Kilombero. Baadhi ya wananchi katika katika kata ya Kalengakelu Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro hawana sehemu ya kuishi baada ya nyumba 21 na madarasa matatu ya shule ya msingi Kalengakule kuezuliwa na upepo.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Jumapili Januari 2, 2022 Mkuu wa Wilaya ya Kilombero (DC), Hanji Godigodi amethibitisha kutokea tukio hilo.
Amesema kuwa mpaka sasa hakuna taarifa za watu kupoteza maisha
“Ni kweli nyumba 21 zimeezuka lakini hakuna mtu aliyepoteza maisha” amesema DC Hanji
Amesema kuwa upepo huo umeezua madarasa matatu na ofisi moja ya walimu.
“Kwa upande wa shule kuna madarasa matatu na ofisi, vitabu vilivyokuwemo mule hakuna kilichoharibika” amesema
Mkuu wa Wilaya ameagiza wataalamu kufanya tathimini ya haraka kwa kushirikiana na kamati za maafa za kata na vijiji ili wananchi wapate msaada.