Ni Mnyukano wa Mawakili, Shahidi Kesi ya Kina Mbowe



Dar es Salaam. Mawakili wanaomtetea Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu wanaokabiliwa na kesi ya ugaidi, jana walichuana vikali na shahidi wa 11 wa Jamhuri kuhusu upatikanaji na utunzaji wa vielelezo vilivyopatikana kwa washtakiwa.

Mawakili hao, Dickson Matata na Peter Kibatala (kiongozi wa jopo) walimbana shahidi huyo, askari mpelelezi Goodluck Minja wakati wa maswali ya dodoso kuhusu ushahidi alioutoa Ijumaa iliyopita.

Wiki iliyopita, askari huyo, pamoja na mambo mengine, alitoa ushahidi uliolenga kujenga mnyororo wa uhifadhi wa vielelezo vinavyohusishwa na washtakiwa, moja ya kigezo cha msingi cha kuthibitisha hatia.

Katika kesi hiyo hoja ya mnyororo wa utunzaji wa vielelezo imekuwa ikiibuliwa mara kwa mara na hivyo kuibua mvutano mkali na malumbano ya hoja za kisheria kati ya mawakili wa utetezi na waendesha mashtaka.


Shahidi huyo kutoka idara ya upelelezi mkoa wa Arusha alieleza kuwa ndiye aliyepewa vielelezo vilivyokutwa kwa washtakiwa ikiwemo bastola, dawa zinazodhaniwa za kulevya pamoja na simu baada ya upekuzi.

Baada ya maswali hayo, waendesha mashtaka, mawakili wa Serikali waandamizi, Pius Hilla na Robert Kidando (kiongozi) walimhoji shahidi huyo kwa lengo la kutoa ufafanuzi wa kusawazisha baadhi ya hoja zilizoibuliwa katika maswali ya mawakili wa utetezi.

Baada ya hatua hiyo, Kidando aliieleza Mahakama kuwa hawakuwa na shahidi mwingin, kwani shahidi waliyemtegemea amepata udhuru na ameshindwa kusafiri, hivyo aliomba ahirisho la kesi hadi kesho.


Wakili Kibatala aliwataka upande wa mashtaka watambue washtakiwa wanasubiri kujua hatima yao na akahoji kama wangekuwa ni ndugu zao au wao wenyewe wangejisikiaje.

Alipoulizwa na Jaji kuhusu maombi ya kuahirisha alijibu kuwa wanaiachia Mahakama. Hivyo Jaji Joachim Tiganga anayesikiliza kesi hiyo alitoa amri kwa upande wa mashtaka kuhakikisha wanakuwa na shahidi na akaahirisha kesi hiyo hadi kesho.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo inayosikilizwa Mahakama Kuu Divisheni ya Maosa ya Rushwa na Uhjumu Uchumi ni Halfan Bwire Hassan, Adamu Hassan Kasekwa na Mohamed Abdillahi Ling’wenya.

Washtakiwa hao watatu walikuwa askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Kikosi maalumu, maarufu kama kikosi cha makomando kilichopo Sangasanga, Ngerengere mkoani Morogoro walioachishwa kazi kwa nyakati tofauti kwa sababu za kinidhamu.


Washtakiwa wote wanakabiliwa na mashtaka sita, ya kula njama kutenda vitendo vya kigaidi, kushiriki vikao vya kupanga vitendo vya kigaidi kwa lengo la kuibua hofu miongoni mwa wananchi wa Jamhuri ya Tanzania yanayowakabili washtakiwa wote na kufadhili vitendo vya kigaidi (kwa Mbowe peke yake).

Mashtaka mengine ni kukutwa na vifaa vya kutekelezea vitendo vya kigaidi kama vile sila (bastola kwa Kasekwa, sare vifaa vingine vya JWT na za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa Bwire.

Vitendo hivyo vya kigaidi wanavyotuhumiwa ni kutaka kulipua vituo vya mafuta na maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi na kuhamaisha maandamano yasiyokoma katika miji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Mbeya.

Vingine ni kukata miti na kuiweka barabarani na kutaka kumdhuru aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hai, Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya.


Wanadaiwa kula njama za kutenda vitendo hivyo kwa nyakati na mahalitofautitofauti mwezi Agosti, 2020, katika mikoa ya Kilimanjaro, Dar es Salaama na Morogoro.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad