Ni Shida...Utabiri wa Godbless Lema Unavyotimia na Kutesa Viongozi

 


Dar es Salaam. Usithubutu kutabiriwa na aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema. Ndivyo inavyojionyesha baada ya kile alichokitabiri kutimia kwa baadhi ya watu waliowatabiria.


Lema amekuwa akiandika utabiri wake kwenye mtandao wa Twitter na wakati mwingine kuzungumza kile anachodai ameoteshwa na Mungu juu ya hatima ya viongozi anaowatabiria mambo mbalimbali.


Mwanasiasa huyo ambaye kwa sasa anaishi uhamishoni Canada, amekuwa akihusisha utabiri wake na vitendo vya ukiukaji wa demokrasia na matumizi mabaya ya madaraka unaofanywa na viongozi dhidi ya baadhi ya wananchi.


Tabiri zake zimekuwa zikipokelewa kwa maoni tofauti, ambapo baadhi ya watu wanadhani ni kelele za kawaida za upinzani, wakati wengine wakimwamini hasa kutokana na kutimia kwa yale anayoyasema.


Moja ya utabiri wake ni alioutoa mwaka 2016 aliposema kwamba Rais wa wakati huo, Hayati John Magufuli atafariki kwa kile alichodai Serikali iliyokuwa chini ya kiongozi huyo imeumiza watu.


Kutokana na utabiri huo, Lema alikamatwa na kushikiliwa mahabusu kwa miezi minne kwa kosa la uchochezi kutokana na matamshi yake.

Hata hivyo, Novemba 11, 2016 wakati akiachiwa kwa dhamana, Lema aliendelea kusisitiza utabiri wake kwamba mkuu huyo wa nchi hangefika mwaka 2020.


Kama vile kutimia kwa utabiri huo, Machi 17, 2021, Watanzania walipokea taarifa za kifo cha kiongozi huyo, likiwa ni tukio la kwanza katika taifa hili kwa kiongozi wa nchi kufariki akiwa madarakani.


“Huyu jamaa (Lema) huwa nafuatilia kwa karibu kila anachosema, tumeona baadhi ya maneno yake yametimia. Haya mambo siyo ya kubeza, ni kuyasikiliza kwa makini,” alisema Yusuf Mrisho, mkazi wa Gongolamboto.

Spika Ndugai

Kama vile haitoshi, Lema aligeuzia utabiri wake kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai akisema ana ujumbe wake kutoka kwa Mungu, huku akimtaka akamwone ili amweleze lakini akidharau naye yatamfika.


Machi 18, 2020, Lema aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter akisema: “Spika Job Ndugai, nina ujumbe wako kutoka kwa Mungu, wewe pamoja na wenzako kadhaa. Unatakiwa kunitafuta haraka nikueleze.


“Unaweza kuchagua kudharau, lakini ukinisikiliza na ukaheshimu ujumbe, utaishi, lakini ukifanya shingo kuwa ngumu, hamtadumu. Mungu ameamua kulisaidia taifa bila vita,” aliandika Lema, siku moja baada ya kifo cha Rais Magufuli.


Mei 3, 2021, aliandika tena: “Acheni kuumizwa na matendo ya Spika Job Ndugai, Mungu anatarajia kutenda muujiza hivi karibuni kwake, asiwachoshe kabisa, kwani imeandikwa, Mithali 16:5 – Mungu huwachukia wote wenye kiburi cha moyo. Uwe na hakika kwa hili. Hawataepuka kuadhibiwa,” aliandika Lema.


Unaweza kusema utabiri wa Lema wa Mei 3, 2021 ulitimia Januari 6 baada ya Ndugai kujiuzulu nafasi ya Spika wa Bunge kutokana na kauli aliyoitoa Desemba 26, 2021 akipinga Serikali kukopa nje kwa madai kuwa itasababisha nchi ipigwe mnada, hivyo akashauri iwabane watu kwenye tozo mbalimbali.


Ndugai, ambaye amekuwa mwiba kwa watu mbalimbali, alishinikizwa kujiuzulu nafasi hiyo na watu tofauti kwa sababu walidai asingeweza kufanya kazi na wabunge ambao wanamuunga mkono Rais Samia.


Utabiri kwa Sabaya


Lema aliendelea kutabiri ambapo mwaka 2019 alizungumza kwa njia ya simu na aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na kumweleza kwamba siku moja atakuja kulipa kutokana na matendo yake ya kuumiza watu na kuwapora fedha.


“Acha kujipendekeza kiasi cha kuumiza watu, there is karma, one day you gonna pay it (siku moja utalipa). Haya mambo unayofanya kuna siku you will pay (utalipa), acha kufanya haya mambo unayofanya,” alisema Lema kwenye mazungumzo yake na Sabaya kwa njia ya simu.


Mei 13, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan alitengua uteuzi wa Sabaya na siku mbili baadaye alikamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zilizokuwa zikimkabili na Oktoba 15 mwaka jana, Mahakama ilimkuta na hatia na kumhukumu kifungo cha miaka 30 jela.


Licha ya kukata rufaa kwenye hukumu hiyo, Sabaya bado anasota gerezani wakati mashauri yake mengine yakiendelea kusikilizwa Mahakamani huko Arusha na bado hatima yake haijulikani hadi sasa.


“Ukisikiliza ile clip yake (Lema) na Sabaya, utaona kwamba akisema jambo linakuwa. Huwa namfuatilia sana Twitter, ukisoma unacheka lakini baadaye unashangaa yanatokea kweli,” alisema mkazi wa Tabata, Chrispin Jumanne.

Kushughulikiwa wapinzani

Wakati wa Bunge la 11, Lema alitabiri pia kwamba Serikali ikimaliza kuwashughulikia wapinzani, itawashughulikia pia wabunge wa CCM kwa utaratibu uleule, kwa maana ya kwamba watabaki wanashughulikiana wenyewe kwa wenyewe.


“Nyie mnafikiri ni kwetu tu, wakishamaliza kutushughulikia sisi, meno yaleyale, msumeno uleule, utakuja upande wenu. Ngoja watumalize kwanza watakuja upande wenu na ninawaambia, kila mbegu mnayopanda mtavuna, tuko kushuhudia haya na Mungu ni shahidi,” alisema Lema bungeni.


Wakati Lema akisema hayo baadhi ya wabunge wa CCM walikuwa wakiona ni maneno ya kawaida waliyoyazoea kuyasikia kutoka kwake au kwa wapinzani ambao walionekana wanabanwa kufanya siasa.


Hata hivyo, baadaye utabiri huo wa Lema ulionekana ukitimia baada ya baadhi ya wabunge na makada wa CCM kushughulikiwa kutokana na kile kilichotajwa ni mwenendo usiofaa ndani ya chama hicho na bungeni.


Miongoni mwa walioonja joto la kushughulikiwa ni mbunge wa Mtama, Nape Nnauye, aliyekuwa mbunge wa Igunga, Dk Dalaly Kafumu na aliyekuwa mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia


Juni 2018, Nape Ghasia walisema hawakubaliani na mapendekezo ya Serikali ya kufuta ushuru wa asilimia 65 wa fedha zinazotokana na mauzo ya korosho nje na kubainisha kuwa kinachofanywa ni kuiua CCM mikoa ya Kusini.


Sakata la Ndugai na Rais Samia ni moja ya mifano inayodhihirisha kwamba wanashughulikia wenyewe kwa wenyewe, ukienda bungeni pia utaona wabunge kadhaa kama Humphrey Polepole, Josephat Gwajima na Jerry Silaa wamechukuliwa hatua za kinidhamu kwa sababu ya mitazamo yao tofauti.


Mtifuano umehama kutoka kambi ya upinzani na sasa ni vigogo wa CCM.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad