Newala. Mvuke mweupe unaotoka kwenye shimo maarufu kwa jina la Shimo la Mungu lililopo wilayani hapa Mkoa wa Mtwara, umewashtua wenyeji wa eneo hilo na kufanya matambiko wakiamini kuwa kuna jambo wamekosea.
Shimo hilo ambalo limekuwa likitumika kwa shughuli mbalimbali za kimila na kiimani limekuwa kivutio hasa wakati ambao mvuke mweupe hujitokeza na kufanya wenyeji wa eneo hilo kufanya matambiko wakiamini kuwa kuna jambo wamekosea ndio maana moshi hutokea.
Akizungumzia shimo hilo leo Januari 20, mbele ya Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi, Meja Generali Ibrahim Mhona na wanachuo wa chuo hicho, Ofisa Utamaduni wa Wilaya ya Newala Faraj Hamis alisema kuwa wanajitahidi kulitunza.
Akifafanua kuhusu shimo hilo lenye ukubwa wa ekari 40, Hamis amesema wakazi wa eneo hilo wamekuwa na imani kuwa eneo hilo linalindwa na mizimu iliyopo ndani na wanalitumia kama eneo la utalii na lina historia kubwa ya mji wa Newala.
Amesema wakazi hao wanaamini kuwa haiwezekani kuingia ndani ya shimo hilo bila kufanya tambiko na ukatoka salama na kwamba waganga wa jadi huingia eneo hilo kutafuta miti dawa.
“Ule mvuke mweupe unapotoka ndani na kutanda Newala yote kwa mila za zamani wanaamini kuwa kuna nyakati watu wanakuwa wamesahau Mungu kwahiyo tunakuwa tunakumbushwa hivyo hulazimika kufanya maombi,” amesema Hamis.
Kwa upande wake Issa Rajabu ambaye ni mkazi wa Newala amesema kuwa eneo hilo lilikuwa pori kubwa na haikuwezekana kuingia bila idhini ya wazee wanaotambika.
“Eneo hili lilikuwa hatarishi sana kwa kuwa kulikuwa na majoka makubwa sana kama unaingia kwa hoja inayodhuru ulikuwa unapambana nayo, lakini wale wazee walikuwa wanafanya maombi eneo hili halijachezewa ingawa mabadiliko ya tabia nchi yanaonekana kwakuwa msitu umepungua,” amesema Rajab.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC), Meja Generali Ibrahim Mhona amesema kuwa amefurahishwa na historia ya shimo hilo.
“Tupo shimo la mungu ukiona kitu kinahusianishwa na mungu ni kitu cha thamani kiutamaduni kiutalii na kiimani kinakuwa ni kitu cha thamani tungependa mtwara mfanye jitihada za kutangaza mahala hapa ili baadae pawe ni mahala pazuri pa utalii ili wengine waje kuabudu lakini wengine waje kupunga upepo na wengine waje kutalii,” amesema Mhona.