NIT kuanza kutoa kozi ya urubani, gharama Sh70 milioni




Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam alipotembelea Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).
Dar es Salaam. Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimesema kipo katika hatua za mwisho kukamilisha mchakato wa kuanza kufundisha kozi ya urubani wa ndege inayotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwaka huu na itagharimu Sh70 milioni.

Kimesema kuwa kati ya fedha hizo Sh21 milioni ni gharama za kozi hiyo ngazi ya awali ambayo itamuwezesha mwanafunzi kusoma masomo ya awali na kuruka angani saa 50.

Hayo yamebainishwa leo Jumatano Januari 26, 2022 na Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Zacharia Mganilwa wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete aliyekitembelea chuo hicho kujifunza mambo mbalimbali.

Profesa Mganilwa amesema mwanafunzi wa ngazi ya awali akihitimu na kupata leseni yake ya kurusha ndege za watu binafsi atapaswa kuendelea kusoma tena miaka miwili na nusu ili kuweza kupata leseni ya biashara ya CPL ambayo itafanya gharama ya kozi hiyo kuwa jumla ya Sh70 milioni.


 
"Mwanafunzi huyu akiwa na jumla ya Sh70 milioni atasoma masomo hayo ya awali na hayo mengine yatakayomuwezesha kupata leseni ya CPL ambayo itamuwezesha kuruka saa 200 na kufanya masomo mbalimbali ya hali ya hewa, baada ya hapo muhitimu huyu ataweza kuajiriwa na mashirika ya ndege ya kibiashara ila atatakiwa kuanza na ndege ndogo zenye uwezo wa kubeba abiria 70," amesema na kuongeza

"Hata hivyo baada ya hapo atatakiwa kusoma tena kidogo ili apate leseni inayoitwa ATPL akipata hiyo anaweza kuendelea kusoma zaidi hadi kufikia hatua ya kuendesha ndege aina ya Dreamliner," amesema Profesa Mganilwa

Profesa Mganilwa amesema wanamatumaini kuwa kabla ya mwaka huu kuisha kozi hiyo itakuwa imeanza rasmi hivyo wanafunzi wa kitanzania wataanza kuipata elimu hiyo ya urubani hapa nchini.

Amesema ili kozi hii ianze lazima wapate ithibati kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) hivyo katika mchakato wa kupata kibali hicho wapo kwenye hatua ya nne ambayo inawataka wawe na ndege ambazo amebainisha kuwa tayari Serikali imenunua ndege mbili zinazogharimu Dola za Marekani 600,000 sawa na Sh1.2 bilioni kwa kila moja.

"Ninaimani tutapata kibali hiko kwa sababu malipo ya awali ya ndege hizo tayari yameshafanyika, matarajio ni kwamba mwezi wa saba au wa nane ndege hizo zitafika hapa nchini, lakini pia walimu wapo, mitaala tunayo yaani kila kitu kimekamilika kwa maana maandalizi upande wa kwetu umekamilika," amesema Profesa Mganilwa

Kwa upande wake Naibu Waziri Mwakibete amesema kuwa mipango waliyonayo NIT kuanza kufundisha marubani ni mizuri na inalengo la kupata wataalamu wakutosha.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad