Ndugai mwingine ajiuzulu Ujerumani



MKUU wa jeshi la wanamaji nchini Ujerumani, Kay-Achim Schoenbach amejiuzulu, kufuatia matamshi yake yenye utata kuhusu mzozo wa Ukraine. Inaripoti mitandao ya kimataifa

Schoenbach ametangaza kujiuzulu Jumamosi usiku baada ya kunukuliwa akisema, Rais wa Urusi, Vladmir Putin anahitaji heshima na kwamba Rasi ya Crimea kamwe haitorejea kwa Ukraine.

Alitoa kauli hiyo, katika ziara yake nchini India, akieleza kuwa “anachohitaji sana ni heshima. Na kumpa mtu heshima ni gharama ndogo. Iwapo ingeulizwa, ni rahisi kumpa heshima anayoidai na pengine anastahili heshima hiyo.”

Matamshi ya Schönbach hayakuifurahisha Ukraine. Imeamua kupitia wizara ya mambo yake ya nje, kumuita balozi wa Ujerumani, Anka Feldhusen kuelezea kwamba haikubaliani na matamshi hayo.


 
Katika taarifa yake ya kujiuzulu, Schönbach alisema, amemuomba Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Christine Lambrecht, kumruhusu kuachana na majukumu yake mara moja na amethibitisha kuwa waziri huyo amelikubali ombi lake.

Matamshi hayo ameyatoa baada ya Urusi kuwapeleka wanajeshi 100,000 katika mpaka wake na Ukraine na kusababisha wiki kadhaa za mazungumzo ya kidiplomasia kuzuia kuzuka kwa uhasama.

Hata hivyo, Urusi imekanusha kuivamia Ukraine kijeshi, lakini imetaka kuhakikishiwa na Jumuia ya Kujihami ya NATO kuwa haitoingia kwenye ardhi ya Ukraine, wala haitoendelea kujitanua katika upande wa mashariki ya Ulaya.


Akizungumza katika Taasisi ya Mafunzo ya Ulinzi na Utafiti ya Manohar Parrikar, Schoenbach alisema anaiona China kuwa ndiyo kitisho kikubwa na kwamba Ujerumani na India kwa pamoja zinamuhitaji Urusi kwa lengo la kupambana na China.

Kuhusu mzozo kati ya Urusi na Ukraine, Schoenbach amesema, Rasi ya Crimea imetoweka na ukweli ni kwamba haiwezi kamwe kurejea Ukraine. Matamshi yake yanagusia hatua ya Urusi kuinyakua Rasi ya Crimea mwaka 2014, moja ya matukio yaliyoanzisha uhasama uliodumu kwa muda mrefu.

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Ujerumani amesema, wizara hiyo imejitenga na maoni ya Schoenbach na kwamba matamshi hayo hayafungamani na msimamo wa wizara.

Wizara hiyo imesema Schoenbach anapaswa kujieleza kwa mkuu wake, Inspekta Jenerali Eberhard Zorn na kwamba serikali ya muungano ya Ujerumani italijadili suala hilo siku ya Jumatatu.


 
Kwa upande wake, Schoenbach ameomba radhi kupitia ukurasa wake wa Twitter, akisema kuwa matamshi yake yalikuwa “kosa la wazi,” na hakuna haja ya kubishana.

Alisema, “matamshi yangu ya sera ya utetezi wakati wa kikao na taasisi ya India yaliakisi maoni yangu binafsi kwa wakatu huo,” aliandika Schoenbach na kuongeza, matamshi yake hayaakisi msimamo wa wizara ya ulinzi.

Ni kama alivyofanya aliyekuwa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, ambaye alitangaza kujiuzulu tarehe 6 Januari mwaka huu. Kujiuzulu kwa Ndugai, kulitokan ana matamshi yake kuhusu mikopo inayochukuliwa na serikali kutoka mashirika ya fedha ya kimataifa, ikiwamo Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la kimataifa (IMF), kwamba haina tija kwa taifa.

Alisema, mikopo hiyo ni mzigo kwa nchi na haina faida kwa watu wake. Akataka serikali kuwekeza kwenye ukusanyaji wa mapato yake ya ndani na kutumia fedha hizo kutekeleza miradi ya maendeleo.


Akizungumza wakati akifungua mkutano mkuu wa Mikaleli Ye Wanyausi (umoja wa Wagogo), Desemba mwaka jana, Ndugai alisema, mikopo inayochukuliwa na serikali kupitia mashirika hayo, yaweza kusababisha siku moja “nchi kupigwa mnada.”

Aliongeza: “Mama (Rais Samia), amekwenda kukopa Sh. 1.3 trilioni. Tunapiga makofi nchi nzima. Tunawapa Wazungu Sh. 10 trilioni, riba tupu, wanatufanya mazezeta. Hela yako mwenyewe, anachukua hela yako, anakupa kidogo halafu unashangilia. Toza tozo, fanya hivi tujitegemee, tusimame wenyewe…”

Alisema, “…ninyi si wasomi? Mwaka 2025, mtaamua wenyewe muwachague wanaopenda kukopakopa au wanaotaka tujitegemee.”

Baadaye mwanasiasa huyo aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kusema, “…nimekosa mimi, nimekosa sana, nisameheni Watanzania.” Hakuishia hapo, akamuomba msamaha Rais Samia Suluhu Hassan na kudai kile kinachoonekana kutoka mdomoni mwake, kilitengenezwa na vyombo vya habari.

Mara baada ya kauli hiyo, Rais Samia aliibuka na kumshambulia Ndugai kuwa amepotosha umma. Tofauti kati ya Ndugai, ambaye pia ni mbunge wa Kongwa, mkoani Dodoma na Schoenbach, ni kwamba mmoja alielewa kosa lake mapema na hivyo kuamua kujiuzulu kwa hiari, wakati mwingine alichukua hatua hiyo, baada ya kutukanwa na kushambuliwa kila kona.


 
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba, ameikosoa hatua ya Ujerumani kukataa kupeleka silaha nchini humo na kuitaka nchi hiyo, kuacha “kuudhofisha umoja” katikati ya hofu ya Urusi kuivamia Ukraine.
Wito wa Ukraine kwa nchi washirika wa Magharibi kuimarisha uwezo wake wa ulinzi umepokelewa na Marekani, Uingereza na mataifa ya Baltic kwa kukubali kupeleka silaha nchini humo, zikiwemo za kujikinga na mashambulizi ya vifaru vya kijeshi.

Mapema juzi Jumamosi, Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Christine Lambrecht alisema, nchi hiyo haina mpango wa kuipatia silaha Ukraine katika mzozo unaondelea kati yake na Urusi. Lakini akasema, serikali ya Ujerumani itaendelea kuiunga mkono nchi hiyo dhidi ya kitisho kutoka Urusi.

Kuleba aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba kauli ya Ujerumani kuhusu kutoweza kuipatia silaha za ulinzi Ukraine, hazilingani na hali ya sasa ya kiusalama.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad