Nyoka wa Kichawi Asimamisha Mradi wa Sh. 99 Bilioni Tanga

 


Nyoka mkubwa anayesadikika kuwa ni wa kishirikina ametajwa kuwa moja ya sababu ya mradi wa maji wa Sh. 99 Bilioni katika Wilaya ya Handeni Mkoa wa Tanga kusimama.


Hayo yamebainishwa wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Tanga ilipotembelea mradi huo na kuzungumza na watekelezaji.


Kulwa Juma, ambaye ni simamizi wa mradi huo kutoka Kampuni ya Civil Loths Construction LTD inayotekeleza mradi aliiambia Kamati kuwa wafanyakazi wamekuwa wakiripoti kuona mauzauza wakati wakifanya kazi, ikiwa ni pamoja na uwepo wa nyoka mkubwa anayetokea na kupotea.


Alisema kuwa wafanyakazi hao wanadai kuwa nyoka huyo amekuwa akiifuatilia nyuma ‘greda’ wakati wakiendelea na kazi.


Aidha, Msimamizi huyo aliongeza kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakilalamika wakidai hawajalipwa fidia ya kuupisha mradi. Hivyo, wananchi hao wamekuwa wakitishia kuwa mradi huo hautakamilika kama hawatapata haki yao.

Vilevile, alisema wamekuwa wakipata changamoto zaidi ya vifaa kuharibika muda mfupi baada ya kuanza kazi, katika mazingira ambayo wanaamini sio ya kawaida kutokana na uzoefu wao katika kazi hiyo.


Akizungumza baada ya kusikiliza maelezo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Siriel Mchembe aliilaumu Wakala wa Maji na Usafi na Mazingira (Ruwasa) kwa kuchelewesha malipo ya fidia kwa wananchi ambayo ni Sh. 15 Milioni.


Hivyo, Aliutaka uongozi wa Ruwasa kuwatendea haki ‘wazee’ kwa kuwalipa fidia ili mambo yaendelee.


“Hivi kweli Ruwasa Sh.15 milioni tunajadili mpaka leo, na mbaya zaidi sasa wazee wale kila siku wanaahidiwa na wanatafuta maeneo mengine ya kulima sasa hawana maeneo na hawana fedha,” alisema Mkuu huyo wa Wilaya.

“Inawezekana ni maruweruwe au ni hofu, mi sijayaona wao ndio waliyoyaona kwa hiyo mi sitaki kuyasemea lakini ninachotaka kusema badala ya kuanza kuwalaumu wazee kuwa kuna maruweruwe tuanze kwanza, wazee wamekosewa na wameonewa na Ruwasa,” aliongeza.

Alisema mradi huo ulitarajiwa kukamilika Februari 16, 2022 na utawafaidisha wananchi 28,735 wa kata sita za Wilaya hiyo, lakini hadi sasa hakuna dalili.

Kamati hiyo iliagiza changamoto zote zilizobainishwa zinazopunguza kasi ya kukamilika kwa mradi huo zishughulikiwe haraka.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad