Mwana Mfalme wa Uingereza aliyeweka makaazi yake nchini Marekani amekata rufaa kwenye mahakama za Uingereza baada ya serikali ya Uingereza kukataa kumpa ulinzi wa polisi alioulipia kwa pesa yake binafsi.
Mwanamfalme Harry amedai uamuzi huo kunyimwa ulinzi wa polisi ya Uingereza unamaanisha hawezi kurudi nyumbani. Harry na mkewe Meghan walipoteza huduma ya kulindwa na polisi ya Uingereza kwa fedha za mlipa kodi wa Uingereza baada ya kujiondowa kwenye majukumu ya kifalme mnamo mwaka 2020 na kuhamia Marekani.
Nyaraka za kisheria zimeonesha kwamba Harry anasema kwamba Timu ya ulinzi ya Marekani haitokuwa na mamlaka ya kutosha kuilinda familia yake itakapokuwa nchini Uingereza.
Mwanamfalme huyo amekata rufaa kutaka suala hilo litathminiwe kisheria katika mahakama mjini London baada ya wizara ya mambo ya ndani ya Uingereza kumkatalia ombi lake la kutaka kujilipia mwenyewe ulinzi wa polisi ya Uingereza.