Selina Chacha, mkazi wa Kitunda Nyantira jijini Dar es Salaam akilia mbele ya nyumba yake iliyobomolewa Januari 6, 2021 kwa kile kinachodaiwa kuwa nyumba hiyo iliuzwa kwa njia ya mnada bila yeye kujua. Picha na Aurea Simtowe
Dar es Salaam. Familia moja jijini hapa imejikuta ikilala nje kwa kukosa makazi baada ya nyumba yao kuvunjwa na vitu kutupwa nje.
Hiyo ni kutokana na kile kilichosadikika nyumba hiyo iliuzwa zaidi ya miaka 10 baada ya baba mwenye nyumba, Nyahure Range (mmiliki) kudaiwa kushindwa kulipa Sh300,000 katika mkopo wa Sh3 milioni aliochukua katika chama cha akiba na mikopo cha Kitunda.
Mwananchi ilifika eneo la Kitunda Nyantira, Januari 6 na kukuta vitu vya nyumba hiyo vikiwa nje, huku majirani wakimfariji mama wa nyumba hiyo, Selina Chacha aliyekuwa akiomboleza.
“Yaani Sh9 milioni zinaniweka mimi na watoto watano nje, si wangeniambia mapema nisingeshindwa kulipa fedha hizo kidogo kidogo,” alisema mama hiyo huku akilia.
Selina alisema miaka yote ambayo inasadikika nyumba yake kuwa na kesi mahakamani hakufahamu na alipata taarifa rasmi Oktoba, 2021 alipopokea samasi ya utekelezaji wa hukumu iliyotolewa.
Alisema alikwenda Mahakama ya Ardi Ilala ambako aliambiwa mumewe alishindwa kulipa deni la Saccos, jambo lililofanya nyumba kuuzwa kwa njia ya mnada.
“Nikawaambia sikujui na wala sijawahi kusaini fomu yoyote, nikaomba mwenendo wa kesi nikapewa, sikuona hata ni shilingi ngapi alikopa wala vielelezo vilivyotumika. Nikachukua mwenendo huo nikaenda kufungua kesi Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi,” alisema.
Alisema baada ya kufungua kesi alipeleka barua ya kusimamisha utekelezaji wa hukumu hiyo na kesi mpya ikawa ikiendelea na hukumu ilitarajiwa kutolewa Februari 15, 2022.
“Jana (Januari 6) nikiwa mjini, mdogo wangu alinipigia simu na kuniambia nyumba inavunjwa. nikamwambia awaambie waache kwa sababu kesi bado iko mahakani, lakini hawakumsikiliza,” alisema.
Alisema alikwenda kuripoti tukio hilo polisi, lakini aliambiwa kuwa wao walipewa mamlaka ya kufanya hivyo na mahakama.
“Watoto hawa watano wote wanatakiwa kwenda shule, wanaendaje kwa mazingira haya? Hata kama ni haki, hii nyumba ilikuwa ni ya zaidi ya Sh400 milioni na si kwa bei iliyouzwa,”
Eneo ambalo nyumba hiyo ipo linakadiriwa kuwa na zaidi ya ekari moja, huku pembeni kukiwa na bustani kubwa ya mbogamboga na mabanda ya kuku zaidi ya 10 ambayo baadhi yana vifaranga na mengine kuku wakubwa.
“Kama ni hela hiyo walikuwa wanataka si wangeniambia, ningekata eneo nikauza, ili nilipe deni hilo kuliko kuvunja nyumba hii na baadhi ya mabanda,” alisema mama huyo.
Hata hivyo, kwa mujibu wa barua ya Kabango General Business iliyotolewa Novemba 23 mwaka jana inaonyesha watu hao walitakiwa kutoka katika nyumba hiyo siku 14 tangu barua ilipotolewa na kukamata mali, ili kufidia Sh9.9 milioni kama ilivyoamriwa.
Pia barua hiyo ambayo imetoka kwa dalali wa baraza la ardhi na nyumba Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam inaeleza endapo familia hiyo ingeshindwa kutoka, wangetolewa na kukamata mali kwa mujibu wa sheria na taratibu za baraza bila kuwapo taarifa nyingine.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, nyumba hiyo ni mali ya Nicodemus Mrosso ambaye alinunua na aliwataka watu hao kuondoka na kumuachia eneo lake.
Mwananchi ilimtafuta Mrosso ili kuthibitisha uhalali wa umiliki wake na ikiwa aliagiza kubomolewa nyumba huyo, lakini liliishia kumpata aliyekuwa mwanasheria wake wakati wa kusimamia kesi hiyo.
“Nilisimamia kesi hii na Mrosso alishinda, kilichokuwa kimebaki ni kukazia hukumu. Suala la kubomolewa nyumba sijui chochote,” alisema Mwanasheria huyo ambaye hakutaka kutaja jina.
Alisema kila kitu kilifanyika kwa mujibu wa sheria, wahusika walitakiwa kusema kila kitu kuhusu kesi hiyo. Hata alipoulizwa shauri hilo la madai lilianza lini aligoma kulizungumzia.
Mmoja wa wafanyakazi wa Kitunda Saccos alisema alipoanza kufanya kazi katika ofisi hiyo mwaka 2012 aliikuta kesi hiyo ya madai.
Deni lilivyoanza
Mwananchi ilimtafuta Nyahure, baba wa familia hiyo aliyepoTarime tangu mwaka 2020, ambapo alikiri kukopa katika chama hicho Sh3 milioni, lakini alieleza alilipa deni lote.
Hata hivyo, alisema mwaka 2011 aliletewa tangazo kutoka chama hicho akidaiwa Sh300,000 ambayo aliuliza inatoka wapi bila kupewa ufafanuzi.
“Katika kesi niliyofungua mwaka 2011 dhidi ya Kitunda Saccos, nilipeleka vielelezo vyote kuwa sidaiwi, ila wao walishindwa kuleta vielelezo kuwa wananidai na hadi mwaka 2013 shauri lilifungwa maana nilikuwa napeleka samasi kila wakati, lakini hawatokei mahakamani,” alisema Nyahure.
Alisema tangu hapo hakuwahi kusikia kitu chochote kinachohusu mkopo huo hadi alipopigiwa simu juzi akielezwa kuwa nyumba imevunjwa.
Baadhi ya nyaraka ambazo Mwananchi ilionyeshwa kwa vipindi tofauti, Nyahure alikuwa akipelekewa samasi hizo wakati mwingine hadi nyumbani kwake na kuzikataa huku wakati mwiingine wakimkosa bila mkewe kujua.