Kamanda Polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Jumanne Murilo
JESHI la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam nchini Tanzania, linamshikilia Isaya Mzava (59), Mkazi wa Bunju Beach, Kinondoni kwa tuhuma za mauaji ya mke wake, Irene John Mzava (56), mfanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), yaliyofanyika tarehe 26 Desemba 2021. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa, tarehe 7 Januari 2022, Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Jumanne Muliro amesema, mtuhumiwa huyo baada ya kutekeleza mauaji hayo kwa kutumia kitu chenye nch kali alitoroka.
“Baada ya kufanya mauaji hayo mtuhumiwa alitoroka na kuelekea Mkoa Kilimanjaro kwa kutumia gari namba T 727 DKK aina ya Toyota Harrier ambapo alipobaini anafuatiliwa alilitelekeza gari hilo Moshi mjini na kulekea Mkoa wa Arusha.”
“Jeshi la Polisi liliendelea kumfuatilia ambapo alikimbilia Mkoa wa Shinyanga, wilaya Kahama mjini, ufuatiliaji wa kina ulipofanyika ilibanika alikimbia tena na kulekea Mkoa wa Kagera, Wilaya Muleba,” amesema.
Kamanda Muliro amesema, tarehe 4 Januari 2022, mtuhumiwa huyo alikamatwa katika kijiji cha Kagoma, wilaya ya Muleba, Mkoa wa Kagera na kurudishwa jijini Dar es salaam.
“Kilichofanywa na mtuhumiwa huyo ni cha kikatili ambacho hakivumiliki na ndio maana Jeshi la Polisi limefanya kila jitihada kuhakikisha mtuhumiwa huyo anakamatwa na hatimaye kufikishwa mahakamani haraka iwezekenavyo ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake,” amesema
Amesema, Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linatoa wito kwa wananchi wote kujiepusha kufanya matukio ya kihalifu kwa kufikiri wanaweza kukimbia na wasipatikane.
Kamanda huyo amesema, Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linasisitiza ukifanya tukio la kihalifu litakufuatilia mahali popote ulipo iwe ndani au nje ya Mkoa wa Dar es salaam, utakamatwa na kurejeshwa kwenye eneo alilofanya tukio kwa hatua zaidi za kisheria.