BAADA ya Spika Job Ndugai kumuomba radhi Rais Samia Suluhu Hassan na Watanzania, kufuatia madai ya deni la taifa, baadhi ya wachambuzi wa siasa wamezungumzia hatua hiyo wakimuunga mkono kwa kuwa muungwana, lakini wakakosoa mazoea ya baadhi ya viongozi kusema kuwa wananukuliwa vibaya.
Gwandumi Mwakatobe ni miongoni mwa wachambuzi hao, anayezungumza na Nipashe akisema kuomba msamaha ni uungwana na ni jambo jema na linaloonyesha mtu kukiri kosa, lakini akawa na mashaka na mtindo wa baadhi ya viongozi wanaoendeleza kusema jambo likisharushwa kwenye vyombo vya habari au mitandao, baadaye wanaibuka na kudai kwamba wamenukuliwa vibaya.
"Ninaamini kwamba, wana lengo la kufikisha ujumbe sehemu fulani na hata wakikana, tayari unakuwa umefika, lakini sidhani kama ni jambo jema, wanasababisha jamii isijue upande wa kusimamia," anasema.
Anakumbusha kuwa mtu au kiongozi anapotoka hadharani na kusema jambo huenda anakuwa na uhakika nalo, lakini baadaye anapoibuka na kudai kwamba vyombo vya habari vimemnukuu vibaya, anajishushia heshima kwani zama hizi teknolojia inakuwa ndiyo ushahidi hasa pale , ujumbe unaporekodiwa.
"Lakini pia kwenye suala la Ndugai, kuna jambo jingine nimeliona ambalo limenishangaza sana. Yaani watu walikuwa hawajadili hoja aliyoitoa, badala yake wanamshambulia yeye," anaeleza.
Anasema, Spika alikuwa ameibua hoja ya kufikirisha ambayo kulikuwa na haja ya kuijadili ili kama kuna njia mbadala ambayo serikali inaweza kuitumia kukopa, itumike, lakini kilichoendelea ni watu hawakuliona hilo na kuamua 'kumshambulia' kwa maneno makali.
Mkurugenzi Mtendaji mstaafu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba, anasema Spika Ndugai, nafasi yake kama mkuu wa mhimili mmojawapo wa dola kwa vile alijua alichosema na anayaamini, angesimamia usemi wake.
Alianza kwa kusema mitandao ya kijamii imemuwekea maneno, baadaye anaomba msamaha, hapa ni kwamba alikubali shinikizo, kwa mujibu wa uchambuzi wa Dk. Kijo-Bisimba na kwamba baada ya kutoa kauli hiyo, baadhi ya viongozi wa CCM katika mikoa walijitokeza na kumpinga wazi wazi, hali ambayo inaonyesha kuwa imemlazimisha kuomba msamaha kutokana na kupingwa.
"Mimi ninaamini kwamba, hatua hiyo ya kuomba msamaha inatokana na shinikizo kubwa kutoka ndani ya chama chake, ndipo akalazimika kuja hadharani kuomba radhi ," anasema na kumshauri kuwa wakati mwingine kama hana uhakika na jambo ni vyema kukaa kimya.
Aidha, anasema kiongozi anayeongoza mhimili mwingine mkubwa wa dola ambao ni bunge anapokuwa hana uhakika na jambo, ni vyema akawa kimya, kuliko kwenda katika vyombo vya habari kulisema, kisha anaibuka na kulikanusha na kwamba, anaichanganya jamii.
SULUHU KATIBA MPYA
Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Bob Wangwe, anasema, kilichotokea kimeonyesha wazi kuwa kuna haja ya kuwa na katiba mpya ili kupata viongozi ambao hawaegemei upande wowote au wasiofungamana na chama chochote.
"Ni muhimu kufanya mabidiliko ya kimfumo kupitia katiba mpya, ili kuwa na chombo imara kinachoweza kuishauri na kuisimamia serikali, inavyotakiwa bila kuyumba,"anasema Wangwe na kufafanua kuwa kuomba msamaha ni uungwana, lakini anaongeza kuwa kitendo cha Ndugai kutoa maoni na kisha akaomba msamaha, kinaonyesha upungufu wa kimfumo unaotokana na katiba iliyopo.
"Bunge na serikali ni mihimili miwili inayojitegemea, hakuna mmoja unaotakiwa kujiegemeza kwa mwingine. Nimepata fundisho kwamba huenda Spika ameona kuna hatari ya kupoteza nafasi yake lakini alitakiwa kile alichokisema kama kilikuwa na ukweli akisimamie ili kujitengenezea urathi (legacy) ," anasema Wangwe.
Juzi Spika alikaririwa na vyombo vya habari akimuomba radhi Rais na Watanzania kwa kauli yake iliyosambazwa katika mitandao ya kijamii ikimwonyesha kupinga mikopo inayokopwa na serikali ya awamu ya sita.
Aliomba radhi mbele ya waandishi wa habari jijini Dodoma,katika kipande cha video yake kilichosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na kuzua mjadala mkubwa kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwamo wanasiasa.
"Wakati tunaingia mwaka mpya mwezenu nilipata homa kali na hali ilikuwa ni mbaya sana, lakini katika kipindi hicho ndipo kulizuka mambo kwenye mitandao ya kijamii na mimi sikuwa na uwezo wa kuzungumza jambo lolote kuhusu ‘clip’ hiyo.
“Lakini leo nimeona niwaite ili niweze kutoa ufafanuzi kuhusu jambo hilo, Desemba 26, mwaka jana nilialikwa na kikundi kimoja cha Wagogo, lakini katika sehemu ya mazungumzo yangu niliongelea sana umuhimu wa kulipa kodi, ushuru na tozo mbalimbali nikihimiza tujitegemee na siyo kama ambavyo watu walivyokata sehemu ya hotuba yangu na kuiweka kwenye mitandao ya kijamii,” alikaririwa akisema Ndugai.
Akirejea mazungumzo yake katika mkutano huo, anasema alisisitiza suala la ulipaji wa kodi pamoja na tozo huku akitoa msisitizo wa tozo ya miamala ya simu iliyopitishwa na bunge lake.
"Lakini kama kuna sehemu nilihisiwa kuwa kuna jambo nimezungumza la kumvunja moyo Rais wetu naomba radhi sana, anisamehe nimekosa mimi, nimekosa mimi, nimekosa sana, Mungu anisamehe, Watanzania wanisamehe,”.
Anasema, kwake haiwezi kutokea na wala haitatokea kupinga mikopo ambayo imekopwa na Rais, ambayo imeiwezesha nchi kufanya mambo makubwa katika ujenzi wa madarasa nchi nzima.