwa Watanzania wote kutoka vyama vyote vya siasa; navisihi vyama vingine navyo vifungue pazia kwa kuwaruhusu wanachama wao kujitokeza kuwania nafasi hiyo,” alisema Askofu Shoo.

Utitiri wa wagombea CCM

“Ni jambo jema kuona wana CCM wamejitokeza kwa wingi kuchukua fomu kuomba ridhaa ya chama chao kuwania uspika. Nawasihi wote wanaotamani kushika wadhifa huo kujitathmini, kujipima na kujitafakari kama wanaweza kuongoza Bunge,” alisema Askofu Shoo.

Hadi kufikia jana, makada 70 wa CCM walikuwa wamejitokeza kuchukua fomu kuomba kuteuliwa kuwania nafasi hiyo, huku chama hicho tawala kikivuna zaidi ya Sh70 milioni kutokana na ada ya Sh1 milioni kwa kila aliyechukua fomu hiyo.

Askofu Shoo alivishauri vyama vyote vya siasa kutumia vikao na michakato yake kwa mujibu wa katiba zao kuwatathmini, kuwapima na kuwachuja wanaojitokeza kabla ya kumteua mwenye sifa na uwezo wa kuongoza na kusimamia Bunge kwa faida na maslahi ya Taifa.

Hata hivyo, mbunge wa zamani wa jimbo la Rombo, Joseph Selasini (Chadema) ambaye kwa sasa ni kada wa NCCR Mageuzi, akizungumzia idadi kubwa ya waliochukua fomu kuwania nafasi hiyo, alishangazwa na kuhoji kama CCM haina kanuni zinazoeleza sifa za mgombea wa nafasi hiyo.

“Najiuliza CCM haina kanuni zinazoeleza sifa za mgombea kama ilivyo kwenye Katiba, sheria za uchaguzi na Bunge ili kila mtu ajipime kabla ya kuchukua fomu. Chama hakiwezi kuacha ‘open cheque’ (wazi), watu wanadhani kiti cha spika ni chepesi, au Bunge ni dhaifu,” alisema Selasini.


Kwa upande wake, Spika wa Bunge mstaafu, Pius Msekwa alisema kujitokeza kwa makada wengi ni ishara ya kukomaa kwa demokrasia ndani ya chama.

“Mwaka 2005 zaidi ya wana CCM 40 walichukua fomu kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Urais; hivyo siyo ajabu leo kuona watu 50 wanaomba uteuzi kugombea nafasi ya Spika.

Hii ni afya kwa chama na ni ishara ya kukua na kukomaa kwa demokrasia nchini,” alisema Msekwa.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad